Prime
NYUMA YA PAZIA: Unamkumbuka Oscar? Amerudi nyumbani na akaunti ya Bakhresa

Muktasari:
- Unamkumbuka? Yule kijana mwenye sura ya kitoto aliyetua Chelsea mwaka 2012 akitokea kwao Brazili alikokuwa akicheza klabu ya Internacional. Wengi tulimzoea na kumpenda. Tuliamini angekuwa ni Ricardo Kaka mwingine. Alikuwa kiungo maridadi. Ghafla akaondoka zake kwenda China mwaka 2017.
UNAMKUMBUKA Oscar Dos Santos Emboaba? Tulimjua kwa jina moja tu la Oscar. Wakati mwingine Wabrazil wanatushangaza kwa kuwa na majina ambayo huwa hatukudhania kwamba wangeweza kuwa nayo. Mfano ni Oscar.
Unamkumbuka? Yule kijana mwenye sura ya kitoto aliyetua Chelsea mwaka 2012 akitokea kwao Brazili alikokuwa akicheza klabu ya Internacional. Wengi tulimzoea na kumpenda. Tuliamini angekuwa ni Ricardo Kaka mwingine. Alikuwa kiungo maridadi. Ghafla akaondoka zake kwenda China mwaka 2017.
Oscar alituachia majonzi makubwa ambayo siku hizi tunaachiwa na wachezaji vijana wanaokwenda Saudia. Wakati huo Wachina ghafla wakataka mpira uchezwe kwao. Wakaanza kuwapa mikataba minono na mirefu wachezaji mastaa wa Ulaya.
Mfano ni Oscar mwenyewe. Chelsea walilipwa kiasi cha Pauni 60 milioni na klabu ya Shanghai Port kwa ajili ya kuruhusu huduma za Oscar ziende China. Kaka mwenyewe alipewa mkataba ambao ungeruhusu alipwe kiasi cha pauni 400,000 kwa wiki.

Baadaye huu mradi wa kwenda China kwa pesa nyingi ulikufa, lakini Oscar alihakikisha kuwa mkataba wake unadumu mpaka siku ya mwisho. Wakati anatuaga alituachia huzuni kubwa. Oscar alikuwa na miaka 25 tu. Bado tulikuwa tunatazamia afanye mambo makubwa pale darajani.
Hata hivyo, aliwahi kutukumbusha namna ambavyo pesa zilikuwa muhimu kwake. Wakati ule tukimsimanga kwa kuamua kwenda China badala ya kuendelea kuwa moto Ulaya alisikika akisema; “Kila mchezaji, au mtu anayefanya kazi, anataka kupata pesa kwa ajili ya kusaidia familia. Nimetoka katika maisha ya shida sana Brazili. Hatukuwa na chochote. Haya ni matunda ya kazi yangu na ninapopata chochote basi ujue ninastahili.â€
Hivi ndivyo Oscar alivyotutoka Ulaya akaenda zake China, ingawa kulikuwa na klabu kibao za Ulaya zinamtaka. Alituachia majonzi makubwa ingawa wakati mwingine alitufikirisha. Kipi bora, pesa au mchezo wenyewe?

Ile kuondoka tu Chelsea Wabrazil wakamnunia Oscar. Hawakumuita tena katika timu ya taifa. Hadi wakati anaondoka alikuwa amecheza mechi 48 tu. Mpaka leo imesimama idadi hiyo hiyo. Waliamini kwamba alikuwa amekwenda katika Ligi ambayo haikuwa na ushindani mkubwa.
Kuanzia hapo inasemekana Oscar amefanikiwa kuingiza kiasi cha pauni 145 milioni katika kipindi cha miaka nane aliyokaa China. Hiyo ni mbali na mikataba yake mingine ya kibiashara. Inaweza kuwa ni kiasi kikubwa cha pesa kuliko ambacho Ronaldinho ametengeneza katika mpira. Maisha yanataka nini zaidi.
Oscar hakutaka kuwa mnafiki. Akaamua kuchukua chake mapema kadri alivyoweza. Sasa hivi ana umri wa miaka 33 tu na wiki iliyopita ametangaza kurudi katika timu ambayo alianzia maisha yake ya soka. Sao Paulo. Amekwenda nyumbani akiwa na kiinua mgongo cha kutosha katika maisha.

