Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Noela: MVP kikapu mara 5 anayefananishwa na Chama

MVP Pict

Muktasari:

  • Lakini, umewahi kufikiria ni namna gani mwanamichezo anapofananishwa na mwanamichezo au mchezaji wa mchezaji wa mchezo mwingine tofauti na ule anaoucheza, anavyojisikia? Basi elewa kwamba kuna kitu ambacho humfanya mhusika kujisikia vizuri na hasa ikiwa anayefananishwa naye amewahi au anafanya mambo makubwa katika mchezo anaoucheza.

KUNA maisha mengine ndani na nje ya michezo yanafurahisha sana. Yanatia moyo. Lakini kuna wakati yanakatisha tamaa kwa mhusika kuamua kuuweka kando mchezo husika akiamini kwamba hawezi kutoboa kutokana an kile kinachoendelea. Hata hivyo, upande wa kufurahisha ndio huwa lengo haswa na mchezo husika na mwanamichezo kwani lengo lake ni kufurahi huku akiwafurahisha wanaomfuatilia kupitia mchezo husika.

Lakini, umewahi kufikiria ni namna gani mwanamichezo anapofananishwa na mwanamichezo au mchezaji wa mchezaji wa mchezo mwingine tofauti na ule anaoucheza, anavyojisikia? Basi elewa kwamba kuna kitu ambacho humfanya mhusika kujisikia vizuri na hasa ikiwa anayefananishwa naye amewahi au anafanya mambo makubwa katika mchezo anaoucheza.

Kwa mchezaji wa kikapu wa Jeshi Stars, Noela Renatus kufananishwa na Clatous Chama, yule kiungo mshabuliaji mahiri wa Yanga ni jambo la kujivunia kwake, na hasa kwa kuwa mfanano huo umetokana na kazi kubwa anayoifanya uwanjani inayofananishwa na staa huyo wa soka aliyewahi pia kukipiga Simba.

“Kuna kipindi watu walinitungia jina la Clatous Chama. Hilo lilitokana na namna ya urushaji wa mipira yangu iliyokuwa inafika kwa wahusika... wakawa wanalinganisha na pasi za Chama zilivyokuwa zimenyooka kipindi hicho ni panga pangua Simba. Hivyo nikawa namfuatilia kwa ukaribu zaidi aina ya mazoezi yake na nidhamu,” anasema Noela ambaye pia shabiki lialia wa Simba.

Anasema lengo lake kubwa ni kuandika historia na ushawishi mkubwa kupitia mchezo huo akiwaonyesha mabinti kwambna hakuna kitu kinachoshindika iwapo mtu atatia juhudi ili kujitegemea kiuchumi.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, Noela anasema anajifunza kupitia wanawake wanaofanya mambo makubwa katika michezo mbalimbali kama mchezaji wa tenisi wa zamani, Serena Williams; mcheza kikapu wa Marekani, Brittney Griner na wengine wengi ambao wana ushawishi mkubwa duniani.

“Mtazamo katika maisha unaweza ukakufelisha ama kukupa mafanikio. Mfano hapa Tanzania mchezo unaopendwa zaidi ni wa mpira wa miguu, ila naamini ikitokea tukafanya makubwa watu wapate ushawishi wa kuupenda mchezo wa kikapu,” anasema.

“Kikubwa ni kujitambua zaidi, kwani kupitia mchezo huu naweza nikafanya vitu vingine vya ziada mfano urembo. Wapo watu wengi wakiniona muonekano wangu wanaona naweza nikafanya fasheni ama kupata matangazo. Hayo yote yatafanyika nikicheza kwa kiwango na nidhamu ya juu.”

Anasema kujifunza kwake hakujachagua mpira wa kikapu pekee, kwani kuna wakati anatazama Ligi Kuu Bara akiona wachezaji wanaofanya vizuri anaiga mazuri yao na kuyafanyia kazi ili aendelee kuwa bora zaidi.


