NYUMA YA PAZIA: Waarabu walivyoliweka soka kiganjani, pesa inaongea

UTAAMUA mwenyewe kama ni raha au karaha. Pesa inaamua. Utaamua mwenyewe uwe na chuki au utiwe morali. Utaamua mwenyewe. Namna ambavyo Waarabu wameuweka mchezo wa soka katika kiganja. Na naamini itaendelea hivyo kwa muda mrefu ujao.

Nilikuwa natazama pambano la PSG dhidi ya Riyadh All Stars lililochezwa pale Saudi Arabia. Nimekumbuka mambo mengi na namna ambavyo Waarabu wameuweka mchezo wa soka katika kiganja. Waliamua kumchukua Cristiano Ronaldo halafu hapo hapo wakahakikisha anacheza dhidi ya hasimu wake, Lionel Messi. Katika bei hiyo hiyo wakamkutanisha Ronaldo pamoja na mastaa wengine, Kylian Mbappe na Neymar.

Na kuna uvumi kwamba Waarabu wenyewe wanataka Messi akacheze kwao. Wanataka kuwe na Ligi Kuu ya soka nchini kwao ambapo Messi na Ronaldo wapo. Kifupi pia wanataka kuwe na mechi mbili katika Ligi ambapo Ronaldo na Messi watakutana uwanjani. Waarabu wanaupeleka mpira sebuleni kwao.

Ukisoma namba za muamala ambao Messi anaweza kulipa kwa msimu mmoja pale Saudi Arabia unahisi kuchanganyikiwa. Tayari tumeshachanganyikiwa na muamala ambao unasoma katika akaunti ya Ronaldo. Unaposoma muamala unaomuhusu Messi unajihsi kuchangikiwa.

Subiri kwanza. Hii inakuja siku chache baada ya Waarabu kufanikisha michuano ya kombe la dunia pale Qatar. Inatajwa kuwa michuano iliyofana zaidi katika historia ya kombe la dunia. Wazungu walijaribu kubana lakini pesa iliamua kuongea na wote tukakaa kimya. Hata hivyo kwa walichofanya hawana baya.

Nasikia Waarabu wameanza kampeni nyingine ya kuhakikisha Saudi Arabia inaandaa kombe la dunia mwaka 2030. Nani atawazuia? Sijui. Inaonekana watu wa FIFA wapo katika himaya yao. Awali nilidhani kwamba Waarabu walikuwa wamemuweka mkononi Sepp Blatter na genge lake. Hata hivyo nilikosea.

Namna Rais wa sasa wa FIFA bwana, Gianni Infantino alivyoitetea michuano ya kombe la dunia pale Qatar nikajua kwamba tayari yeye na watu wake wapya hawapindui kutoka katika kucha za Waarabu. Waarabu wakitaka kulipeleka kombe la dunia pale Saudia sioni mtu wa kuzuia. Tutaishia kupiga kelele na kisha kuwaruhusu.

Subiri kwanza. Tuache unafiki. Tunaweza kuona Waarabu wanatutawala vibaya katika maeneo hayo lakini kumbe wote tunawatamani katika upande mwingine. Ni nani ambaye hataki klabu yake ya Ulaya inunuliwe na Waarabu? Kila mmoja anatamani. Nani anawataka matajiri wa mawazo kutoka Marekani au Uingereza? Wote tunawataka Waarabu.

Taratibu Newcastle United wanaanza kusumbua Ligi Kuu ya England. Nawapa miaka minne tu kabla hawajatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England. Msimu huu wanaelekea Top Four taratibu huku wakiwa mbele ya muda. Waarabu bado hawajaanza kutia pesa nyingi. Wameanza mchakato huo na tayari timu inaelekea Top Four.

Wachezaji kama Alexander Isak au Bruno Guimares miezi 24 iliyopita hawakuwa na hadhi ya kuichezea Newcastle United. Walikuwa wachezaji wakubwa waliotaja kwenda Real Madrid, Barcelona, Manchester United, Arsenal, Chelsea na kwingineko lakini wameishia katika noti za Kiarabu pale Newcastle.

Huu ni mwanzo tu. Newcastle wakishaenda Ligi ya mabingwa ndio utasikia akina Kylian Mbappe wanatua England. Subiri kwanza. Mbappe? Inawezekana hata yeye mwenyewe ninakosea. Kwanza alipo yupo kwa Waarabu. Halafu ni pesa za Waarabu ndizo zilizomfanya alkane Real Madrid hadharani.

