Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwa Arne Slot muda si mrefu tutegemee ‘Breaking News’

PAZIA Pict

Muktasari:

  • Ndivyo ninavyoogopa kumuandika Arne Slot kama kocha wa Liverpool. Lakini hadi wakati naandika ni kocha wa Liverpool. Hata hivyo, ni ‘mfu’ ambaye anatembea katika viunga vya Anfield. Amepigwa mechi tisa kati ya 12 zilizopita. Makocha wachache wanaweza kuvuka huu mtego.

NATETEMEKA wakati huu naandika. Nahofia huenda makala hii ikawa imepitwa na wakati. Wakati mwingine haya ndio maisha ya mwandishi wa makala za michezo. Unamuandika mtu kama kocha, lakini wakati makala inatoka gazetini kumbe alishafukuzwa usiku.

Ndivyo ninavyoogopa kumuandika Arne Slot kama kocha wa Liverpool. Lakini hadi wakati naandika ni kocha wa Liverpool. Hata hivyo, ni ‘mfu’ ambaye anatembea katika viunga vya Anfield. Amepigwa mechi tisa kati ya 12 zilizopita. Makocha wachache wanaweza kuvuka huu mtego.

Sir Alex Ferguson aliweza kubadili mambo 1989 wakati alipokaribia kuishusha Manchester United daraja. Baadaye akaibuka shujaa na kuna mnara wake nje ya Old Trafford. Slot ametoka kuchukua ubingwa na anaweza kuwa kocha wa kwanza kufukuzwa msimu mmoja tu baada ya kuipa timu yake ubingwa.

PAZ 01

Kila Liverpool inapoingia uwanjani msimu huu haibadiliki. Inacheza vile vile kama mechi iliyopita. Inafungwa mabao yaleyale kama ya mechi iliyopita. Hatuoni kama wanaweza kubadilika tena na tena.

Miguu ya Virgil Van Dijik imejichokea. Safu ya ulinzi inafanya makosa yaleyale kila mechi na Van Dijik sio yule mbabe ambaye tumemzoea kwa miaka nenda rudi kiasi kwamba tulikuwa tunamfananisha na kina Nemanja Vidic, John Terry na Rio Ferdinand.

Halafu kuna Mo Salah. Miguu yake haina maajabu tena. Amechoka zake. Salah alikuwa na uhakika na mabao yake 30 kwa msimu, lakini sasa hivi miguu yake ni kama vile imefungwa na mawe. Yeye ndiye aliyekuwa anaibeba Liverpool mgongoni mwake kiasi kwamba alikuwa anafikiriwa katika tuzo ya mwanasoka bora wa dunia.

PAZ 02

Kuna watu wanadai kwamba msimu uliopita Slot alikuwa anatembelea nyota ya Jurgen Klopp. Kwamba mabaki yake yaliwasaidia Liverpool kupata ubingwa. Binafsi naamini makosa ya Arsenal na makosa ya waamuzi dhidi ya Arsenal pamoja na majeraha ya wachezaji muhimu wa Arsenal yaliwasaidia Liverpool kupata ubingwa.

Liverpool ya kawaida sana ilitwaa ubingwa msimu uliopita. Haikuwa Liverpool bora kuliko zile ambazo zilikosa ubingwa kwa tofauti ya pointi moja kwa Pep Guardiola. Sitaki kuizungumzia Liverpool iliyotwaa ubingwa chini ya Klopp, nazungumzia Liverpool ambayo ilikuwa inateseka kwa pointi chache dhidi ya Guardiola. Ile ilikuwa bora kuliko hii hapa iliyotwaa ubingwa msimu uliopita.

Na sasa Slot alikuwa analazimika kutengeneza Liverpool yake nyingine baada ya miguu ya kina Salah na Van Dijik kuchoka. Hata hivyo, inaonekana imekuwa kazi ngumu kwake. Hadi leo sijui kwanini alimuacha Luis Diaz ambaye anang’ara kule Bayern Munich. Kwa namna Liverpool hii inavyocheza Slot hajahalalisha uamuzi wa kumuacha Diaz.

PAZ 03

Lakini hajahalalisha kiasi cha Pauni 400 milioni ambazo klabu iliwekeza kuwanunua kina Alexander Isaak na wenzake katika dirisha kubwa la uhamisho la majira ya joto. Wakati mwingine pesa hizi ndizo huwa zinawaondoa makocha.

Unapewa bajeti kubwa ya usajili halafu unafungwa mechi tisa kati ya 12 mfululizo kabla dunia haijaugusa Desemba. Anaishia kukuna kipara chake tu pindi mechi zinapomalizika Anfield na kwingineko.

