NYUMA YA PAZIA: Mbappe amefungua mlango, ‘Real Madrid is typing…’

OSCAR Wilde mshairi mahiri wa zamani wa Ireland aliwahi kusema “kama hautachelewa sana nitakusubiri kwa maisha yangu yote.” Wilde alizaliwa Oktoba 16, 1854 akafariki dunia katika Jiji la Paris, Ufaransa, Novemba 30, 1900.

Ni katika jiji hili hili la Paris alilofariki ndipo juzi Kylian Mbappe amewaambia PSG hana mpango wa kubakia tena klabuni hapo pindi mkataba wake utakapofika mwisho pindi michuano mbalimbali itakapofika tamati mwishoni mwa msimu.

Kuna staa kama Mbappe katika soka kwa sasa? Labda Erling Haaland. Habari hii imevumisha mawimbi kidogo. Ni muda wa dunia kutafakari. Mbappe atakwenda wapi. jibu lake ni rahisi. Real Madrid. Naona kabisa Real Madrid wakiwa wanafanya ‘typing’ kwa sasa katika kurasa zao za mitandao ya kijamii.

Hawawezi kumaliza kuandika kwa sasa mpaka mwisho wa msimu kwa sababu Mbappe yupo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na PSG na kuna uwezekano mbele ya safari akakutana na Real Madrid. Halitakuwa jambo lenye afya kwa timu zote mbili.

Yaani pambano kuchezwa huku kukiwa na mchezaji mmoja ambaye anatarajiwa kwenda katika timu nyingine mwishoni mwa msimu.

Suala la Mbappe kwenda Real Madrid lilikuwa la muda tu. Mei 2022 Mbappe alitangaza kubakia PSG huku akiacha hasira kubwa kwa Madrid pamoja na bodi ya Ligi Kuu ya Hispania ambao walishaamini wamempata staa huyu wa Ufaransa.

Niliandika wakati ule, Mbappe alikuwa ananunua muda tu lakini dili lake la kwenda Madrid bado lilikuwa njiani. Wakati ule alipoamua kubakia alikuwa na miaka 23. Haraka ya nini? Leo ana miaka 25 na bado ni kijana mdogo. Angekuwa na miaka 29 tungeweza kusema anachelewa.

Nadhani hata Madrid wenyewe walikubali kusubiri kama alivyosema Oscar Wilde ‘Kama hautachukua muda mrefu basi nitakusubiri kwa maisha yangu yote.” Na ni kama ambavyo Mbappe mwenyewe alisubiri kwenda Real Madrid.

Kwa nini nimeifikiria Madrid na ligi kuu ya Hispania? Sababu ni mbili. Kama sio Hispania basi ningemfikiria Mbappe kwenda England. Hata hivyo sioni timu ambayo Mbappe anaweza kwenda England kwa sasa. Manchester City hawaonekani kuhangaika na Mbappe lakini hapo hapo wana kesi nyingi za kuvunja kanuni za matumizi ya fedha pale UEFA.

Manchester United? Wana pesa lakini kwa sasa wamezidiwa hadhi na Mbappe. Kama hawana uhakika hata wa kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao, achilia mbali kutwaa ubingwa wowote mkubwa kwa sasa Mbappe anawezaje kufikiria kwenda huko?

United ni kama Chelsea tu ambayo kwa sasa haina uelekeo. Wakati huo huo Arsenal na Liverpool hazina pesa ya kutosha kumudu kuipata saini ya Mbappe.

Haishangazi kuona Mbappe anaenda Madrid kwa sababu hata wakubwa wengine wa pale Barcelona wapo hoi kipesa.

Madrid wamepigana vita hii kikubwa kabla Mbappe hajakataa kwenda kwao Mei 2022. Wameshirikiana na watu wa Bodi ya La Liga ambao wana kiu kubwa ya kumwona Mbappe anatua Hispania kwa sababu ligi yao inakosa mchezaji maarufu mwenye hadhi ya ustaa uliopitiliza (League icon).

