Prime
Niyonzima anavyomlea mtoto wa Mafisango

UWEZO wa kiungo mchezeshaji Haruna Niyonzima aliouonyesha Ligi Kuu Bara, ndio unaomfanya aendelee kukaa kwenye kumbukumbu za wadau wa soka nchini na kwa sasa staa huyo anakipiga ALtaewun SC ya Libya.
Katika mahojiano yake na Mwanaspoti anatoa somo namna upendo wa kweli hauwezi kufa wala kuzidiwa na vitu ambavyo vinapita. Je, unataka kujua kwa nini analisema hilo, gazeti hili litakueleza kila kitu.
Niyonzima ambaye aliichezea Yanga kwa mara ya kwanza 2011-2017, kisha akajiunga na Simba 2017-2019 akarejea tena Yanga 2020/21 anasema kwa jinsi Wanajangwani walivyomuonyesha upendo akiwa Tanzania hatakaa asahau kwenye maisha yake.
Hilo linamfanya awe mstari wa mbele kwenda kuisapoti Yanga kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF), ikicheza dhidi ya Al -Merrikh, Septemba 16, Rwanda.
“Kwa namna ambavyo Yanga ilivyonikarimu naaanzaje kuacha kwenda kuiunga mkono ikiwa kwenye majukumu, hilo siyo ombi ni lazima nitakuwepo kuwapa moyo wachezaji kuhakikisha wanapambana na kushinda mechi hiyo,” anasema na kuongeza;
“Tanzania kwangu ni sehemu ya pili ya nyumbani, nimeishi kwa amani na watu wake, ndio maana hadi leo hii kuna watu nawasiliana nao kama ndugu, hivyo wanapokuja Rwanda naona ni familia yangu.”
KUHUSU YONDANI
Mwanaspoti lilifanya mahojiano na beki wa Geita Gold, Kelvin Yondani aliyecheza pamoja na Niyonzima Yanga, alifichua namna ambavyo urafiki wao ni kama ndugu, analifafanua hilo Mnyarwanda huyo.
“Mimi na Yondani tumekuwa kama ndugu na nilimwambia mwanaye atakayecheza mpira nitakuwa meneja wake na hakulikataa ombi langu kwani nitatamani nimuendeleze na afike mbali,” anasema.
Yondani ana vijana wawili wanaocheza beki Patrick (16) na Bryan (10) anayecheza namba 10 baada ya Niyonzima kujua hilo, anasema mambo mengine yatabakia kwao.
“Siyo lazima kila kitu nikiweke hadharani, kwani upendo uliopo baina ya familia yangu na Yondani ni mkubwa, hivyo hakuna linalishindikana hapo.”
Anaongeza: “Sitakaa niusahau upendo alionionyesha Yondani nikiwa Tanzania, nilichojifunza vitu haviwezi kuzidi utu ndio maana naheshimu sana mtu anayekuonyesha upendo wa dhati lazima uupe thamani.”
MTOTO WA MAFISANGO
Anachokifanya Niyonzima kwa mtoto wa Patrick Mafisango (marehemu) kinaonyesha jinsi urafiki wao ulivyokuwa wa kweli.
Baada ya Mafisango kufariki dunia Mei 17, 2012, Niyonzima alichukua jukumu la kumlea mtoto wake anayejulikana kwa jina la Crespo ambaye kwa sasa yupo kwenye timu ya watoto ya Kiyovu.
“Ni kweli Crespo yupo chini yangu. Huyo kwangu ni mwanangu kama walivyo wanangu wengine. Nikiwa nje ya Rwanda huwa nawasiliana naye mara kwa mara kujua maendeleo yake na kumfanya kuwa mwenye furaha.
“Nikirudi Rwanda basi muda mwingi nakuwa naye. Kikubwa ni kuona ndoto za maisha yake zinatimia. Sitamani kumuona akiwa mnyonge kinachotakiwa nikifanye kwake kama baba nakifanya kwa kadiri ninavyoweza.”
KUFUNGUA KITUO
Panapo majaaliwa Niyonzima anawaza kuanzisha kituo chake cha soka mwakani, malengo yake ni kuwakusanya vijana wenye vipaji na kuwasaidia kufikia ndoto zao.
