PUMZI YA MOTO: Objective Football ilivyokufa Kifo cha Diagonal Football

KAULI ya Mwenyekiti wa Bodi ya Klabu ya Simba, Salim Abdallah maarufu kama Try Again kuhusu pongezi za Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa soka safi kuliko lililokuwa likitembezwa na Mamelodi Sundowns na Wydad Casablanca katika mechi ya fainali ya African Football League ni moja kati ya vichekesho vya miaka yote vya Klabu ya Simba.

Simba SC ni klabu yenye vichekesho vingi sana. Unakumbuka kauli ya mtendaji wao mkuu aliyepita, Barbara Gonzalez, kwamba Al Ahly wanatamani kucheza kama Simba? Basi hiyo ndiyo Simba sasa.

Hebu tuachane na hayo nataka kujadili kichekesho cha uwanjani. Aina mpya ya uchezaji ya klabu hiyo ambayo huvuma ghafla na kufia mikononi mwa Yanga. Yaani namaanisha soka la Kibrazili ambalo kocha wao aliyepita, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliliita Objective Football yaani soka la malengo na mashabiki wao pamoja na meneja wao wa habari, Ahmed Ally walilipigia chapuo sana.

Hii siyo mara ya kwanza kwa klabu hiyo kuja na mbwembwe za aina hiyo na baadaye kuishia mikononi mwa Yanga. Mwaka 1983, Simba ilikuja na aina ya uchezaji kutoka Brazil waliyoiita Diagonal Football.

Aina hii ya uchezaji waliipata Brazil ambako walikwenda kukaa siku 45 wakijiandaa na msimu mpya wa ligi ya 1983. Ziara hiyo iliwezeshwa kwa hisani kubwa ya Said Salim Bakhresa ambaye sasa ana timu yake ya Azam FC.

Wakati huo ‘Mnyama’ alikuwa na makocha wawili wa Kibrazili Dk Edil Silva na Paolo Nizzo. Jumamosi ya Januari 15, 1983 Simba walirejea nchini tayari kuuanza msimu mpya ambao ulitakiwa kuanzia Januari 22, mwaka huo.

Viongozi wa Simba, chini ya Katibu Mkuu Ismail Aden Rage ulitamba kwamba umekuja na mtindo mpya unaoitwa DIAGONAL FOOTBALL na timu zijiandae kuteseka kwelikweli. Siku 45 Brazil siyo mchezo, watu wakiamini kwamba Simba ikirudi hapa itakuja na Samba la kina Zico, Socrates, Tostao na kadhalika.

Katika vitu vyote ambavyo watu walisubiri ni kuona Simba ikilipa kisasi kwa CDA ya Dodoma ambayo mwaka mmoja nyuma yaani 1982, iliifunga Simba mabao 6-1 katika pambano lililofanyika kwenye uwanja mpya wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Hiki kilikuwa kipigo cha fedheha sana kwa Simba na kila mtu hasa shabiki wa Simba alitamani Diagnal Football iiishushie CDA hata mabao 10 kwa hasira. Na ratiba iliipa nafasi ya kulipa kisasi kwani ndiyo timu waliyopangwa nayo kufungua msimu.

Katika mchezo huo uliofanyika Januari 22 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, Simba ilishinda mabao 2-0 tu. Mashabiki wa Simba hawakufurahia ushindi huu mdogo, lakini zaidi hawakuridhika na Diagnal Football waliyoisubiri kwa hamu.

Simba ilicheza vibaya na kusababisha kuchekwa sana na mashabiki wa Yanga. Diagnal Football iliendelea hivyohivyo kwa kusuasua lakini kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tumbaku ya Morogoro.

Katika mchezo wa tatu, Simba ikienda Songea kucheza na Majimaji, ngoma ikaisha suluhu. Diagnal Football kwa mara ya kwanza ikashindwa kuzaa bao.