Tulimsimanga sana lakini sasa hivi umefika muda wa yeye kuanza kuzisimanga akaunti zetu. Na unapofikiria kwamba akiwa na Chelsea alitwaa taji la Ligi Kuu ya England, akatwaa kombe la Ligi na kisha akatwaa taji la Europa basi bado ana kitu cha kuzungumzia kuhusu mafanikio yake ya soka la Ulaya.
Kule China ameondoka na pesa nyingi lakini walau Oscar ana kitu cha kuwaambia wajukuu zake kuhusu China. Ameondoka akiwa mchezaji bora zaidi wa kigeni katika historia ya soka la China. Alifunga mabao 77, akatoa pasi za mabao 141 katika mechi 248 alizocheza China. Ameondoka na mataji matatu ya Ligi kuu ya China, kombe la FA yao na Super Cup.
Sisi tunaweza tusizitambue takwimu hizi lakini kwa Wachina zinamfanya kuwa mchezaji bora zaidi kuwahi kutokea katika historia ya China. Ni wazi kwamba Wachina wanaamini kuwa Oscar hajawadhulumu pesa zao kwa mafanikio haya.

Baada ya kila kitu, rafiki yetu Oscar ingawa tumemsahau na alikuwa ametutia huzuni wakati akienda zake China huenda yeye ndiye ambaye atakuwa anawanunulia bia Ronaldinho na Adriano ambao maisha yao hayaeleweki na wanaelekea kufilisika.
Mpaka sasa sijui cha kupongeza wala cha kuponda kuhusu mamuzi ambayo Oscar aliyafanya mwaka 2017 wakati alipoondoka darajani kwenda China lakini siamini kama Oscar mwenyewe ana mambo mengi ya kujutia baada ya kuondoka Ulaya.
Kwa mfano, licha ya kwamba Wabrazil walimsusa katika timu yao ya taifa lakini wana taji moja tu la maana ambalo walichukua tangu waache kumuita Oscar. Ni pale walipochukua taji la Copa America mwaka 2019.

Vinginevyo Wabrazil hawakuchukua kombe la dunia wala kufika fainali tangu walipoachana na Oscar. Mbele yake kulikuwa na michuano miwili ya kombe la dunia pale Russia mwaka 2018 na Qatar mwaka 2022. Brazil hawakufika hata nusu fainali. Oscar hawezi kutazama nyuma na kujuta.
Kama kuna michuano mikubwa ya kueleweka ambayo hakuchukua Ulaya basi ni Ligi ya mabingwa wa Ulaya. Lakini hata Ronaldo de Lima hakuwahi kuchukua ubingwa wa Ulaya. Na kama tunahesabu basi kuna mastaa wengi wakubwa hawakuchukua taji hili.
Na sasa Oscar anarudi kwao Sao Paulo kuanzisha miradi mingi ya maendeleo kupitia mtaji wake wa mabilioni ya pesa aliyovuna China. Alipokea masimango yetu kwa tabasamu lakini nahisi sasa hivi yeye ndiye anacheka zaidi kila anapokwenda kuchungulia akaunti yake ya benki.
Hapa ndipo ambapo tutapoteza wachezaji wengi ambao watakwenda kufukuzia pesa za Waarabu Saudia. Wapo wengine ambao wamekwenda mapema zaidi na hawajafanya mambo yoyote makubwa Ulaya. Kama wao hatuwezi kuwalaumu sana ni vipi tunaweza kumlaumu rafiki yetu Oscar?