Nionavyo: Mkataba wa mchezaji ni kama mpira tu

WAPENDWA wasomaji, juma lililopita katika safu yenu hii mnayoipenda tulizungumzia juu ya umuhimu wa mchezaji kuwa na menejimenti inayoelewa vizuri ibara ya 17 ya kanuni za FIFA zihusuzo uhamisho wa wachezaji wa kulipwa.
Uzoefu unaonyesha kwamba wakati wa kuingia mkataba pande zote huwa zina matumaini makubwa katika kile kitakachopatikana ndani ya mkataba. Inapokuja wakati wa utekelezaji au hata usitishwaji wa mkataba ndipo ningalijua huja.
Majuzi nilihudhuria shughuli iliyoandaliwa na wanasoka wastaafu wengi wakiwa wanaoishi jijini Dar es Salaam. Wengi niliobahatika kuongea nao nilitamani kujua kwa sasa wanafanya shughuli gani.Wengi waliniambia wanasotea beji za ukocha yaani kuwa walimu wa soka. Baadhi walilalamika kuhusu kupanda kwa gharama za kusomea ukocha wakati wengine wakilalamikia ukiritimba kwa waajiri wao kuwalipia au hata kuwaruhusu kupata muda wa kufanya kozi hizo za A,B au C za CAF.
Mmoja aliniambia jambo lililonifikirisha sana; alisema kama angalijua wakati anasaini mkataba wake wa mwisho kama mchezaji wa kulipwa, angeweka kipengele cha mwajiri kumpa nafasi ya kufanya kozi za ukocha na hivyo angestaafu kucheza akiwa labda na leseni B na yawezekana angepata muda wa kufundisha kwenye vikosi vya chini vya klabu yake. Nilisikitika lakini nikamwambia huo ndio ushauri wa kuwapa vijana wetu ambao bado wanatumika.Mara chache sana kusikia mwanamichezo wetu analalamikia maslahi nje ya fedha na gari.
Vijana wetu wamekariri hayo,apewe fedha na gari basi ametimiza ndoto zake. Laiti wangelijua kuwa muda wa kuwa mchezaji wa kulipwa ni miaka 8-10 au kuzidisha kidogo kwa wenye bahati wachache kama Juma Kaseja, Messi na Ronaldo.
Kwa bahati mbaya wanamichezo wengi, hata mawakala na maofisa wa vilabu hasa katika nchi zetu za kiafrika hudhani ya kuwa mikataba hufanana.Ni kawaida hata kwetu Tanzania kusikia watu wakisema mkataba kamili ni ule wa shirikisho la TFF.
Ni kweli,shirikisho la mpira hutoa mfano wa namna mkataba unavyotakiwa kuwa kwa kueleza kuwa ni muhimu au lazima vipengele Fulani viwemo katika mkataba.Mfano mkataba lazima huonyeshe muda wa ukomo, mshahara na marupurupu mengine.
Hata hivyo ni juu ya pande zinazoingia mkataba kuwasilisha maslahi yao mezani wakati wa kuingia mkataba.Kama nilivyosema katika safu hii juma lililopita, mkataba wa mwanamichezo unaweza kuwa na vipengele vingi hata vya kipuuzi ili mradi havivunji sharia ya mpira na sharia ya nchi.Si ajabu kuona mwanamichezo analalamika kuhusu maslahi ya mwenzake kwenye timu moja kuwa bora kuliko yake wakati wanatumikia timu moja.
Lisilojulikana ni jinsi kila mtu alivyoweka karata za maslahi yake wakati wa kuzungumza mkataba.Kama jinsi mpira unavyokwenda kutegemea nguvu na sehemu gani ya mwili imeupiga na mkataba vivyo hivyo hutegemea namna ulivyowekewa vipengele vya mslahi ya mchezaji au ya mwajiri.
Tatizo la kuelewa vifungu na maslahi yaliyojificha haliko kwa wachezaji bali pia hata kwa wanasheria wasomi wanaowakilisha wanamichezo. Katika uzoefu wangu wa utawala wa mpira hapa Tanzania nimeshuhudi wanasheria wengi wasomi wakipata wakati mgumu kuwakilisha vema wateja wao katika sekta ya michezo. Sina hakika sasa hali ikoje lakini kwa siku za nyuma waliokuwa na jicho la ziada ni kama mawakili maarufu wakati ule Damas Ndumbaro, Rutashobya na James Bwana.
