Nooij anatumia mfumo wa kizamani bila ya kujua
Muktasari:
Katika mpangilio huo, mwalimu huoanisha jinsi idara moja inavyotakiwa kusaidiana na idara nyingine ndani ya timu kuanzia kwa golikipa, walinzi, viungo hadi washambuliaji na kisha jukumu la kila mchezaji ndani ya uwanja.
MFUMO ni mpangilio wa wachezaji wanavyojipanga uwanjani ili kutekeleza majukumu waliyopewa na mwalimu wa timu kocha au meneja wao.
Katika mpangilio huo, mwalimu huoanisha jinsi idara moja inavyotakiwa kusaidiana na idara nyingine ndani ya timu kuanzia kwa golikipa, walinzi, viungo hadi washambuliaji na kisha jukumu la kila mchezaji ndani ya uwanja.
Kitu kinachoweza kuzitofautisha timu mbili zinatumia mfumo unaofanana ni mbinu binafsi za kocha alizowapa wachezaji wake na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja.
Kwa wale wanaujua muziki wa dansi hasa ule wa kutoka Jamhuri ya Kidemokaria ya Congo (DRC) ni kwamba bendi zote zinaweza kutumia mtindo mmoja, mfano Mayenu lakini tofauti ya utamu wa muziki kati ya bendi na bendi ni jinsi wanamuziki wanavyopiga vyombo kurutubisha nyimbo zao.
Pia, mifumo ya soka imekuwa ikibadilika siku hadi siku ikitegemea na makocha na aina ya wachezaji walionao.
Moja ya mifumo ya awali ambayo nchi nyingi ziliitumia kwa muda mrefu ni huu wa 4:2:4 ambao ulikuwa unamtambulisha mchezaji mmoja mmoja katika nafasi yake, ulikuwa ni mfumo uliotegemea uwezo wa wachezaji binafsi zaidi na huku mchezo ukiwa si wa pamoja, yaani timu hazikuwa na muunganiko wa pamoja ‘team work’.
Hapa Tanzania ndipo ulipowakuta wachezaji wakiwa na viwango vyenye ubora kila nafasi kuanzia mabeki hadi washambuliaji. Hebu tujaribu kuangalia jinsi timu yetu ya taifa, ‘Taifa Stars’ ilivyocheza katika siku za hivi karibuni na kusababisha watu kuanza kumlaumu, hasa baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Msumbiji Jumapili iliuopita.
Hapa ndipo ninapomuuliza Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij kwamba anajua kama mfumo anaotumia ni wa kizamani au hajui hilo? Siku alipokuwa akiitangaza timu ya taifa kujiandaa na mchezo dhidi ya Msumbiji, aliwaita Simon Msuva, Elias Maguli, Mrisho Ngasa, John Boko, Thomas Ulimwengu na Mbwana Samata kama washambuliaji.
Pia, akawaita kina Mwinyi Kazimoto, Erasto Nyoni na wengineo kama viungo na hata ukiwaona wanavyokuwa wamepangwa uwanjani utajua tu hawa ni viungo.
Sasa unapokuwa umewapanga Ngassa, Boko, Samata na Ulimwengu ambao ni washambuliaji wanne kisha unawapanga Kazimoto na Nyoni katika viungo, hawa wapo wawili tu, huku ukiwatumia Shomari Kapombe, Oscar Joshua, Nadir Haroub na Kelvin Yondani kama mabeki! Huu si mtindo wa zamani wa 4:2:4 ambao kina Edibily Lunyamila,
George Masatu na kina Hussein Marsha ndivyo walivyocheza? Hawa vijana wetu hawachezi mfumo huu kwenye vilabu vyao, ni vipi wataweza kwenda sawa na maono ya kocha?
Hapa lazima utamuona Ngassa akicheza ndivyo sivyo na wataalamu wajuaji watakwambia Ngassa ameshuka kiwango, huku wakijua kuwa mchezaji huyo ni mzuri akicheza huru na nafasi ikiwa kubwa yaani acheze nyuma ya mshambuliaji wa kati.
Unamweka Ulimwengu na Boko ambao kiasilia ni wachezaji wa kati zaidi huku Ulimwengu akiwa na faida kwa sababu anaokuwa na uwezo wa kukimbia na kutumia nguvu.
Boko anangojea tu kufunga, Samatta ni mchezaji mwenye uwezo wa kushuka chini kidogo kuchukua mipira na kutembea nayo, naye anapenda kutanua uwanja. Samatta ni mzuri zaidi akicheza nyuma ya mshambuliaji wa mwisho.
Nooij amtumie Ulimwengu, Boko akiwa benchi na Samatta huku Ngassa akiwa benchi, aongeza viungo watatu zaidi ili wafanye kazi kwa ufasaha. Bila ya hivyo, tutaendelea kuwalaumu akina Nyoni, Joshua, Yondani wakati tatizo linaanzia kwenye mfumo huo wa kizamani.