Anaulizwa je, una mpango wa kuja kuchukua vipaji Tanzania kwa ajili ya kituo hicho. “ “Inshaallah hakuna linaloshindikana, kikubwa nataka kufanya kwa sehemu yangu, kuhakikisha nawasaidia vijana kuziishi ndoto zao.”
SABABU ZA KUREJEA YANGA
Niyonzima anasema aliamua kurejea Yanga kwasababu wakati akiwa Simba, alitamani kufanya hivyo ili kurejesha amani ya mashabiki wake wa Jangwani, jambo analosema anamshukuru Mungu amelitimiza hata akija kuondoka ana amani ya moyo.
“Japokuwa watu wanaojua mpira waliniunga mkono na walinitia moyo nizidi kupambana, binafsi niliona ni hekima kurejea Yanga kwa ajili ya kutengeneza na wale ambao walikuwa na kinyongo, angalau kwa sehemu naona wapo sawa nashukuru Mungu,” anasema.
Nje na kutengeneza amani, anasema viongozi walimsajili upya kwasababu anaamini waliiona huduma yake inafaa, hivyo hakusita kukubaliana nao.
“Katika maisha yangu napenda kufanya kazi kwa bidii mtu anaponipa pesa yake, sipendi kula pesa ya mtu bure na soka nalipenda kwasababu Mungu kanipa kipaji hicho, hivyo lazima nikiheshimu,”anasema.
MIAKA MINANE DAR
Niyonzima anasema Ligi ya Tanzania ina ushindani na ni bora katika Afrika Mashariki na kati, huku akishuhudia jinsi alivyoviona vipaji vikubwa.
“Ligi ya Tanzania ina ushindani mkali, kuna vipaji vya hali ya juu wachezaji wengi wanajua mpira, maana kuna tofauti ya kucheza mpira na kujua mpira, wengi wanaujua mpira, labda ninachoweza kuwashauri waamue kwenda kujaribu maisha nje na mipaka ya nchi yao.
“Mfano wapo wengi wameamua kutoka kama Mbwana Samatta, Simon Msuva, Shabaan Chilunda (amerudi), Himid Mao na wanafanya makubwa kwenye nchi nyingine, nadhani waache malengo ya kucheza Simba na Yanga kuona ndio mwisho wao, hata mimi nimecheza timu zote kubwa Rwanda APR na Rayon Sports lakini niliamua kuja kutafuta changamoto mpya.”
Ndani ya miaka miaka minane, anaifurahia zaidi sita ambayo alicheza Yanga kwa mafanikio ya hali ya juu ambapo alichukua mataji mwaka 2011, 2013, 2015,2016 na 17 alihamia Simba.
“Furaha yangu ni kuona nimecheza Yanga kwa miaka sita kwa mfululizo, huku nikifanikiwa kuipa timu yangu mataji ya Ligi Kuu, Kagame, Mapinduzi na ASFC na tulikuwa tunafanya vyema kwenye michuano ya Caf,” anasema.
Niyonzima pamoja na kuipa Yanga mafanikio, akiwa Simba nako ameacha alama ya kuchukua taji la Ligi Kuu na ASFC, ambayo yatabakia kwenye kumbukumbu ya maisha yake ya soka.
FILAMU, MUZIKI YUMO
Mbali na kipaji cha soka alichonacho, Niyonzima amecheza filamu ya ‘The Ring’ na anaweka wazi kwamba ni kazi anayoipenda na ataendelea kuifanya kadiri atakavyopata muda.
“Filamu hiyo imebeba uhalisia wa wanaume wengi kama watu watapata muda wa kuifuatilia kwa umakini itawafunza na bado haijaisha tutaendelea kuirekodi, lakini pia ninaimba muziki naingia studio narekodi na nimewahi kufanya kolabo na mwanamuziki wa Hip Hop wa Rwanda anayeitwa Jay Pole;
Anaongeza: “Lakini pia kuna nyimbo ambayo nimeitoa mwenyewe nimemuimbia mama yangu mzazi ambaye nimekaa naye kwa muda mrefu baada ya baba yangu kufariki miaka mingi.
“Huo wimbo unaelezea mapenzi yangu kwake. Namna ambavyo mama ametulea, kwani kwetu tumezaliwa watoto 12, wanaume tukiwa wanne wote tunacheza mpira na wanawake wamezaliwa wanane na mimi ni wa nane kuzaliwa kati ya watoto hao,” anasema Niyonzima ambaye alipachikwa jina la utani la Fabregas.