Prime
Pedro, Barker mtego mmoja, wakitoboa hapo freshi
VIKOSI vya Simba na Yanga vipo kambini kwa sasa vikijiandaa na mechi za viporo za Ligi Kuu Bara, lakini makocha wa timu hizo kila mmoja akiwa na wiki moja ngumu ya kuthibitisha ufundi na mbinu za kukabiliana na adui wa aina yoyote.
Simba itaanza kutupa karata kesho Jumapili dhidi ya Mtibwa Sugar katika mechi ya kiporo cha Ligi Kuu kabla ya watani wao kushuka uwanjani siku inayofuata yaani Jumatatu dhidi ya Mashujaa mechi zote zikichezwa jijini Dar es Salaam.
Simba inarudi katika mechi za Ligi Kuu ikiwa na kumbukumbu ya kupasuka kwa mabao 2-0 mbele ya Azam FC katika mechi ya mwisho, wakati Yanga yenyewe ikishinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa ambao ndio wanaokabiliana na Mnyama kesho kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Lakini baada ya mechi hizo kwa vigogo hao, wataanza maandalizi ya safari ya kwenda Afrika ya Kaskazini kwa ajili ya mechi za makundi za Ligi ya Mabingwa Afrika huku kila moja ikiwa na hali tofauti, lakini kibarua kikiwa kwa makocha wa timu hizo ambao ndio wanaanza kuzoeleka.
Yanga itashuka uwanjani Ijumaa ijayo jijini Cairo dhidi ya Al Ahly ya Misri kabla ya Simba nao kushuka siku inayofuata kuikabili Esperance ya Tunisia jijini Tunis, ikiwa chini ya kocha mkuu mpya, Steve Barker aliyetua hivi karibuni kutoka Afrika Kusini.
Mechi ya kiporo cha Ligi Kuu na pambano dhidi ya Esperance ni mtihani mgumu kwa kocha Barker anayeiongoza timu hiyo kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo, ikiwa ni siku chache tangu alipotoka kutolewa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 iliyomalizika visiwani Zanzibar.
Barker aliyetambulishwa Desemba 19 mwaka jana akitokea Stellenbosch ya Afrika Kusini sio mgeni wa michuano ya CAF, lakini safari hii anaiongoza Simba iliyoanza vibaya michuano hiyo ikiwa mkiani mwa Kundi D, akiwa amebeba matumaini ya Msimbazi kuwavusha kwenda robo fainali.
Kocha huyo aliyeishia nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita akiwa na Stellenbosch kwa kutolewa na Simba, ana kibarua cha kuanza vyema katika mechi ya Ligi dhidi ya Mtibwa Sugar kabla ya kukabiliana na Esperance ili kufufua matumaini ya Wekundu hao.
Kutoka mechi ya ligi dhidi ya Mtibwa yaani kesho hadi pambano la ugenini dhidi ya Esperance itakuwa ni kama wiki moja tu, hii ikiwa na maana kocha Barker ana kibarua cha kutumia muda huo kuhakikisha anawapa raha mashabiki wa Simba kabla ya kurudiana na Watunisia hao.
Barker aliyeondoka Stellenbosch akiiacha kileleni mwa Kundi C la michuano ya Kombe la Shirikisho akishinda mechi moja dhidi ya As Otoho ya Congo Brazzaville na kutoka sare ya bao 1-1 ugenini mbele ya Singida Black Stars, akichemsha hapo mwanzoni atajiharibika kazi.
Hii ni kwa sababu matokeo ya kufungwa bao 1-0 na Azam FC na kutolewa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi baada ya awali kuishinda kwa mbinde Muembe Makumbi kwa bao 1-0 kisha kulazimika kupindua meza mbele ya Fufuni iliyotangulia kwa bao la mapema na kutoka na ushindi wa mabao 2-1 haijawavutia mashabiki wa Msimbazi na wanataka kuona vitu vyake katika mechi zijazo.
REKODI ZA ESPERANCE
Simba iliyoanza michuano ya CAF kwa kufungwa nyumbani kwa bao 1-0 na Pedro Atletico ya Angola kisha kulala ugenini kwa mabao 2-1 mbnele ya Stade Malien ya Mali kumeiacha ikiwa mkiani mwa kundi bila pointi yoyote.
