NIONAVYO: Ni kweli wachezaji wetu wanapiga misosi sahihi?

ILI wanamichezo waweze kufanya vizuri, bila kujali ni michezo ipi, wanawake kwa wanaume, vijana kwa watu wazima, wote wanahitaji lishe ya kutosha na yenye ubora unaotakiwa kuendana na mahitaji ya miili yao na pia aina ya michezo wanayocheza.

Mara chache sana,hasa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki kusikia klabu cha michezo kikitafuta mtaalmu wa lishe. Na kwa wanamichezo wasio wa kulipwa ambao kila mtu hula chakula cha aina yake kutegemea baba na mama wameweka nini mezani hali huwa mbaya zaidi. Chakula hutolewa bila kujali majukumu ya mwanamichezo kwa siku husika na pia bila kujali aina ya mchezo anaocheza kama ni mpira wa kikapu, mbio au soka.

Haishangazi, mara nyingi kusikia tukilalama kwamba mchezaji fulani kipaji chake kimepotea au mchezaji fulani kiwango chake kimeshuka ghafla.Kumbe yawezekana kuna utapia mlo (Kukosa lishe muhimu) kumechangia sana udumavu huo.Bahati mbaya sana tamaduni zetu zimetufundisha kwamba kula ni kujaza tumbo bila kujali ni nini kinajaza tumbo.Hatukawii kutafuta kila aina ya lawama ikiwemo kupigwa misumari (kurogwa) kama chimbuko la kutofanya vema kwa wanamichezo wetu.

Kadri michezo inavyozidi kuendeshwa kitaalam zaidi,utendaji wa mwili wa mwanamichezo unaangaliwa zaidi pia.Wanamichezo wanaweza kuwa wanafanya kazi zinazofanana uwanjani lakini mahitaji yao ya chakula ni tofauti.Mathalani mchezaji mwenye umri wa miaka 18 ana uwezo wa kucheza kila siku bila matatizo lakini hali si hivyo kwa mchezaji mwenye miaka zaidi ya 30.Kwa wanamichezo wenye umri mkubwa inachukua muda mwili kurudi kwenye utimamu wake baada ya shughuli nzito kama mechi au mbio nahivyo basi wanahitaji kuangaliwa zaidi katika mlo wanaopewa.

Vilevile,wanamichezo wanaokua wanahitaji aina ya kipekee yam lo ili miili yao iweze kukua na kuwa tayari kwa kazi ngumu wakati unapofika.Alipowasili katika Klabu ya Barcelona inasemekana  Lionel Messi aliwekewa mtalamu maalum wa kuangalia lishe na vichochezi vya mwili ili kumuwezesha kukua kwani pamoja na kipaji alichoonyesha katika umri mdogo bado alikuwa na dalili zote za udumavu wa mwili .

Kocha Jurgen Klopp wa Liverpool alionajiko kama kipaumbele chake mara baada ya kuanza kandarasi yake katika klabu hiyo.Alihakikisha jiko kwenye kituo cha mazoezi cha klabu lina kila aina ya vifaa kuwezesha wachezaji kupata huduma ya uhakika ya wataalam wa lishe.Matokeo ya juhudi zake hayakukawia kuzaa matunda kwani wachezaji wake walikuwa timamu pamoja na kushiriki mashindano mengi.Mtazamo huo alikuwa nao kocha Arsene Wenger alipowasili kwenye klabu ya Arsenal mwaka 1996.Wenger alikuta wachezaji wakiishi maisha wanayopenda wao.Wachezaji walitumia muda wa baada ya mechi za wikendi kwenda klabu kunywa bia,kuvuta sigara na kula chakula chochote kilichokuwa mbele yao.

Chini ya Wenger,wachezaji wakaanza kula mlo ulioandaliwa na wataalam,wakapunguza mafuta katika chakula chao na kuongeza unywaji wa maji na juisi ya machungwa.Ndani yam waka mmoja timu ilibadilika kwa wachezaji kuwa wepesi na majeraha au muda wa kuuguza majeraha kupungua.

Katika uzoefu wangu na mpira wa klabu za hapa kwetu au hata timu za taifa,suala la lishe halijawahi kuwa kipa umbele.sitaki kumaanisha kuwa vilabu na timu za taifa hawakujali chakula kwa wachezaji,asha,walijali chakula lakini suala la lishe halikuwa kitu cha mbele.Sijui hali ikoje sasa lakini kwa ujumla naweza kubashiri kwamba ni klabu chache,narudia,ni klabu chache,kama zipo,zinazoajiri wataalam wa lishe kwa ajili ya timu zao.
Natolea mifano zaidi ya mpira wa miguu ambao ndio unahusisha watu wengi katika Afrika Mashariki lakini pia uzoefu wangu mkubwa na ukaribu na wachezaji wa soka.

Wachezaji wetu pia,walio wengi hawajui ni aina gani ya chakula kinafaa mwilini mwao na wakati gani.wengi hawajui wale nini kabla ya mchezo au baada ya mchezo.sasa hapo ndipo mtaalam wa lishe anapotakiwa ili kumwelekeza mchezaji nini cha kufanya.Jambo hili ni muhimu pia kwa makocha wetu,kama nilivotoa mifano ya makocha Arsene Wenger na Jurgen Klopp katika klabu za Arsenal na Liverpool mtawalia,utagundua kwamba uelewa wa kocha katika suala la lishe ni muhimu katika kuwabadilisha wachezaji.Angalia miili ya makocha wenyewe ilivyo,utagundua wao pia walikuwa mfano kwa wachezaji.

Haina maana kabisa kama klabu itaajiri mtaalam wa lishe halafu kocha wa timu akawa haelewi au haoni umuhimu wa suala hilo.Hivyo ni muhimu kwa makocha wetu pia kujua elimu ya lishe ili waweze kuishi kama mfano kwa wachezaji.

Michezo ni ajira katika ulimwengu wa sasa.Taifa lina vijana wengi wanaotoka vyuoni na shahada za masuala ya lishe.Ni muhimu sasa kwa serikali shirikisho na vilabu kuanza kuwavutia na kuwapa mafunzo na ajira ili wachangie katika maendeleo ya michezo huku wakipunguza wimbi la wasomi wasio na ajira.
Ikiwa kweli tumeamua kuingia kwenye barabara ya maendeleo ya michezo ni lazima tuiangalie michezo kama kitu kizima.Hatuwezi kuendelea vipande vipande.

Ni muhimu kuhakikisha tunaelimisha na kuajiri wataalam wa viungo,wataalam wa saikolojia,wataalam wa viwanja n.k. Michezo sasa inachezwa kwanza kichwani kabla ya kuchezwa viwanjani hivyo tofauti kidogo ya utaalam (kama wa lishe)yaweza kurudisha mipango yote ya maendeleo nyuma.

Nionavyo mimi,kama msisitizo utawekwa katika suala la lishe na utaalam wake,tunaweza kupata moja ya vitu vinavyotubakiza nyuma ya wengine katika maendeleo ya michezo.
Mwandishi wa makala hii amewahi kuwa katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)