Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIONAVYO: Simba, Yanga katikati ya mtego

Nionavyo Pict
Nionavyo Pict

Muktasari:

  • Tangu Zanzibar ilipochukuliwa kama mwanachama mshiriki wa Shirikisho la Soka Africa (CAF), imekuwa ikiwakilishwa na timu mbili, moja Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine Kombe la Shirikisho Afrika.

MARA nyingi nimeandika hapa, Tanzania ni nchi yenye nafasi kubwa au nyingi katika mashindano ya klabu za soka Afrika.

Tangu Zanzibar ilipochukuliwa kama mwanachama mshiriki wa Shirikisho la Soka Africa (CAF), imekuwa ikiwakilishwa na timu mbili, moja Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa upande wa Tanzania Bara ilikuwa ikiwakilishwa na timu  mbili kabla ya hivi karibuni kuongezwa hadi kufikia nne kutokana na pointi zilizokusanywa na mafanikio ya wawakilishi wa nchini katika michuano hiyo.

Kuongezwa kwa idadi ya timu kutoka mbili, kumeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 12 zenye takwimu za kufanya vizuri katika michuano hiyo ya CAF kwa ngazi za klabu.

Hata hivyo, alama nyingi zinazoibeba Tanzania kwa kiasi kikubwa zimetokana na Simba na Yanga, ilihali klabu nyingine sambamba na zile za Zanzibar zimekuwa zikikwamia njiani.

Kwa miaka ya hivi karibuni, Yanga na Simba zimekuwa zikipambana mno kuhakikisha zinakuwa na uhakika wa kutinga makundi kitu ambacho kwa Zanzibar na baadhi ya klabu wawakilishi imekuwa ngumu na mbali na vigogo hivyo ni Namungo pekee iliyowahi kutinga makundi Kombe la Shirikisho.

NIONA01

Mfano mdogo ni msimu huu, Azam iliyokuwa inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika iling’olewa na APR ya Rwanda katika raundi ya kwanza, huku Coastal Union iliyocheza Kombe la Shirikisho ilitolewa na Bravo ya Angola pia katika raundi ya kwanza. Waangola hao kwa sasa wapo kundi moja na Simba.

Kwa ufupi, matumaini ya Tanzania katika michuano hiyo ya Afrika bado yapo kwa Simba na Yanga na msimu huu zikiwa makundi zimeanza mechi zake kwa wastani usioridhisha, Yanga ikipoteza mechi mbili za kwanza dhidi ya Al Hilal ya Sudan na MC Alger ya Algeria wanaounda kundi A ya Ligi ya Mabingwa pamoja na TP Mazembe ya DR Congo.

Kwa upande wa Simba ilianza na ushindi wa 1-0 dhidi ya Bravos, lakini ikalala ilipokutana na CS Constantine ya Algeria, inayoongoza kundi A la Kombe la Shirikisho linaloijumuisha pia CS Sfaxien ya Tunisia.

NIONA02

Kifupi, Simba na Yanga zikiteleza, Tanzania nayo inayumba katika orodha ya nchi zinazopaswa kuendelea kuwa na klabu nne za kushiriki michuano hiyo miwili kila msimu. Yaani ni kama mayai yote yanakuwa kwenye vikapu viwili tu, yakiangushwa na kuvunjika ni hasara kwa mbebaji.

Pamoja na Ligi Kuu Bara kutajwa kuwa miongoni mwa ligi ya sita kwa ubora Afrika bado si nzuri ukilinganisha na mataifa ya Kaskazini kama Algeria, Tunisia, Morocco na Misri. Wenzetu kila anayewakilisha nchi kweli anaonekana anastahili.

Msimu huu ukiwa katika raundi ya pili ya makundi matumaini ya Tanzania kupitia Yanga na Simba yako mguu ndani, mguu nje. Kifupi, timu hizo zipo mtegoni katika kuhakikisha zinapata matokeo mazuri kwa mechi zilizosalia kama kweli zinataka kusonga mbele kufika robo fainali kama ilivyokuwa msimu uliopita.