Sasa inakutana na mabingwa hao wa zamani wa Afrika yenye pointi mbili baada ya mechi zote za awali kutoka sare na wapinzani walioitungua Simba, ina maana haitakuwa kazi nyepesi kwa Barker na jeshi lake kwa jumla.
Matokeo yoyote ya kupoteza kwa Simba itakuwa na maana itajiweka pabaya katika safari ya kuisaka robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya tano ndani ya misimu sita ya michuano hiyo tangu 2018-2019.
Simba imetinga robo fainali nne katika misimu sita iliyopita ya Ligi ya Mabingwa ikiwamo ya 2018-2019, 2020-2021, 2022-2023 na 2023-2024, huku ikifuzu pili hatua hiyo mara mbili katika Kombe la Shirikisho Afrika ikiwamo 2021-2022 ilipoangukia kutoka Ligi ya Mabingwa na msimu uliopita ilipopenya hadi fainali na kupoteza mbele ya RS Berkane ya Morocco kwa mabao 3-1.
Licha ya kuwa itakuwa ni mara ya kwanza timu hizo kukutana katika michuano ya CAF, lakini rekodi za Esperance zinatisha ikiwa imebeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mara nne na kupoteza fainali tano ikimaliza kama mshindi wa pili kikiwa msimu wa 2023-2024 ilipolala mbele ya Al Ahly.
Pia imewahi kubeba ubingwa wa Kombe la CAF 1997, Kombe la Washindi Afrika 1998, michuano iliyokuja kunganishwa mwaka 2004 na kuwa Kombe la Shirikisho Afrika la sasa, mbali na taji la CAF Super Cup 1995 na kupoteza fainali nne za 1999, 2012, 2019 na 20220, mbali na ile ya Kombe la Washindi mwaka 1987 mbele ya Gor Mahia ya Kenya.
Kifupi ni Barker na kikosi hicho cha Msimbazi kina kibarua kigumu mbele ya Esperance ambao watarudiana nao wiki moja baadae jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Simba klabu yenye rekodi tamu katika michuano ya CAF hususani ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuliko timu yoyote ya Tanzania inajivunia nyota iliyonayo na wapya wanaodaiwa wameongezwa japo hawajatambulishwa kwa sasa.
Lakini kuwakosa makipa wote namba moja, kwa maana Moussa Camara na Yakoub Suleiman walio majeruhi ina maana Barker ana wiki moja ngumu ya kufanya miujiza kuibeba timu hiyo ikisaka tiketi ya robo fainali kwa mara nyingine, vinginevyo litampalia Msimbazi.
PEDRO SASA
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Barker na Wekundu wa Msimbazi, kwa upande wa Pedro hana kazi nyepesi kwani baada ya mechi dhidi ya Mashujaa, itakuwa na siku kama nne tu kabla ya kuikabili Al Ahly ugenini, pambano ambalo ni gumu kulitabiri kwa sasa.
Hata hivyo, tofauti na Barker, kocha huyu wa Yanga raia wa Ureno ameshakaa na timu kwa muda mrefu, kwani ameiongoza katika mechi mbili za awali za Kundi B dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco ikishinda 1-0 visiwani Zanzibar kisha kuibana JS Kabylie ya Algeria ugenini.
Kwa upande wa Ligi Kuu, Pedro ameiongoza timu hiyo katika mechi nne na zote ikishinda dhidi ya Mtibwa Sugar (2-0), KMC (4-1), Fountain Gate (2-0) na kuilaza Coastal Union kwa bao 1-0, huku katika Kombe la Mapinduzi ameiongoza pia mechi nne na kushinda zote.
Ilianza kwa kuifunga KVZ kwa mabao 3-0, kisha TRA United kwa bao 1-0 na kuifumua pia Singida Black Stars katika nusu fainali kwa bao 1-0 na kuishinda kwa penalti 5-5 Azam FC.
Hii ikiwa na maana Pedro anaingia katika vita mpya ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa akiwa hajaonja machungu ya kupoteza mechi yoyote tangu atue Yanga Oktoba kuchukua nafasi ya Romain Folz aliyetimuliwa baada ya kuingoza timu hiyo katika mechi nane ikishinda sita, sare moja na kipigo kimoja tu na kuruhusu wavu wa kikosi hicho kuguswa mara moja tu.