Tangu kuondoka kwa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi halafu na Karim Benzema pia akaondoka, hawajapata staa mkubwa wa kutengeneza hadhi kubwa katika ligi yao. Hata mechi za El Clasico zimekosa msisimko kwa sababu hazina wachezaji wenye hadhi kubwa.

Kwa Waingereza hali ni tofauti. Wana timu nyingi zenye hadhi kubwa ambazo zinashindana lakini pia wana mchezaji kama Haaland ambaye ni kivutio achilia mbali akina Kevin de Bruyne, Bukayo Saka, Bruno fernandes na wengineo wengi ambao wanatengenezewa ukubwa wa majina yao sio tu kwa sababu ya ubora wao lakini pia namna Ligi yao ilivyopokelewa katika mataifa mengi tofauti.

Lakini kwa Mbappe mwenyewe nadhani ameona kuna nafasi kubwa kwake kuja kuwa mwanasoka bora wa dunia akiwa na Real Madrid kuliko ilivyo sasa akiwa na PSG.

Hawa jamaa wa Paris wamepambana kwa kila walivyoweza kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya lakini hadi sasa wameshindwa.

Wamepambana wakiwa na Zlatan Ibrahimovic, Edinson Cavani, Mbappe mwenyewe, Lionel Messi, Neymar lakini imeshindikana. Mbappe anafahamu kwa Real Madrid hilo sio tatizo. Hilo kombe wakati mwingine linawafuata wao wenyewe.

Wakati fulani hapa juzi juzi walilitwaa mara tatu mfululizo chini ya Zinedine Zidane na Cristiano Ronaldo. Mbappe ametwaa kombe la dunia lakini anahitaji kutwaa La Liga pamoja na ubingwa wa Ulaya kwa ajili ya kufikiriwa kuwa mwanasoka bora wa dunia.

Unaweza kuliona hili kwa msimu uliopita tu wakati Messin alipolalamikiwa kutwaa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia kwa kutwaa kombe la dunia. Bado walalamishi waliamini mchezaji aliyestahili angeweza kuwa Haaland. Kwa nini hakutajwa Mbappe? Ni kwa sababu Haaland aliiongoza Manchester City kutwaa mataji matatu mwishoni mwa msimu uliopita.

Mpaka sasa Haaland yupo mbele ya Mbappe kwa sababu Manchester City inambeba na anaibeba. Mbappe anaibeba PSG lakini timu yenyewe haimbebi. Walau akienda Madrid atakutana na wataalamu kina Vinicius, Toni Kroos, Luka Modric, Jude Billingham na watajaribu kubebana.

Mwisho wa kila kitu ni ukweli licha ya kuwa na ndoto hii ya kuchukua tuzo ya mwanasoka bora wa dunia, lakini Mbappe bado anaenda kuogelea katika noti za soka. Fikiria katika jina kama lake na umri kama wake anakwenda zake Real Madrid akiwa mchezaji huru.

Hapa hesabu zinakuwa rahisi tu. kama katika soko halisi Madrid wangeweza kutoa Euro 250 milioni kumnunua Mbappe, sasa hivi kinachoweza kufanyika ni wao kutoa Euro 150 milioni kumpa Mbappe mwenyewe.

Madrid watakuwa wamempata Mbappe bila ya gharama kubwa. Na hapo hapo kiasi ambacho kitabakia katika zile Euro 250 milioni kinaweza kwenda katika mishahara yake. Hivi ndivyo hesabu za mchezaji huru zinavyokwenda.

Lakini Madrid pia wanaweza kujikuta wakirudisha pesa hizi bila ya shida kwa kuzingatia mauzo ya jezi yake, pamoja na matumizi ya sura yake katika bidhaa yake. Hii ni achilia mbali kuongezeka kwa thamani ya klabu katika soko la hisa.