NJIAPANDA: Utabiri wa wapi mastaa hawa wataenda mikataba yao ikimalizika mwisho wa msimu
Muktasari:
- Kylian Mbappe alifanya hivyo alipohamia Real Madrid kutoka Paris Saint-Germain mwaka 2024, na Trent Alexander-Arnold alimfuata Bernabéu msimu uliopita, akiamua kuondoka katika klabu yake ya utotoni, Liverpool.
LONDON, ENGLAND: KILA mwaka, mikataba inayomalizika huleta hatari kwa baadhi ya klabu huku ikifungua milango kwa wachezaji wakubwa kujiunga na timu mpya, wengine wakichagua kumaliza mikataba yao kabla ya kuondoka.
Kylian Mbappe alifanya hivyo alipohamia Real Madrid kutoka Paris Saint-Germain mwaka 2024, na Trent Alexander-Arnold alimfuata Bernabéu msimu uliopita, akiamua kuondoka katika klabu yake ya utotoni, Liverpool.
Marc Guehi angeweza kuondoka bure majira ya joto ya 2026 kama Crystal Palace wasingemuuzia Manchester City mwezi Januari.
Hata hivyo, bado kuna majina makubwa katika soka la dunia yatakayokuwa hayana mkataba majira ya joto yajayo na hapa tunatabiri wapi wachezaji 10 kati yao wataishia.
Dayot Upamecano – Bayern Munich
Upamecano ni mchezaji wa Bayern Munich tangu 2021 na amekuwa na kiwango kizuri na cha kuaminika.
Kuna klabu kubwa zinazotamani mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 apatikane bure, huku mkataba wake wa Bayern ukimalizika majira yajayo ya kiangazi.
Hata hivyo, ripoti za mapema mwaka huu zilidokeza alikuwa karibu kuongeza mkataba na klabu hiyo.
Ingawa mazungumzo yamekwama kidogo kutokana na masharti ya mkataba na Bayern wakitaka kumbakiza beki wao wa kati, inaonekana kuna uwezekano mkubwa ataendelea kubaki hapo.
Ibrahima Konate – Liverpool
Mustakabali wa Upamecano unaweza pia kuathiri hatima ya Konate. Beki huyo wa Liverpool amekuwa akifuatiliwa na Bayern Munich na Real Madrid, ingawa Los Blancos walijitoa baada ya kiwango chake kushuka.
Iwapo Bayern watambakiza Upamecano, huenda wasimhitaji Konaté, ambaye mkataba wake na Liverpool bado uko kwenye hali ya sintofahamu.
Imependekezwa msimu mzima kuwa Konaté amekataa ofa kadhaa za mkataba. Hata hivyo, ana masharti mezani ambayo yakitimia, ataendelea kusalia Anfield.
Dusan Vlahovic – AC Milan
Tetesi za hivi karibuni zinaonyesha kuwa AC Milan na Barcelona zinamtaka Vlahovic. Kuichezea Barcelona ni heshima kubwa, lakini kuondoka kwenye ligi anayoiweza kwenda mazingira mapya kunaweza kuwa hatari.
Kuhamia Milan kutamweka Vlahovic ndani ya Serie A, ligi ambayo ameichezea tangu 2018, kwanza Fiorentina kisha Juventus.
Katika mechi 215 za Serie A, Vlahovic ana mabao 90 na asisti 18. Kuhamia Milan kutamruhusu kuongeza takwimu hizo, akiendelea kucheza katika nchi ambayo ameizoea na ana uwezo mkubwa.
Bernardo Silva – Barcelona
Kwa miaka mingi, Barcelona imekuwa ikimtaka Bernardo Silva, lakini hali yao ya kifedha imekuwa kikwazo cha kumsajili mmoja wa wachezaji muhimu zaidi wa Manchester City.
Hata hivyo, ukweli Barca imeendelea kumtamani kwa muda mrefu na sasa mkataba wake unakaribia kumalizika, unaweza kuwapa mabosi wa Barca nafasi nzuri ya kumsajili.
Silva anajua anathaminiwa kwa muda mrefu na kuhamia Barcelona kutampa fursa ya kuendelea kushinda mataji katika ngazi ya juu. Akiwa na umri wa miaka 31, bado ana miaka kadhaa ya kucheza kwa kiwango cha juu.
