Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NYUMA YA PAZIA : Tunampeleka shetani huyu kwa Jose Mourinho?

Muktasari:

  • Tatizo United ni wajanja. Wamesisitiza kwamba Rooney hauzwi. Sio kweli kwamba Rooney hauzwi. Anauzwa sana. na hata wenyewe mabosi wa United wanajua. Wanachofanya ni kumpandisha bei.

ALBERT Einstein, mwanafalsafa mahiri wa zamani wa Ujerumani aliwahi kusema ‘Shetani ametuacha tuamue vitu vingi tunavyofurahia katika maisha, ama tuumie katika afya zetu, au tuumie katika mioyo yetu au tunenepe.’

Na ndicho kinachotokea Old Trafford kwa sasa. Iwe kwa mashabiki, kwa David Moyes, Sir Alex Ferguson, au yeyote anayehusika na Manchester United, Wayne Rooney anabakia kuwa shetani huyu.

Ni wazi kwamba Wayne Rooney anauzwa Old Trafford. Siku hizi mbili zilizopita inaonekana wazi kwamba Rooney yuko katika siku za mwisho za maisha yake Old Trafford. Tatizo ni kwamba Jose Mourinho ndiye mtu anayemtaka kwa hamu kubwa.

Amemtolea macho. Anawavuruga kweli kweli Manchester United. Kila anapotamka kuwa anamtaka Rooney ndipo ambapo Old Trafford inavurugukiwa. Saa 48 zilizopita alikuwa ametoa ofa yake ya kumtaka Rooney.

Tatizo United ni wajanja. Wamesisitiza kwamba Rooney hauzwi. Sio kweli kwamba Rooney hauzwi. Anauzwa sana. na hata wenyewe mabosi wa United wanajua. Wanachofanya ni kumpandisha bei.

Moyes amezidi kuchochea uuzwaji wa Rooney kwa kutamka wazi kwamba mshambuliaji wake namba moja atakuwa Robin Van Persie. Kauli hii inazidi kumtia hasira Rooney kufuatia kauli ya Ferguson aliyoitoa katika mechi dhidi ya Swansea kwamba Rooney ameomba kuuzwa kitu ambacho Rooney mwenyewe anakanusha.

Wanachofanya United hapa ni kumpandisha bei Rooney kwa timu inayomtaka Rooney hili ijikamue zaidi mfukoni. Tatizo kubwa ambalo United wanakumbana nalo ni ukweli kwamba hawataki kumuuza Rooney ndani ya England na wakati huo huo hakuna timu ya nje ya England ambayo inamuhitaji Rooney.

Vyombo vya habari vya Uingereza viliendeleza tabia yao ya kuwafanya wachezaji wao wafalme kwa kumpeleka Rooney Barcelona, kisha Real Madrid halafu Bayern Munich. Lakini imegundulika kuwa wote huo ulikuwa uongo. Barcelona ilikuwa bize na Neymar, Bayern Munich walikuwa makini na Roberto Lewandowski, huku Bayern Munich wakichanga karata zao kwa namna nyingine na kutangaza rasmi kwamba walikuwa hawana mpango na Rooney.

Mchezaji pekee anayetakiwa nje ya ardhi ya England kwa sasa ni Gareth Bale. Huyu ndiye ambaye majuzi mashabiki wa Real Madrid walikuwa wanamuimba wakati Rais wa Real Madrid, Fiorentino Perez akimtambulisha kiungo wao mpya, Assier Illarramendi.

Mtu pekee ambaye anamuhitaji sana shetani wao ni Mourinho. Ukimpeleka Rooney kwa Mourinho ni tatizo. Kwanza kabisa atatengeneza mvuto mkubwa kwa Chelsea ndani na nje ya uwanja. Atawaimarisha kama timu ndani ya uwanja, lakini pia nje ya uwanja atakuwa mchezaji wa kibiashara.

Ndani ya uwanja, Rooney anafaa katika staili ya Mourinho. Ana nguvu, kasi, ari na ni mpiganaji. Anaweza kubaki peke yake mbele akasukumana na kila mlinzi huku nyuma yake wakicheza Juan Mata, Oscar na Eden Hazard (utatu mtakatifu).

Hiki ndicho ambacho United hawataki kusikia.  Atawaachia maamuzi magumu kama shetani. Ama ataumiza afya zao, ama ataumiza mioyo yao, au ataacha wanenepe endapo kwa bahati mbaya Rooney akivurunda Chelsea.

Ilipofikia hatua ya kumuuza David Beckham, Ferguson aliwaachia Barcelona na Madrid wauane na bahati nzuri Madrid wakashinda kesi hiyo na kumchukua Beckham. Lakini kwa sasa kuna tofauti kubwa kati ya Beckham na Rooney.

Beckham alikuwa mchezaji wa biashara. Aliangalia mengi wakati anakwenda Madrid. Sura yake ilikuwa katika ofisi nyingi za matangazo kama ilivyo kwa Cristiano Ronaldo leo. Lakini pia ilikuwa inamaanisha kwamba mke wake, Victoria alikuwa anakwenda katika mji mwingine ambao angeweza kufanya kazi zake za uanamitindo kwa utulivu.

Kwa Rooney hali ni tofauti. Hana mvuto sana katika matangazo ya biashara wala sura yake. Mke wake, Coleen naye hayupo katika maisha ya Victoria. Na ndio maana Rooney hana mawazo sana ya kucheza nje.

Tatizo pamoja na hamu ya Rooney kutaka kubaki England akichezea Chelsea au Arsenal ugumu unabakia pale pale kwa United kama watamruhusu shetani wao kuendelea kucheza England. Anaweza kuwaumiza mioyo yao kama ambavyo Van Persie anawaumiza Arsenal kwa sasa.

Uamuzi mgumu ungetolewa na Sir Alex kama angekuwa madarakani. Lakini kwa Moyes lolote linaweza kutokea. Beckham, Ruud Van Nisterlooy, Gabriel Heinze, Paul Ince, na wengineo wote Sir Alex aliwauza nje ya nchi. Ince alijirejesha Liverpool baadaye akitokea Inter Milan, lakini ni wazi kwamba Sir Alex asingeweza kumuuza Liverpool moja kwa moja akitokea Old Trafford.

Naendelea kuitazama filamu hii ya shetani Rooney kwa umakini mkubwa. Kama Rooney atabakia Old Trafford nadhani ni kwa sababu wana United watakuwa wanaona bora wabaki na shetani wao kuliko kumpeleka kwingine awaumize.

Lakini hapo hapo kama watalazimika kumtoa, nadhani wengi watahafikiana na mimi kuwa ni bora wampeleke Rooney Arsenal kuliko Chelsea kwa sababu Chelsea inaonekana timu tishio zaidi kwao na itaimarika maradufu kuliko kama akienda Gunners.

Nasubiri kwa hamu kuona Manchester wataamua nini kuhusu shetani huyu. Kama akibaki, sioni kama mahusiano yake na United yataimarika. Rooney ameyavunja mara nyingi mahusiano yake na United. Na hata kukaa kimya katika kipindi hiki ni kuendelea kuvunja mahusiano yake. Shetani huyu atapelekwa wapi na United? Nasubiri.