Amorim: Wakikosa timu tunaishi nao
Muktasari:
- Jadon Sancho, Antony, Alejandro Garnacho na Tyrell Malacia bado wapo njiapanda juu ya hatima zao za kuondoka kwenye timu hiyo baada ya Kocha Amorim kuwaambia watafute pa kwenda.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim huenda akafungua milango kuwakaribisha kikosi mastaa wanne asiowataka endapo kama watashindwa dili za kuwaondoa jumla Old Trafford.
Jadon Sancho, Antony, Alejandro Garnacho na Tyrell Malacia bado wapo njiapanda juu ya hatima zao za kuondoka kwenye timu hiyo baada ya Kocha Amorim kuwaambia watafute pa kwenda.
Sancho aligomea ofa ya kwenda AS Roma, huku klabu hiyo ya Italia ikihitaji pia saini ya Malacia, wakati Garnacho akiamini Chelsea itakuja kumsajili na Antony akitaka arudi Real Betis baada ya kutumikia nusu ya pili ya msimu uliopita kwa mkopo kwenye kikosi hicho cha La Liga.
Lakini, hakuna uhakika kama wachezaji hao wote au baadhi watapata timu za kujiunga nazo kabla ya dirisha la usajili England halijafungwa, Septemba 1.
Kocha Amorim ametoa matumaini kwa wachezaji kupata nafasi ya kujumuika na wenzao kwenye kikosi endapo watashindwa kuondoka.
Amorim alisema: "Ipo wazi wachezaji hawa wanataka kwenda kucheza kwenye klabu nyingine, hivyo tunajaribu kuwatengenezea mazingira ambayo wote yatatufanya tuwe na furaha na wanafurahia. Lakini, dirisha litakapofungwa itabidi tuwapokee wachezaji ambao hawajahama na baada ya hapo chochote kinaweza kutokea."
Maneno hayo yanaweza kupoza moyo wa Garnacho baada ya kutibuana na kocha mwishoni mwa msimu uliopita na Amorim alimwambia "apige sala apate timu nyingine ya kwenda."
Man United imefungua milango ya kupokea ofa kwa wachezaji hao wanne, ikiwa tayari kuwauza hata kwa hasara ili kuwaondoa kwenye kikosi. Kocha Amorim na mkurugenzi wa soka, Jason Wilcox bado wanahitaji wachezaji wapya zaidi kwenye kikosi baada ya kuwasajili Matheus Cunha, Bryan Mbuemo, Benjamin Sesko na Diego León kwa ada inayokaribia Pauni 200 milioni.
Kipa mpya anahitajika baada ya Andre Onana na Altay Bayinder kufanya makosa mengi, huku klabu hiyo ikihusishwa pia na kiungo mkabaji.