Licha ya rekodi hizo tamu tangu ajiunge na Yanga, kocha Pedro anakabiliwa na kibarua kigumu dhidi ya Al Ahly kwani wababe hao wa Afrika wamekuwa wakiiburuza Yanga katika mechi za CAF.
Katika mechi nane zilizopita baina yao katika CAF tangu mwaka 2009, Yanga imeshinda marta moja tu ilipoichapa Al Ahly jijini Dar es Salaam Machi Mosi, 2014, lakini yenyewe imepasuka mara tano na mechi mbili tu zilizoisha kwa sare.
Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana ilikuwa Machi Mosi, 2024 zikiwa makundi ya Ligi ya Mabingwa 2023-2024 na Al Ahly ilishinda nyumbani kwa bao 1-0 baada ya mechi ya awali jijini Dar es Salaam iliyopigwa Desemba 2, 2023 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Bao hilo la Yanga lililokuwa la kusawazisha liliwekwa kimiani na Pacome Zouzoua ambaye yupo katika kikosi cha sasa cha Pedro baada ya Percy Tau kuitanguliza Al Ahly dakika za lala salama na zote zikifuzu robo fainali Yanga ilitolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Hii ina maana Pedro anapaswa kuliandaa jeshi lake kikamilifu kabla ya kuifuata Al Ahly jijini Cairo kusaka ushindi wa kwanza msimu huu ugenini katika michuano ya CAF, lakini kujiweka pazuri kabla ya kurudiana na mabingwa hao wa kihistoria wa Afrika wiki moja baadae.
Ingizo la majembe matano mapya akiwamo Allan Okello, Depu, Mohammed Damaro, Emmanuel Mwanengo na kurejea kwa Yao Kouassi, sambamba na uwepo kwa nyota walioibeba timu hiyo ndani na kimataifa wanampa jeuri Pedro licha ya kuwa na muda mfupi wa mechi zilizopo mbele yake.
REKODI ZA AL AHLY
Ukiachana kuwa na rekodi tamu ya Yanga kabla ya kukabiliana nao kwa mara ya tisa tangu 2009, Al Ahly pia inabebwa na ubabe iliyonayo katika michuano ya CAF ikiwa ndiyo klabu iliyobeba mataji ya Afrika mara nyingi zaidi kuliko klabu yoyote, huku Yanga ikiwa haina chake.
Al Ahly imebeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mara 12, ikiwa pia na taji moja la Kombe la Shirikisho, manne ya Kombe la Washindi na CAF Super Cup mara nane, lakini ikiwa na rekodi tamu ikicheza nyumbani dhidi ya Yanga, kwani mechi nne zilizopita Cairo imeshinda zote.
AZAM FC NA SINGIDA BS
Ukiacha mbali wawakilishi hao wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, pia timu za Azam FC na Singida Black Stars zinazoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika zikicheza makundi kwa mara ya kwanza nazo zina kazi nzito katika wiki moja ijayo.
Singida iliyopo Kundi C ikiwa na pointi moja baada ya kupoteza mechi moja ugenini na kupata sare nyumbani yenyewe jana usiku ilikuwa uwanjani kuvaana na Dodoma Jiji katika mechi ya kiporo cha Ligi Kuu kabla ya kurudi tena uwanjani Jumanne ijayo dhidi ya JKT Tanzania kisha kuvuka Bahari ya Hindi kwenda Zanzibar kuisubiri As Otoho d'Oyo ya Congo Brazzaville.
Mechi hiyo ya CAF itapigwa Januari 25, siku ambayo wawakilishi wengine wa michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho itakapokuwa ugenini jijini Nairobi katika mechi ya Kundi B kuikabili Nairobi United, huku ikiwa imetoka kupoteza mechi mbili za awali za kundi hilo.
Singida ilipoteza kwa CR Belouizdad ya Algeria kwa mabao 2-0 kisha kutoka sare ya 1-1 na Stellenbosch ya Afrika Kusini na inapaswa kushinda mechi mbili zijazo dhidi ya Otoho ili kujiweka pazuri, lakini ni baada ya mechi ijayo na vinara wa Ligi Kuu, JKT Tanzania.