MVP MARA 5

Noela anasema amefanikiwa kuwa mchezaji mwenye thamani zaidi yaani MVP kwa vipindi vitano tofauti kwani 2021 akicheza mashindano ya Taifa (Taifa Cup) alichukua ubingwa wa Taifa wa Ligi ya Kikapu (NBL) na All Star Ligi ya Kikapu Dar es Salaam (RBA), 2022 RBA na 2024 Taifa Cup na 2025 anatarajia atafanya vizuri, na huenda akachukua tena tuzo mbalimbali katika Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam iliyosimama kwa muda kupisha Taifa Cup inayofanyika Dodoma.

“Matarajio yangu ya kwanza kwa mwaka huu ni timu nayoichezea kuchukua ubingwa wa BDL na ikiwezekana kuwa miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri ndiyo maana najituma katika mazoezi binafsi na ya timu kwa ujumla,” anasema Noela.

“Ligi ya mwaka huu ina ushindani mkali unaotokana na udhamini ambapo timu ikishinda kila mchezaji na watu wa benchi la ufundi tunaingiziwa kiasi cha Sh87,500 katika simu baada ya mchezo. Hilo linatupa chachu ya kujipatia pesa inayoongeza kipato chetu.”

Mbali na hilo, anasema anajifunza vitu vingi kupitia wachezaji waliowahi kucheza Ligi Kikapu Marekani (NBA), akiwemo Mtanzania Hasheem Thabeet anayechezea Dar City kwa sasa kutokana na nidhamu yake ya mazoezi na namna anavyotafsiri mambo mbalimbali kwa haraka uwanjani.

“Mchezaji kama Thabeet japokuwa hatuchezi naye timu moja kuna wakati anakuwa na hamu ya kufanya makubwa zaidi kila anapopata fursa, na ikumbukwe ni mchezaji mwenye mafanikio makubwa katika mchezo huo. Hilo kwangu ni funzo la kutobweteka na kujua nina safari ndefu,” anasema Noela.

“Baadhi ya timu zinazoshiriki ligi ya BDL zimesajili wachezaji kutoka nje, hivyo na sisi tukifanya vizuri twende nje ili kuwafungulia milango wengine ambao watakuja nyuma yetu kuona mchezo wa kikapu unalipa kama ilivyo michezo mingine.

“Zamani ilikuwa inaonekana mchezaji wa kikapu ni lazima awe mrefu, ila kwa sasa anacheza mtu yeyote, kikubwa ni mbinu, ufundi na kipaji. Hilo linanipa nguvu ya kujifunza bila kuchoka kwa wachezaji wakubwa kujua wanafanya kitu gani hadi wanafanikiwa na kuwa na ushawishi mkubwa katika jamii zinazowazunguka.”


PESA ZA KIKAPU ZIMEMSOMESHA

Tangu Noela aanze kucheza kikapu kupitia timu tatu za Ukonga Queens, Vijana Queens na sasa Jeshi Stars anayodai ni timu ambayo imempa pesa ndefu na kufanikisha masomo yake.

“Jeshi Stars ilinisajili kutoka Vijana Queens nikiwa kidato cha nne, ndiyo timu iliyonilipia ada hadi nimemaliza chuo. Nimesomea mambo ya meneja rasilimali watu. Kwangu hayo ni mafanikio makubwa,” anasema Noela.

“Mbali na elimu nimefanya vitu vingi siwezi kuweka kila kitu wazi. Naamini kadri nitakavyoendelea kucheza ndivyo nitakavyonufaika na matunda ya kipaji changu.”

Mchezaji huyo anafafanua kwa nini mchezo wa kikapu unaonekana wa watu wasomi zaidi duniani akisema: “Vipaji vinaibuliwa kuanzia shuleni ndiyo maana inakuwa rahisi kuendelezwa kimasomo. Mfano ni mimi timu iliponiona kuanzia kidato cha nne viongozi walinisimamia kwa upande wa elimu, ingawa sina maana kwamba lazima uchezwe na wasomi pekee.”