NIONA03

Vipigo ilivyopata Yanga mbele ya Al Hilal na MC Alger zimeiacha timu hiyo ikiwa haina pointi wala bao lolote, huku Simba ikiwa na pointi tatu na mabao mawili, kabla ya wikiendi hii kurudi tena uwanjani kuvaana na TP Mazembe na CS Sfaxien.

Yanga iliyopo mkiani, kesho Jumamosi inatarajiwa kutia mguu kwenye uwanja wa Mazembe jijini Lubumbashi, DR Congo kuvaana na TP Mazembe inayomiliki pointi moja iliyotokana na suluhu dhidi ya MC Alger na kufumuliwa 2-1 na Al Hilal inayoongoza kundi A kwa sasa.

Mchezo huo ndiyo utakaotoa dira kama Tanzania itakuwa na nafasi ya kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa au la, kwani vipigo vya mechi mbili vimeiangusha licha ya heshima iliyopewa Yanga kutokana na kivuli cha kucheza fainali ya CAf na kutinga robo fainali msimu uliopita na kutolewa kwa penalti.

NIONA04

Yanga kwa msimu huu ilianza vizuri kwa kuziondosha Vital’O ya Burundi kwa mabao 10-0, kisha kuifumua CBE ya Ethiopia kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-0, lakini katika hali isiyo ya kawaida timu hiyo iliamua kumfurusha kocha Miguel Gamondi wiki moja kabla ya kuanza mechi hizo za makundi kisha kumpa kibarua kocha wa Sead Ramovic aliyetokea TS Galaxy ya Afrika Kusini.

Hatua hiyi ilitokana na mwenendo usiovutia wa timu hiyo katika Ligi Kuu Bara kwa kufungwa mechi mbili mfululizo dhidi ya Azam FC na Tabora United.

Mabadiliko hayo ya ghafla yanaweza kwa kiasi kikubwa kuchangia mdororo wa timu hiyo katika michezo hiyo ya makundi, kwani wachezaji bado hawajaanza kuzishika falsafa za Mjerumani huyo kwa sasa baada ya Muargentina, Gamondi kutimuliwa klabuni.

NIONA05

Ikiwa kuna mchezo wa ‘kufia’ uwanjani kwa ajili ya mashabiki na timu yao basi ni mchezo wa kesho dhidi ya TP  Mazembe. Sifichi kitu, sioni Yanga ikifanya iliyoyafanya msimu uliopita kama itakwaa kizingiti mbele ya Mazembe.

Kwa upande wa Simba yenyewe Jumapili itakuwa tena Kwa Mkapa kuikaribisha CS Sfaxien ya Tunisia katika mchezo muhimu kwa Wekundu hao wa Msimbazi wenye pointi tatu katika kundi linaloonekana kuwa gumu.

Mwanzo mzuri wa kuifunga Bravos ulishindwa kuendelezwa mbele ya CS Constantine baada ya kupigwa mabao 2-1, ila jambo linalotia moyo katika mechi hiyo ya Algeria ni mpira ‘mkubwa’ iliocheza Simba hasa katika kipindi cha kwanza na kuifanya iende mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Simba ina uzoefu wa kushinda michezo ya nyumbani na mara nyingi imeonyesha hilo inapocheza mbele ya mashabiki kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

NIONA06
NIONA06

Kwa namna yoyote ile Simba inahitaji ushindi katika michezo ya Dar es Salaam kwani rekodi yake ya ugenini imekuwa siyo nzuri.

Pamoja na kuwa na kikosi kipya ikiwa ni pamoja na kocha mpya Fadlu David kutoka Afrika ya Kusini, Simba wanaonekana kuelewana na wanaweza kuongeza kiwango kadri mashindano yanavyoendelea.

Yote kwa yote kupoteza mchezo katika hatua hii ya makundi ni jambo hasi hasa unapokuwa na wapinzani kama CS Constantine na CS Sfaxien ambao ni mabingwa wa kihistoria wa Kombe la Shirikisho na wamelitwaa mara tatu.

Wikendi hii itakuwa na maamuzi ya mwelekeo wa klabu za Yanga na Simba, kwani ndio takayotoa mwelekeo wa Tanzania katika mashindano hayo ya klabu za Afrika kwa msimu huu wa 2024/25.


Mwandishi wa makala haya ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake iliyopo hapo juu.