Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Opah: Bocco, Kagere wamenibeba

KAMA hujui siri ya mshambuliaji wa Simba Queens, Opah Clement kufanya vizuri Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), Mwanaspoti linakufichulia.

Mastaa wa Simba, Meddie Kagere mwenye mabao 11 na nahodha John Bocco aliyepachika mabao 10 walikuwa na kazi nzito kuhakikisha kikosi cha Simba Queens kinafanya vizuri kwenye ligi iliyomalizika hivi karibuni na wao kutwaa ubingwa huo.

Opah anafichua siri ya Bocco na Kagere kwamba, kabla na baada ya mazoezi wakikutana Uwanja wa Mo Simba Arena, nyota hao wanawatembelea mazoezini na kuwaibia siri ya ufungaji.

Opah ambaye yupo vizuri msimu huu, wapinzani wake wanajua hawawezi kukoswa ndani ya dakika 90, anasema Bocco na Kagere wanawapa mwanga mkubwa.

Katika mahojiano maalumu yaliyofanyika kwenye kambi ya timu hiyo iliyopo Bunju, Opa anafunguka vitu vingi ndani na nje ya kazi yake.

Mrembo huyu mzaliwa wa Mbeya alianza kucheza na wanaume akiwa kwao, baadaye Oscar Milambo (kwa sasa mkurugenzi wa Ufundi TFF) alimchukua kwenda Sekondari ya Makongo ambapo alimaliza kidato cha nne. Baada ya hapo alijiunga na Ever Green mwaka mmoja, aliondoka kwenda Kigoma Sisterz na baadaye kutua Simba msimu uliopita.

“Kabla sijajiunga Simba Queens nilikuwa napenda sana kuwatazama Kagere na Bocco, bahati nzuri naitumikia timu hii ambapo tunafanya mazoezi sehemu moja, hivyo nimepata nafasi ya kuwafahamu kwa ukaribu zaidi,” anasema Opah.

“Kagere na Bocco wanakuja kwenye mazoezi yetu na kutuelekeza baadhi ya mambo na namna tunavyotakiwa kuchukuliwa kazi hii, wamekuwa wanatuongoza vyema, hivyo wana mchango katika hatua zetu.”


CHANGAMOTO

Anasema kuna changamoto nyingi, lakini wakati anacheza timu za wanaume alijifunza mengi ambayo yamempa uimara wa kuamini kipaji chake.

“Najua nini ninakihitaji katika kazi yangu ndio maana hata changamoto sizifikilii kabisa, napambana kuhakikisha kila nililolipanga linaenda sawa na kwa muda muafaka, hata wakati nacheza timu ya wanaume mtaani kwetu nilishukuru walinichukulia kama mwenzao, ndio maana hakuna kinachonistaajabisha,” anasema.


VITA YA NAMBA

Anakiri kuwa vita ya namba ni kubwa, lakini anaichukulia upande wa kumfundisha nidhamu, umakini na upambanaji, akitambua kwamba akibweteka tu basi benchi litamhusu.

“Raha ya kikosi kuwepo na ushindani wa namba unaokufanya muda wote uheshimu nafasi unayopewa na kocha, jambo zuri tunafundishwa na Mgosi (Mussa Hassan) ambaye amecheza kwa mafanikio makubwa, hivyo anachotuelekeza tunatambua ni kwa ajili ya manufaa yetu.”


LIGI MSIMU HUU

Opah anasema ligi ilikuwa ngumu, kila timu ilipambana kuacha alama ya heshima, lakini aliamini upande wao wangetetea taji hilo.

“Msimu uliopita kulikuwa hakuna ushindani sana, unakuta timu inafungwa mabao 20, lakini msimu uliomalizika majuzi hakuna kitu kama hicho tunafunga, lakini sio kwa idadi kubwa ya mabao kama hayo, jambo hilo linatafsiri ushindani,” anasema.


KWA NINI SOKA

Opah anasema katika michezo yote aliona soka ndio chagua lake na hata alipojaribu kucheza michezo ya kike alishindwa na kujikuta mpira umekubali vizuri miguuni kwake.

“Mpira ndio kipaji changu toka utotoni, nimejikuta nacheza mpira nimefuata nyayo za baba alikuwa anacheza mpira huko nyuma, na hata nilipotaka kucheza mpira nilikuwa naenda uwanjani na baba na hata kaka zangu.”

Anaongeza kuwa: “Kufuatana nao kulinifanya nijikute napenda kuwa kama wao na hawakuniacha hata kidogo kila waendapo kwenye mechi tunaongozana hadi leo hii wanaendelea kunishika mkono.”


MBALI NA SOKA

Anasema kama asingecheza soka huenda angekuwa muimbaji wa muziki wa kizazi kipya kama Zuchu wa lebo ya Wasafi.

“Napenda sana muziki, nikiwa sina majukumu yangu ya uwanjani napenda kusikiliza sana muziki, na naimba pia,” anasema Opah ambaye anadai kuzipenda nyimbo za Daimond Platinumz


UFUNGAJI WAKE

Anasema msimu huu aliamua kuhakikisha anapita mabao aliyoyafunga msimu uliopita aliomaliza akiwa na mabao 20, lakini malengo yake ilikuwa ni kupita rekodi hiyo ambapo mpaka sasa amemaliza na mabao 30.

“Kama mshambuliaji nilipanga kabisa kuhakikisha navuka yale niliyokuwa nayo msimu uliopita na nashukuru sana Mungu mpaka sasa nimeyavuka nasubiri mchezo wetu wa mwisho.”


UBINGWA MSIMU HUU

“Kama wachezaji dhamira yetu ni kuhakikisha tunalitwaa taji la ligi, japokuwa ushindani ulikuwa mkubwa kwa sisi hasa na Yanga tulihakikisha tunatimiza malengo yetu, ni pointi tatu tulihitaji tu,”anasema


NAFASI TIMU YA TAIFA

Mechi yake ya kwanza kuitwa ilikuwa dhidi ya Nigeria nje ya nchi na ilikuwa faraja kwake siku hiyo alipopata nafasi hiyo

“Kila mchezaji anatamani kuitwa timu ya Taifa, hakuna ambaye hatamani ni ishu ya muda tu, hata kama hujabahatika kuitwa usikate tamaa ipo siku tu unaitwa,” anasisitiza Opah.


WITO KWA WAZAZI

Anasema licha ya wazazi wengi kutowaruhusu watoto wa kike kucheza amewataka kuwapa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao kwa kuwa soka la sasa ni ajira tofauti na huko nyuma.

“Mpira ni ajira siku hizi, kila mchezaji anapambana kuhakikisha maisha yanaenda hii kasumba ya kusema mpira ni uhuni imepitwa na wakati hakuna kitu kama hicho, unaweza usicheze mpira na ukawa muhuni vile vile.”


MALENGO YAKE

Anasema anafarijika kuona wachezaji wenzake wakipata nafasi ya kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kama ilivyokuwa Mwanahamis Omary ‘Gaucho’ anayecheza nchini Morocco.

“Najua ipo siku tu nitatoboa kama waliotutangulia, ni wakati tu ukifika hakuna kinachoshindikana,” anasema Opah.