NJE YA BOKSI: Mapambano haya yaliwaletea neema

Muktasari:

  • Haijalishi bondia atapigana kwa muda gani. Wapo wanaopanda na kushuka kwa maana ndani ya sekunde chache tu wameshakalishwa, lakini hilo haliwazuiii kuchota chao. Malipo kama kawa.

NEVADA, MAREKANI: Kazi kazi. Mchezo wa ngumi ni moja ya michezo inayolipa pesa ndefu kwa mabondia kupanda ulingoni.

Haijalishi bondia atapigana kwa muda gani. Wapo wanaopanda na kushuka kwa maana ndani ya sekunde chache tu wameshakalishwa, lakini hilo haliwazuiii kuchota chao. Malipo kama kawa.

Ni moja ya michezo ambayo uhakika wa pesa ni nje nje. Hakuna longolongo. Hunilipi, sipigani.

Ingawa kuna mabondia wamekuwa wakiingia kwenye mtego wa kudhulumiwa lakini wapo wanaosaini kupigana na wapinzani wao kwa pesa ndefu.

Wapo wanaofanya makubaliano maalumu na wanaotafutwa na mapromota kuwakutanisha wakiamini watatengeneza pesa za kutosha.

Wapo wanaopigana mapambano mengi kusaka pesa ndogo ndogo, na wengine pambano moja tu lakini pesa anayopata ni ‘funga mwaka’.

Haya hapa mapambano yaliyowahi kuzalisha pesa nyingi katika historia ya mchezo huu kutokana na pesa za viingilio na wanaotazama kwenye mtandao mbalimbali na kufanya mabondia kukusanya pesa nyingi.


Floyd Mayweather vs Manny Pacquiao - Mei 2015

Wengi hupenda kuliita ni pambano la karne. Hili ndio pambano lililowahi kuzalisha pesa nyingi zaidi kuwahi kutokea katika historia ya mchezo wa ngumi hadi sasa.

Pambano hili lililofanyika Ukumbi na MGM Grand Garden, Nevada Marekani tiketi ya bei ya chini kabisa ilikuwa ikiuzwa Dola 1,500.

Jumla ya watu milioni 4.6 walinunua tiketi za kutazama mechi, wengine wakalipia kutazama mtandaoni.

Pauni 333 miulioni ilikuwa ni malipo ya kutazama mtandaoni wakati Pauni 58 milioni yakawa ni malipo ya viingilio getini.

Jumla ya Pauni 678 milioni ikazalishwa kupitia pambano hilo na Mayweather ambaye alishinda kwa pointi akachukua Pauni 223 milioni wakati Pacquiao akiondoka na Pauni 122 milioni.


Floyd Mayweather vs. Conor McGregor - Agosti 2017

Lilipewa jina la  ‘The Money Fight’ yaani pambano la pesa.

Mabondia hawa walikutana katika Ukumbi wa T-Mobile, Nevada Marekani.

McGregor hakuwa anacheza ngumi alitoka kwenye mchezo wa UFC na kutokana na kukosa uzoefu alipoteza na akampa nafasi ya Mayweather kushinda pambano lake la 50.

Jumla ya pesa zilizopatikana ilikuwa ni Pauni 662.5 milioni na Pauni 325 milioni zilitokana na watu waliolipia kutazama mtandaoni, Pauni 44 milioni mapato ya getini.

Mayweather ambaye baada ya hapo alistaafu alikunja Pauni 223.5 mlioni huku McGregor akipata Pauni 70 milioni.


 Floyd Mayweather vs Canelo Alvarez - Septemba 2013

Pambano dhidi ya Canelo mwaka 2013 halikuwa na pesa nyingi ingawa si haba.

 Mayweather  alishinda kwa pointi mbele ya mashabiki 16,000 ndani ya Ukumbi wa MGM Grand kutazama pambano.

Jumla ya Pauni 214 milioni zilizalishwa kupitia mtandaoni, Pauni 20 milioni ilikuwa ni malipo ya tiketi za kuingilia uwanjani.

Mayweather akaondoka na Pauni 65 milioni na Canelo akapata Pauni 9.7 milioni.


 Floyd Mayweather vs. Oscar De La Hoya - Mei 2007

Ndio pambano la kwanza la pesa nyingi kwa Mayweather na wakati huu, hakuwa na jina kubwa kama ilivyokuwa kwa Oscar De La Hoya na ndiye aliyekuwa maarufu zaidi na hata kwenye mgawo wa pesa alipata mara mbili ya Mayweather.

Hata hivyo, Myweather ndiye aliyeibuka mshindi kulikochangia kumnyanyua na kujulikana kimataifa.

Pambano hilo lilizalisha Pauni 187 milioni na La Hoya akapata Pauni 42 mlioni, huku Myweather akipata Pauni 20 milioni.

Pesa zilizopatikana mtandaoni ni Pauni 110 milioni na viingilio vya mlangoni Pauni 15 milioni.


Evander Holyfield vs. Mike Tyson II - 1997

Pambano la tano lililokuwa na pesa ndefu ni la mwaka 1997. Jumla ya Pauni 145 milioni zilipatikana na hiyo ilitokana na watu wengi kutaka kujua nini kitatokea.

Tyson na Evander walikutana kwa mara yakwanza mwaka 1996, Tyson akachezea kichapo. Hivyo mechi hii iliyopigwa mwaka 1997 ilikuwa na lengo la Tyson kulipa kisasi na usiku wa pambano hilo kwenye Ukumbi wa MGM Grand Garden mshindi hakupatikana kutokana na kitendo cha Tyson kumng’ata sikio Evander zaidi ya mara moja.

Katika pambano hilo, Pauni 81.4 milioni zilipatikana kutokana na malipo ya watazamaji wa mtandaoni na Pauni 11.6 milioni ni viingilio vya getini.


Lennox Lewis vs. Mike Tyson - 2002

Hili ndio pambano la mwisho kuwakutnisha wawili hawa na Tyson alipoteza raundi ya nane mbele ya Lewis aliyekuwa bingwa wa uzito wa juu.

Jumla ya watu 15,000 walikuwa kwenye uwanja wa Pyramid Memphis, Tennessee, Marekani.

Jumla ya Pauni 132 milioni zilipatikana, Pauni 90 milioni kutokana na malipo ya waliotazama mtandaoni   na Pauni 14.2 milioni viingilio vya mlangoni.

Lewis akaondoka na Pauni 14.2 milioni, na Tyson akapata Pauni 14.2 milioni pia.