Polisi vs Simba usiyotarajia yalitokea

MOSHI. Polisi Tanzania FC ilipata alama moja dhidi ya Simba juzi, tangu ilipopanda Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/20 baada ya kutoka suluhu kwani katika michezo mitano ambayo timu hizo zimekutana kabla ya hapo timu hiyo imepoteza yote.
Katika mchezo ambao uliopigwa kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi ilikuwa shoo ya kibabe kwa timu hizo ambazo zilikuwa zinahitaji ushindi kila moja na Simba walihitaji zaidi kushinda ili kupunguza pengo la alama dhidi ya vinara, Yanga huku Polisi wakitaka kufuta uteja wa kupoteza kila mara mbele ya Wekundu wa Msimbazi.
Mwanaspoti lilikuwapo uwanjani na hapa linakupa kile kilichojiri ndani ya dakika 90 za mchezo huo uliouacha kila pande na jambo la kukumbuka.
NYOMI MAPEMA TU
Licha ya kiingilio kuwa Sh10,000 kwa mzunguko na Sh20,000 jukwaa kuu, huku ikidhaniwa labda idadi ya watazamaji ingepungua, lakini hali ilikuwa tofauti kwani ilishuhudiwa mapema tu saa saba za mchana uwanja ukiwa umependeza kwa kuwa na nyomi ya maana.
Idadi kubwa ya mashabiki wengi walikuwa wa Simba waliokuwa na matumaini makubwa timu yao kushinda kutokana na rekodi yake dhidi ya Polisi Tanzania.
POLISI TZ YAJILIPUA
Unaweza kusema Polisi Tanzania ilijilipua kutokana na mabadiliko ambayo ilifanya katika kikosi kwani ilikuwa tofauti na michezo miwili ya ligi iliyocheza dhidi ya Azam FC na Ruvu Shooting, ambapo waliingia vijana wa kazi waliopambana kubakisha alama moja.
Licha ya kukosekana kwa Said Makapu katika eneo la ulinzi hakukuwa na shida kwani ukuta ulijengwa imara na Datius Peter, Yahya Mbegu, Mohammed Mmanga, Hussein Bakari na Tariq Simba uliowafanya washambuliaji na mawinga wa Simba walioongozwa na Meddie Kagere, Chris Mugalu, Yusuph Mhilu na Rally Bwalya kutii sheria bila shuruti.
Hata walipoingia kina Ousmane Shakho, Clatous Chama, Bernard Morisson na Jimmyson Mwanuke walihitaji kutafuta anga lao spesho la kupita ili wakamsalimie mlinda lango Metacha Mnata ambaye naye alikuwa katika kiwango bora.
DEUS VS MZAMIRU
Kiungo Deus Cosmas akiwa katika kiwango bora mbele ya viungo wa Simba, operesheni yake katikati ya uwanja eneo la uchezeshaji iliwavuruga pasi kali, huku ‘akikata umeme’ ambapo kama washambuliaji wa Polisi Tanzania wangekuwa makini, basi wangeondoka na ushindi kwani aliwatengenezea nafasi mbili za wazi, lakini wakashindwa kuzitumia.
Hata hivyo, Simba nayo ilikuwa na Mzamiru Yassin ambaye aliisumbua Polisi akihahaha uwanja mzima, ambapo hata hivyo kuna nyakati alijikuta anatulizwa na Deus, jambo lililomfanya kocha Pablo Franco kumbadilisha dakika ya 60 na nafasi yake kuchukuliwa na Jonas Mkude.
HARUNA VS KAPOMBE
Winga Kassim Haruna wa Polisi Tanzania alikuwa na siku bora, akikimbiza eneo la kulia na japo hakuwa na madhara langoni mwa Simba, alimfanya beki Shomary Kapombe asipande mara kwa mara kupiga krosi zenye madhara upande wa Polisi na kwa ubora wa Haruna alimlazimisha wakati mwingine Pascal Wawa asaidiane na Kapombe kumdhibiti.
Hata hivyo, vita ya Haruna na Kapombe ilikuwa kali kwani alihakikisha akishika mpira anatembea na Kapombe.
DAKIKA 90 BILA KADI
Moja kati ya jambo la nadra mchezoni ni mechi kqwisha bila kadi na ndivyo ilivyokuwa baina ya timu hizo, kwani mpaka kipenga cha mwamuzi Fiorentina Zabron kutoka Dodoma kilipopulizwa kuashiria kumalizika kwa mchezo haikushuhudiwa kadi yoyote, licha ya kwamba yalifanyika madhambi 11 kwa Polisi na Simba 18.
PABLO ALIZINGUA KIKOSI
Ilikuwa kama ni sapraizi kwa mashabiki wa Simba ambao walitarajia kuona kikosi kilichosheheni katika mchezo huo kutokana na umuhimu wake, lakini badala yake kocha Pablo alianza na wachezaji wengi ambao wamekuwa wakikosa namba kikosini mara kwa mara.
Katika mchezo huo Pablo alianza na Beno Kakolanya, Kapombe, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Wawa, Erasto Nyoni, Bwalya, Mzamiru, Kagere, Mugalu na Mhilu.
Waliokuwa benchi ni Morisson, Chama, Mkude, Joash Onyango, Shakho huku Aishi Manula, Mohammed Hussein, Sadio Kanoute, Kibu Denis na Taddeo Lwanga walikuwa jukwaani kuwashuhudia wenzao wakipambana.
Baada ya mchezo furaha na shangwe ilitawala kwa mashabiki wa Polisi Tanzania ikiwa ni baada ya kuondoka na alama moja, hali ambayo iliwafanya kuangusha sebene uwanjani wakati upande wa Simba wakiondoka vichwa chini.
HAWA HAPA MAKOCHA
Baada ya mchezo kumalizika kocha wa Simba, Pablo alisema vijana wake walishindwa kucheza vyema kutokana na ubovu wa uwanja, lakini akaweka wazi kuwa kwa sasa wanaangalia mchezo wao wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambao kwao ni muhimu kushinda ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kutinga nusu fainali.
Kwa upande wake, kocha msaidizi wa Polisi Tanzania, Geoge Mketo alisema changamoto iliyokuwa ikikabili kikosi chake ni majeruhi, lakini hivi sasa timu imerudi katika hali waliyokuwa mwanzo na wanaamini watashinda katika uwanja wowote.