Prime
NYUMA YA PAZIA: Nistelrooy sikumtazamia katika kazi nyingine uwanjani
Muktasari:
- Kuzaliwa kwa ajili ya kufunga? Tumewahi kusikia kauli hizi huko nyuma. Lakini nilikuwa najiambia hivyo wakati namtazama Ruud van Nistelrooy miaka hiyo akiwa na jezi ya Manchester United. Sikuamini kama angeweza kufanya kazi nyingine yoyote katika soka zaidi ya kufunga mabao.
Erling Haaland alizaliwa kwa ajili ya kufunga mabao Pep Guardiola alisikika akiwaambia waandishi wa habari jioni ya Jumapili Agosti 7, 2022 wakati Haaland alipoisaidia Manchester City kuichapa West Ham United mabao 2-0 ugenini.
Kuzaliwa kwa ajili ya kufunga? Tumewahi kusikia kauli hizi huko nyuma. Lakini nilikuwa najiambia hivyo wakati namtazama Ruud van Nistelrooy miaka hiyo akiwa na jezi ya Manchester United. Sikuamini kama angeweza kufanya kazi nyingine yoyote katika soka zaidi ya kufunga mabao.
Ronaldo de Lima alikuwa mfungaji hasa, lakini angeweza kufanya mambo mengine uwanjani. Angeweza kupiga chenga kuanzia katikati ya uwanja na kwenda kufunga. Kumbe alikuwa anaiweza kazi ya chenga. Ruud hakuweza kazi nyingine zaidi ya kuvizia katika boksi la adui na kufunga.
Bao pekee alilowahi kufunga nje ya boksi ya adui lilikuwa dhidi ya Fulham enzi hizo. Vinginevyo mabao yake mengine yote aliyafunga ndani ya kumi na nane, na hasa ndani ya sita. Sijawahi kumuona mshambuliaji mviziaji zaidi yake.
Sikuwahi kudhani kama anaufahamu mpira zaidi ya kufungua nafasi na kufunga. Sikudhani kama alikuwa anaelewa lolote namna mpira unavyoweza kutoka nyuma mpaka katika miguu yake. Nilichofahamu ni kwamba alikuwa anajua kufungua nafasi na kufunga. Basi.
Lakini muda wowote kuanzia sasa atatangazwa kuwa kocha mpya wa Leicester City. Majuzi nilikuwa natabasamu wakati alipokuwa kocha wa muda baada ya kufukuzwa kwa Erik Ten Hag pale Manchester United. Sikuamini kwamba angeweza kuwa kocha wa soka.
Kwamba angeweza kuwaelekeza wachezaji wake namna ya kutawala mechi ya soka na kushinda. Kwamba angeweza kuwaelekeza wachezaji wake namna ya kulilinda lango lao. Kwamba angeweza kuwalekeza wachezaji wake namna ya kukaa na mpira kwa muda mrefu, wakati mwingine bila ya kutafuta mshambuliaji wao aliyesimama mbele kama ilivyokuwa kwa yeye enzi zake.
Kumbe anaiweza kazi hii na kitu kizuri zaidi ni kwamba katika mikono yake United ilionekana kama vile inaelekea kufufuka. Hata hivyo United hawakumuamini kumpa kazi hii moja kwa moja na badala yake wamemchagua Ruben Amorim kuwa kocha wao mkuu.
Nilimsikia staa mmoja wa zamani wa United, Paul Scholes akisema kwamba kwa kile ambacho Ruud alionyesha kwa siku chache pale Old Trafford basi hakustahili kuwa kocha wa msaidizi tena pale Trafford. Alistahili kupata timu yake mwenyewe kwingineko. Na kweli, Leicester wanakaribia kumchukua baada ya kumfukuza Steve Cooper.
Kwa Ruud nimeendelea kujifunza kwamba ukocha ni kazi tofauti na kucheza soka. Unaweza usiwe mchezaji mahiri lakini ukawa kocha mahiri kama Jose Mourinho. Unaweza ukawa mchezaji mahiri na dunia ikakuimba lakini ukaishia kuwa kocha mbovu. Mara chache pia tumeona wachezaji mahiri wakaibuka kuwa makocha mahiri kama ilivyowahi kutokea kwa Johan Cruffy.
Lakini ndani ya uwanja nilidhani aina yako ya mchezo inaweza kuamua uwe kocha au usiwe. Sikuamini kama mchezaji kama Ruud anaweza kuwa kocha achilia mbali kuwa kocha mzuri. Hata kwa rafiki yake, Pipo Inzaghi naye sikuamini kama angeweza kuwa kocha mzuri wa soka. wote walikuwa watu wa aina moja. Waviziaji.
Makocha wengi bora inadaiwa kuwa huwa wanatoka katika eneo la kiungo na ulinzi. Ni kwa sababu mara nyingi katika maisha yao ya soka kama wachezaji walikuwa wanakaa sehemu ambao wanautazama mpira katika mapana yake na wanaweza kuusoma vema mchezo.
Mfano ni kama makocha wanaotamba sasa akina Pep Guardiola, Xabi Alonso, Luis Enrique Martinez, Didier Deschamps, Mikel Arteta, Diego Simeone, Antonio Conte, na wengineo. Hawa wote walikuwa viungo. Wachache kina Ronald Koeman, Jurgen Klopp walikuwa walinzi.
Washambuliaji wengi hatari walishindwa kuwa makocha. Pele wa Brazil hakujaribu. Lionel Messi amedai hataki kuwa kocha. Maradona alichemsha. Wachache waliweza. Waviziaji kama akina Nistelrooy ndio hawa wameingia kazini.
Kwa Ruud sikutazamia lakini hivi tunavyozungumza ni kwamba msimu wa 2022/23 pale Uholanzi alitwaa ngao ya hisani na kombe la FA la Uholanzi akiwa na PSV Eindhoven. Baadaye aliondoka kwa sababu anadai alikosa sapoti kutoka kwa utawala wa timu hiyo.
Kumbe hakuja Manchester United kwa bahati mbaya. Hakuja Manchester United kwa sababu ni legendari wa timu hiyo. Hakuja Manchester United kwa sababu alikuwa anatoka nchi moja na Ten Hag. Alikuja kwa sababu alikuwa na kitu mkononi kama kocha.
Na sasa ni wakati wa kumtazama. Ni wakati wa yeye kuendelea kunithibitishia kwamba nilikuwa nimekosea kumtazama yeye kama mtu asiyefahamu mengi katika mpira zaidi ya kuuweka mpira katika wavu tu. Ni wakati wa yeye kunithibitishia kwamba ukocha ni kazi nyingine tofauti na ile kazi ya uchezaji. Ni kitu ambacho nilikuwa nakifikiria awali lakini kwa Ruud sikutazamia.
Kwa Leicester City? Nadhani Ruud ana kazi ya kututhibitishia kwamba wachezaji wa kizazi chache waliocheza England wanaweza kuwa makocha mazuri. Wenzake akina Patrick Vieira, Franck Lampard, Roy Keane, Steven Gerrard wote walipewa timu na wamechemsha katika ligi kuu ya England.
Kwa sasa tuna majina ya makocha ambao hawakutamba enzi zile za Ligi kuu mwanzoni mwa miaka ya 2000. Enzi zile wakati akina Roy Keane na Patrick Vieira wakishikana mashati mara kwa mara. Huenda yeye akawa na kitu tofauti kwa Leicester City ambayo katika miaka ya karibuni inaonekana kuyumba baada ya kutwaa ubingwa wa maajabu wa England 2016.