Kwa upande wa Azam nayo ina mechi mbili za viporo vya Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union inayopigwa leo Jumamosi kisha kurudi uwanjani Jumanne ijayo dhidi ya Fountain Gate ndipo iifuate Nairobi United Januari 25 na kurudiana nao wiki moja baadae visiwani Zanzibar.
Kocha wa timu hiyo, Florent Ibenge mwenye rekodi tangu ya michuano ya CAF akiwa ameiingiza timu hiyo katika makundi kwa mara ya kwanza, ana kazi kubwa katika kundi lenye timu za AS Maniema ya DR Congo na Wydad Casablanca ya Morocco ili kuipeleka Azam Fc robo fainali.
Akiwa na kikosi chenye damu mchanganyiko Ibenge kama ilivyo kwa David Ouma wa Singida BS anahitaji ushindi katika mechi hizo mbili zijazo za CAF kama anataka kuendelea rekodi yake ya kucheza mara kadhaa hatua ya robo fainali na hata kubeba ubingwa wa michuano ya CAF.
Kama ilivyo kwa Simba na Yanga, wawakilishi wa michuano ya Shirikisho zina muda mfupi pia wa kujiandaa kabla ya mechi hizo za CAF kutokana na kuwa na viporo vya mechi mbili za CAF kila mmoja ikiwa na siku tano tu baada ya mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara.
MSIMAMO MABINGWA
KUNDI B
P W D L F A PTS
1. Al Ahly 2 1 1 0 5 2 4
2. Yanga 2 1 1 0 1 0 4
3. AS FAR Rabat 2 0 1 1 1 2 1
4. JS Kabylie 2 0 1 1 1 4 1
KUNDI D
P W D L F A PTS
1. Petro Luanda 2 1 1 0 2 1 4
2. Stade Malien 2 1 1 0 2 2 4
3. Esperance 2 0 2 0 1 1 2
4. Simba 2 0 0 2 1 3 0
MSIMAMO SHIRIKISHO
KUNDI B
P W D L F A PTS
1. Wydad AC 2 2 0 0 4 0 6
2. AS Maniema 2 2 0 0 3 0 6
3. Azam FC 2 0 0 2 0 3 0 0
4. Nairobi Utd 2 0 0 2 0 4 0
KUNDI C
P W D L F A PTS
1. Stellenbosh 2 1 1 0 2 1 4
2. Otoho D'Oyo 2 1 1 0 4 2 4
3. Belouizdad 2 1 0 1 3 4 3
4. Singida BS 2 0 1 1 1 3 1
RATIBA ZILIVYO YANGA
Jan 19, 2026
v Mashujaa (Ligi Kuu)
Jan 23, 2026
v Al Ahly (CAF)
Jan 30, 2026
v Al Ahly (CAF)
SIMBA
Jan 18, 2026
v Mtibwa Sugar (Ligi Kuu)
Jan 24, 2026
v Esperance (CAF)
Jan 30, 2026
v Esperance (CAF)
AZAM FC
Leo Jumamosi
v Coastal Union (Ligi Kuu)
Jumanne, Jan 20, 2026
v Fountain Gate (Ligi Kuu)
Jan 25, 2026
v Nairobi United (CAF)
Feb 01, 2026
v Nairobi United (CAF)
SINGIDA BS
Jumanne, Jan 20, 2026
v JKT Tanzania (Ligi Kuu)
Jan 25, 2026
v AS Otoho (CAF)
Feb 01, 2026
v AS Otoho (CAF)
06 Misimu ambayo Simba imefika robo fainali ya michuano ya CAF tangu 2018-2019
04 Huu ni msimu wa nne mfululizo kwa Yanga kucheza hatua ya makundi ya michuano ya CAF
01 Ndio msimu ambao Azam FC na Singida BS zimefika hatua ya makudni ya michuano ya CAF
1974 Mwaka ambao Simba ilifika nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa)
2023 Mwaka ambao Yanga iliandika historia ya kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika
00 Hakuna klabu yoyote ya Tanzania iliyowahi kubeba taji la CAF tangu zianze kushiriki 1968.