Hofu ikawaingia mashabiki wa Simba kwani mchezo uliokuwa ukifuata ulikuwa dhidi ya Yanga ambayo ilionyesha kiwango kizuri ikiwemo kuwafunga mabingwa watetezi, Pan Africa, ambayo ilikuwa timu bora sana mwaka huo na ikishiriki Klabu Bingwa Afrika.

Hadi hapo, Yanga ilikuwa kileleni na alama 18 huku Simba ikiwa katika nafasi ya tatu kwa alama 11, moja nyuma ya Majimaji ya Songea iliyokuwa nafasi ya pili. Pambano dhidi ya Yanga lilifanyika Februari 10, 1983 na kumalizika kwa suluhu (0-0). Suluhu haikuwa stori kubwa, bali kiwango kibovu cha Simba siku hiyo.

Kama utaukumbuka mchezo wa Simba na Yanga wa Septemba 30, 2018 ambao kipa Beno Kakolanya aliiokoa Yanga ya Mwinyi Zahera, basi ifanye kinyume chake. Mateso waliyopata Yanga uwanjani siku ile ndiyo waliyoyapata Simba 1983.

Kwa timu iliyokaa Brazil siku 45 ikiwa na Diagnal Football kuteseka namna ile halikuwa jambo lenye kupendeza. Uongozi wa Simba ukaamua kuwafuta kazi makocha wale wa Kibrazil na huo ndiyo ukawa mwisho wa Diagnal Football.

Zaidi ya hapo, huu pia ndiyo ukawa mwisho wa Said Salim Bakhresa ndani ya Simba, kwani sare hiyo iliwauma sana mashabiki wa Simba ambao walitegemea makubwa kutoka kwa timu yao iliyokuwa Brazil kwa siku 45.

Kwa hiyo baada ya haya matokeo, mashabiki wakaanza kumtukana Bakhresa kwamba alijifanya kuipeleka Simba Brazil wakati hakuna kilichobadilika. Anajifanya ana hela huku anauza chapati. Maneno haya yakamkera na kujitoa Simba na hajarudi hadi sasa.

Mkasa huo wa Diagnal Football unataka kufanana na huu wa Objective Football wa Robertinho Oliveira kutoka Brazil. Kocha huyo aliyekuwa na timu kambini nchini Uturuki na kusababisha vyombo vya habari nchini kuitabiria Simba kucheza pira Ottoman, alikuja na msemo wake wa Objective Football akielezea namna timu yake inacheza.

Watu wengi walikuwa wakikosoa namna timu hiyo inavyocheza hata kama inashinda, ukizingatia historia ya Simba ilishawahi kumfukuza kocha Moses Basena kutoka Uganda, siyo kwa matokeo mabaya bali soka butuabutua.

Kwa hiyo Objective Football ya Robertinho iliwatia shaka wengi. Lakini Simba wenyewe kupitia meneja habari wao wakawa wanajinasibu na Objective Football huku yeye akilinogesha kwa kuliita pira kokoto.

Simba wakaanza ligi kwa mwembwe wakishinda mechi zote za kwanza. Ligi ya Mabingwa Afrika wakafuzu hatua ya makundi. Kwenye African Football League wakatolewa kwa sheria ya bao la ugenini na timu namba moja kwa ubora barani Afrika, Al Ahly ya Misri.

Hii iliendelea kuwapa jeuri ya kulipamba pira malengo la Robertinho, lakini hali haikuwa hali pale walipokutana na Yanga. Kipigo cha 5-1 kikaharibu kila kitu. Robertinho, kama Wabrazil wenzake wa 1983 akafungashiwa virago.

Objective Football kama Diagnal Football ya 1983 ikageuka kituko. Na bila shaka itakufa kama vile.

Kama nilivyoanza kule juu kwamba Simba ni klabu inayoongoza kwa vichekesho, ili kuzima mjadala wa Objective Football wakaja na uzinduzi wa chaneli ya Whatsapp na sifa za kucheza boli linalovutia zaidi  walizodai kupewa na Rais wa Fifa, Gianni Infantino.