Mchezaji wa hadhi yake, aliyemaliza mkataba wake, angewezaje kuikana klabu kama Real Madrid? Na zaidi ya yote kuikana Madrid kwa sababu ya kubakia PSG. Labda kama angekuwa ameikana Madrid na kubakia Manchester United au Barcelona au Juventus. Hapana, ameamua kuikana Real Madrid huku akiwa amebakia PSG. Timu ambayo haijawahi hata kuchukua ubingwa wa Ulaya.

Jibu ni moja tu. Pesa. Lakini yeye hatakuwa wa kwanza. Ni pesa hizi hizi za Waarabu ndizo zilizosababisha wachezaji wakubwa wa zama hizi kama Kelvin de Bruyne, David Silva, Sergio Aguero, Vincent Kompany na wengineo kuamua kucheza timu kama City na kuachana na habari za Real Madrid na Barcelona.

Zamani wachezaji wa kariba hii vituo vikubwa vingekuwa Santiago Bernabeu, San Siro, Camp Nou, Old Trafford au Stamford Bridge. Kibao kimegeuka na maisha yamekuwa tofauti. Yote haya ni kwa sababu ya pesa za Waarabu. Wamebadili mkondo wa historia.

Lakini kama unadhani Waarabu wanajaribu kuliweka kombe la dunia mkononi basi nadhani katika vilabu itakuwa maradufu zaidi. Kuna rafiki zangu pale Qatar wanaitaka Liverpool kwa udi na uvumba. Kuna Wasaudia wanaitaka Manchester United kwa udi na uvumba.

Hii inaweza kuwa dawa pekee ya wachezaji wakubwa kuendelea kubaki katika klabu zetu zenye mafanikio makubwa ya kihistoria lakini vinginevyo wataishia kucheza City, Newcastle United au PSG ambazo hazina mafanikio makubwa katika historia. Ni ukweli mchungu lakini lazima tuumeze.

Pale kwangu Arsenal Mikel Arteta amekuwa akifanya kazi nzuri lakini nadhani kazi yake itakwenda sawa zaidi kama akisaidiwa na noti za Mwarabu. Hiki ndicho kwa kiasi kikubwa kimemsaidia Mwalimu wake, Pep Guardiola pale Etihad. Unaweza kuwa kocha mzuri kadri unavyoweza lakini unahitajj wachezaji bora.

Kama Arsenal wangekuwa na tajiri Mwarabu sidhani kama wangemkosa mchezaji anayeitwa Mykhailo Mudryk. Arteta alimuhitaji lakini Wazungu wana maadili yao katika matumizi. Wakamuacha aende Chelsea. Waarabu wa Manchester City wasingeruhusu hali hii. Nadhani ni vile tu Arsenal imekuwa ikifanya vizuri msimu huu ndio maana mashabiki hawajapeleka hasira zao kwa tajiri, Stan Kroenke baada ya kumkosa Mudryk.

Binafsi nina asilimia nyingi za kupenda kile ambacho Waarabu wanafanya. Nina asilimia chache za kuchukia kile ambacho wanafanya. Ukweli ni kwamba dunia ilikuwa lazima ichangamke. Ni lini upinzani kati ya Manchester United na Manchester City ungekuwa halisi kama Waarabu wasingeingilia kati?

Ni lini wachezaji wakubwa wangezikataa Real Madrid na Barcelona? Lini Manchester City wangekaribia kutwaa Ligi Kuu ya England kwa miaka mitatu mfululizo? Kuna maswali mengi yanayojibu swali 'lini ambayo yameondolewa na pesa za Mwarabu. Hili lilikuwa swali maarufu katika soka lakini majibu mengi yameanza kupatikana baada ya Mwarabu kutia noti zake za mafuta katika soka.

Wakati watu wengi tukiwa hatujui namna ya kuviandaa vichwa vyetu kujua namna ya kupokea pesa za Waarabu katika soka ukweli ambao inabidi tukubaliane nao ni kwamba shughuli ndio kwanza imeanza kutoka kwa Waarabu. Sioni kama ndoto za kile wanachofikiria zitakwama hivi karibuni. Tujiandae tu kuwapokea.