Ni vizuri kwa klabu, mwanamichezo au hata wasimamizi wake kujitahidi kupata uzoefu wa mikataba ya wanamichezo wengine wa hapa nchini au nje ya nchi kama imeonekana kubeba vizuri maslahi ya upande husika.
Kuna mikataba imewahi kugonga vichwa vya habari kama ya ajabu lakini inaweza kutumika kuwasaidia wanamichezo, wawakilishi wao na hata taasisi kama shirikisho na vilabu kujua namna ya kulinda maslahi kwenye mkataba. Hapa chini ni baadhi ya mikataba ya kushangaza ya wanamichezo:
Neymar na wageni
Mwaka 2013 mchezaji kutoka Brazil Neymar alijiunga na klabu ya Barcelona ya Hispania. Katika mkataba wake kiliwekwa kifungu kinachomruhusu kutembelewa na wageni kila baada ya wiki mbili. Klabu yake ya Barcelona ililipia gharama za ugeni huo bila kinyongo kwani ni kifungu cha mkataba ilichoridhia.
Denis Bergamp asiyepanda mwewe
Klabu ya Arsenal ilimsajili mchezaji wa Kiholanzi Denis Bergamp ambaye alikuwa na woga wa kupanda ndege. Klabu ililazimika kumtanguliza kwa taxi kila mara ilipoenda kucheza sehemu mbalimbali Ulaya. Hilo halikuwasumbua Arsenal kwani waliridhia wakati wa kusaini mkataba.
Samuel Eto’o na ndege binafsi
Kuelekea mwisho wa uwezo wake kama mchezaji wa kulipwa, mchezaji kutoka Cameroon Samuel Eto’o alipata kandarasi katika klabu ya Anzhi Makhachkala. Kwa vile alipachukulia Makhachkala kama kijijini, Eto’o alihakikisha kuna kifungu cha kukodishiwa ndege binafsi kila mara alipotaka kwenda jijini Moscow ambako ndiko alitumia muda mwingi. Klabu ilitekeleza kama ilivyoingia mkataba.
Tom Saintfiet na mchumba wake Cheryl
Mwaka 2012 klabu ya Young Africans (Yanga) ya Dar Es Salaam ilimpata kocha raia wa Ubelgiji aliyetwa Tom Saintfiet, kocha huyo aliyeipa Yanga Kombe la Kagame ndani ya wiki ya pili ofisini alitaka mkataba wake utamke bayana kuwa wakati wa likizo yake atapewa tiketi ya ndege ya kwenda na kurudi yeye na mchumba wake Cheryl ambaye alikuwa raia wa Zimbabwe. Kwa sababu klabu ilimhitaji kocha ililazimika kumlipia yeye na mchumba wake Cheryl ambaye sasa ni mke wake.
Ronaldinho na ruhusa ya ‘kula bata’
Aliporudi nyumbani akitokea Ulaya, nyota Ronaldinho Gaucho alijiunga na klabu ya Flamengo. Katika mkataba wake aliweka kifungu cha kumruhusu kwenda kwenye kumbi za starehe mara mbili kwa wiki.
Hili halikuwa tatizo kwa klabu ya Flamengo iliyoamini kuwa Gaucho atafanya vizuri uwanjani anapokuwa na furaha kwenye kumbi za starehe.
Mifano hiyo hapo juu inatuonyesha kuwa maslahi ya mchezaji au ya klabu yanalindwa zaidi wakati wa ‘kuchumbiana’. Ni machache sana mapya yanayoweza kuingizwa kwenye mkataba wakati wa utekelezaji. Utaratibu huu hutumika pia kulinda maslahi ya wadhamini wa mchezaji na wa klabu.
Bahati mbaya sana kwetu Watanzania, maumivu yetu tangu enzi za Karl Peters hutokana na kuingia mkataba bila kujua kilichomo na madhara yake huku tukiishia kulaani kulaghaiwa au kupunjwa wakati wa utekelezaji.
Ni wakati sasa kwa wanamichezo wetu na wadau wote kuwa waangalifu katika namna wanavyoendesha mambo yao ikiwa tunataka kuleta maendeleo na kupata faida toka kwenye vipaji na uwekezaji katika michezo.