Kitu kingine kinachomfanya awe mfu anayetembea ni namna ambavyo kuna wakongwe wanaoheshimika pale Anfield hawajasimama nyuma yake. Nimemsikia Jamie Carragher akiwashambulia wachezaji wakongwe kama Van Dijik na Salah lakini ameelekeza mashambulizi yake kwa Arne Slot. Carragher anaheshimika vilivyo Anfield.

Nimemsikia Steven Gerrard akiwa amekata tamaa na kocha baada ya kichapo kutoka PSV katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. Anapokata tamaa mtu kama Gerrard basi ujue una maisha magumu. Kama Gerrard na Carragher wanaungana na mashabiki kukata tamaa, basi ujue maisha yako ni magumu. Tajiri wa klabu anaanza kupatwa na joto na mwisho anahofia asije kuonekana kuwa kiburi.

PAZ 04

Hii tabia ipo pia Old Trafford. Ukiona kina Rio, Roy Keane, Paul Scholes na Gary Neville wanaanza kukukatia tamaa katika makochi ya studio basi ujue maisha yako ni mafupi. Ukiona tu wanaanza kuungana na hisia za mashabiki basi ujue tayari umeingia katika kundi la wafu wanaotembea. Ndicho wanachofanya kina Gerrard na Carragher sasa hivi pale Anfield.

Nimemsikia Arne Slot mwenyewe akidai kwamba ameongea na mkurugenzi wa ufundi na amemhakikishia kuwa nafasi yake ipo salama.

Sio kweli. Mara nyingi ndivyo huwa inasemwa wakati kocha anapokuwa anazama katika maji ya shingo. Halafu ghafla utakisia ‘breaking news’ pale BBC, Skysport na kwingineko kwamba kocha amefukuzwa. Na naamini tunaweza kuamka na hiyo habari Jumatatu asubuhi kama Liverpool wakipasuliwa na West Ham Jumapili pale London.

Matajiri huwa wanaangalia biashara zao. Licha ya kutumbukiza Pauni 400 milioni katika dirisha kubwa lililopita, tajiri pia anaangalia uwezekano wa kukosa nafasi nne za juu. Ukikosa Top four kuna hasara ya pesa ambayo tajiri hakuitegemea. Vitabu vyake vinashindwa kukaa sawa. Hapa ndipo matajiri huwa wanachukua uamuzi mgumu hata kama una urafiki naye binafsi.

PAZ 05

Tatizo kubwa ni kwamba endapo matajiri wa Anfield watachukua uamuzi huo, basi bundi atakuwa anaunguruma pale Anfield kwa muda mrefu.

Liverpool walifurahi wakati Slot moja kwa moja alipotwaa Ligi Kuu. Lakini kama wanaamini sasa kwamba alitembelea nyota ya Klopp basi kuna uwezekano mkubwa wa kuwa mwanzo wa kuhangaika na makocha.

Anapoondoka kocha mkubwa maisha yanakuwa magumu kwa klabu husika. Tangu Sir Alex alipoondoka maisha yamekuwa magumu pale Trafford. Wamebadilisha makocha lukuki. Wenye uzoefu na wasio na uzoefu. Na hata wa sasa hivi hawana uhakika naye. Juzi tu ametoka kufungwa na timu iliyocheza pungufu kwa dakika 77.

Na kila ninapotazama nje ya mlango sioni kama kuna makocha wengi hodari ambao wanakuhakikishia mafanikio. Labda waende pale Como kumchukua Cesc Fabregas ambaye katika dirisha kubwa lililopita alikataa kwenda Inter Milan.

Hakuna makocha wengi wanaokuhakikishia mambo makubwa kama unavyodhani kabla haujamfukuza kocha.

Lakini kabla hatujafika huko tusubiri kwanza kuona hatima ya Slot. Kwangu ni mfu anayetembea. Sioni kama anabadilisha mbinu zake kila anapotoka kufungwa.

Timu inacheza vile vile na bahati mbaya kwake kuna mambo mawili hayafanyi jwa ufasaha kama ambavyo Klopp alikuwa anafanya. Kwanza kabisa Klopp alikuwa anakaa na mpira kwa muda mrefu kiasi kwamba hakupi nafasi ya wewe kukaa na mpira na kutengeneza mashambulizi.

Lakini pili Klopp alikuwa anahemea langoni kwako kwa muda mrefu akitengeneza mashambulizi na kufunga. Arne Slot hana mambo haya mawili na hata msimu uliopita licha ya kutwaa ubingwa lakini hakuwa bora katika mambo haya. Tusubiri na kuona ataamkaje pale London kesho jioni akicheza na wapiga nyundo.