Mike Maignan – Chelsea
Katika mwaka mmoja uliopita, imeonekana ni suala la muda tu kabla Maignan hajajiunga na Chelsea. Ameendelea kuwa kwenye rada yao baada ya AC Milan kudai ada kubwa majira ya joto yaliyopita, huku Robert Sánchez akishindwa kuwathibitishia Blues anastahili jezi namba moja Stamford Bridge.
Hivi karibuni, imeelezwa kuwa kocha mpya Liam Rosenior ameidhinisha Chelsea kumsajili Maignan na ikizingatiwa kuwa kipa huyo yuko tayari kuhama, huenda hakuna kitakachozuia dili hilo.
Ruben Neves – Man United
Kwa kuondoka kwa Casemiro, Manchester United watahitaji kuimarisha safu ya kiungo. Tayari wamekuwa wakifuatilia wachezaji kama Carlos Baleba, Adam Wharton na Elliot Anderson.
Hata hivyo, wachezaji hao watagharimu pesa nyingi na ikiwa Man United inahitaji viungo wawili, huenda wakajikuta katika mzigo mkubwa wa kifedha.
Kwa hiyo, kumsajili Neves, ambaye inasemekana anatamani kutua Old Trafford kunaweza kuwa chaguo bora, kwani hatagharimu ada ya uhamisho, bali mshahara mkubwa tu na ana uzoefu mkubwa wa kucheza Ligi Kuu England.
Serge Gnabry – Bayern Munich
Kama ilivyo kwa Upamecano, Gnabry pia yuko mwishoni mwa mkataba wake Bayern, lakini mazungumzo ya kuongeza mkataba yanaendelea.
Inasemekana winga huyo wa Ujerumani yuko tayari kupunguza mshahara wake na mazungumzo bado yanaendelea, ndiyo maana hajatia saini mkataba mpya wala kuafikiana na klabu nyingine.
Harry Wilson – Everton
Wilson amekuwa na ofa ya mkataba kutoka Fulham, ambako amecheza mechi 171 tangu 2021.
Hata hivyo, inaaminika mazungumzo yamekwama, huku Leeds na Everton zikionyesha nia ya kumsajili winga huyo.
Leeds ilimtaka Wilson majira ya joto yaliyopita lakini walishindwa kumpata, huku Everton wakikabiliwa na hatari ya kupoteza nguvu ya kushambulia majira yajayo.
Jack Grealish alianza vizuri sana akiwa kwa mkopo Everton, lakini kiwango chake kimeshuka na jeraha linaloweza kumuweka nje kwa muda linafanya uhamisho wa kudumu kuwa na mashaka. Hali hiyo inaweza kumshawishi Wilson kuwa atakuwa mchezaji muhimu wa kushambulia katika klabu iliyo katikati ya msimamo wa Ligi Kuu, juu zaidi ya Leeds wanaomwania pia.
Casemiro – Saudi Pro League
Kumekuwepo na tetesi kuwa Casemiro anaweza kurejea Brazil, huku mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 akithibitisha ataondoka Manchester United majira ya joto yajayo.
Amezichezea klabu kubwa mbili duniani, Real Madrid na Manchester United na ikiwa atalazimika kuchagua kati ya Brazil na Saudi Arabia, inaonekana ataelekea Saudia.
Baada ya taaluma kubwa aliyokuwa nayo, huku akilipwa takribani Pauni 350,000 kwa wiki hivi karibuni, ni vigumu kuona akipunguza mshahara wake kwa kiwango kikubwa kama ataenda Brazil.
Al-Hilal, Al-Ahli, Al-Nassr na Al-Ittihad ni miongoni mwa klabu zinazoweza kumpa makazi Saudi Arabia.
John Stones – Napoli
Stones amekumbwa na matatizo makubwa ya majeraha katika misimu ya hivi karibuni na Manchester City huenda ikaamua kuondoa mkataba mkubwa wa mchezaji ambaye hachangii sana kwa sasa.
Kwa mujibu wa TEAMtalk, Napoli, AC Milan, Como, Atletico Madrid, Bayern Munich pamoja na klabu za Saudi Arabia na Amerika Kaskazini zinamfuatilia beki huyo wa England.
Kuhamia Napoli, ambako Scott McTominay amefufua kiwango chake na Antonio Conte anataka kuleta mastaa zaidi kutoka England, kunaweza kuwa chaguo bora. Ni fursa ya kuendelea kucheza soka la kiwango cha juu, kulipwa vizuri na mfumo wa Napoli unaonekana rahisi kuuzoea kama alivyothibitisha McTominay.