Ni rekodi ya ubabe tu Yanga

Saturday August 06 2022
Yanga2 PIC
By Ramadhan Elias

YANGA ikiendelea na shamrashamra za tamasha lao la kilele cha Wiki ya Mwananchi leo, makocha, uongozi na wachezaji wote wameweka wazi matarajio yao kwa msimu huu ni kuvunja rekodi mbalimbali na kuendelezea ubabe wake kwenye michuano ya ndani na Afrika kiujumla.

Msimu uliopita Yanga ilirejea kwenye ubora wake wa kutwaa kombe la Ligi Kuu baada ya kulikosa kwa misimu minne mfululizo nyuma likienda kwa watani wao wa jadi Simba na sasa Wanajangwani wanataka kuendelea walipoishia.

Sio tu kwenyeubingwa wa Ligi, uongozi wa Yanga msimu huu pamoja na kikosi na benchi la ufundi wamejipanga kuchukua kila kombe litakalokatiza mbele yao kwa mashindano ya ndani na kufika mbali katika michuano ya kimataifa.

Ili kuhakikisha hilo linatokea, timu hiyo imejiimarisha kwa kuhakikisha inawabakiza kikosini mastaa wake wote iliowahitaji na kushusha majembe mengine mapya kwaajili ya kuliongezea nguvu chama hilo linaloongozwa na kocha Mtunisia Nassredine Nabi.

Katika usajili wa msimu huu, Yanga imevunja benki kwa kusaini mastaa wenye ubora na wasifu mkubwa kwa pesa ndefu ambapo ilizama England na kumchukua kiungo wa zamani wa Newcastle United, Mrundi Gael Bigirimana.

Haikuishia hapo imemshusha beki wa timu ya taifa ya Congo DR, Joyce Lomalisa na kwenda ndani ya Afrika Kusini kutoka Kaizer Chiefs na kumchomoa straika Mzambia Lazarous Kambole kisha kurudi Bongo kwa watani wao Simba na kuwapiga na kitu kizito kwa kumchukua nyota mtukutu Mghana Bernard Morrison na kummrudisha Jangwani.

Advertisement

Pia imenasa saini ya kiungo mshambuliaji kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo, Mburkina Faso, Aziz Ki kutokea Asec Mimosac ya Ivory Coast ikifunga usajili kibabe.


MSIKIE NABI

Nabi baada ya kukabidhiwa majembe hayo mapya kikosini aliweka wazi licha ya kwamba ligi ya msimu huu itakuwa ngumu lakini amejipanga kuendeleza alipoishia na kuifanya timu inakuwa imara na tishio zaidi uwanjani.

Nabi ameeleza shauku yake ya kuendelea kufanya vizuri ikiwemo kushinda kila mechi iliyo mbele yake na kwenda mbali kimataifa jambo analoamini linawezekana kutokana na ubora wa kikosi chake.

“Msimu huu tunataka kuendelea tulipoishia, tumeongeza wachezaji wazoefu katika soka la Afrika hivyo tunataka kufanya vizuri kote kote ndani na nje.

Msimu uliopita ulikuwa mgumu lakini tuliweza kumaliza ligi bila kupoteza mchezo, nadhani msimu ujao utakuwa mgumu zaidi lakini tumejipanga vyema kuhakikisha tunafanya vizuri kuliko msimu ule,” alisema Nabi aliyeibuka kocha mkuu wa Ligi Kuu msimu uliopita na kuongeza;

“Kila mchezaji anajua malengo ya timu hivyo kwa kushirikiana pamoja na benchi la ufundi naamini tutakuwa na timu imara kuliko ile ya msimu uliopita.”

Kati ya rekodi zinazosubiriwa kuvunjwa na skwadi la Nabi ni ile ya Azam FC iliyoiweka kuanzia msimu wa 2012/2013 hadi 2014/2015 ya kucheza jumla ya mechi 38 za Ligi Kuu bila kupoteza mchezo na hadi sasa Yanga imecheza michezo 37 bila kupoteza mchezo hivyo kama haitafungwa katika mechi mbili za kwanza za Ligi dhidi ya Polisi Tanzania na Coastal Union zote za ugenini, itakiwa imeivunja rasmi.


MASTA WATAMBA

Sambamba na Nabi kutamba kuwa na kikosi imara, mastaa wa timu hiyo wametamba kuwa bora zaidi ya wale wa timu nyingine ikiwemo wapinzani wao wa karibu Simba na kuapa kupambana kuhakikisha wanatisha ndani na Afrika kwaujumla.

Morrison ni miongoni mwa mastaa waliotamba huku akijinasibu kurudi nyumbani kukiwasha zaidi.

“Nimerudi nyumbani, msimu huu tutakuwa imara zaidi ya kipindi kile nilipoondoka hivyo mashabiki wetu wasiwaze kwani hakuna wa kutusimamisha,” anasema Morrison.

Mfungaji bora wa Yanga msimu uliopita Fiston Mayele amewatoa shaka mashabiki wa timu hiyo na kuwaahidi kuendelea kutetema.

“Wasisikilize maneno ya watu, mimi bado nipo Yanga na msimu huu wajipange kuendelea kutetema,” anasema Mayele.

Nahodha wa timu hiyo, Bakari Mwamnyeto anasema amefurahishwa na usajili uliofanya na unaenda kuongeza ubora na ushindani ndani ya Yanga.

“Usajili umefanyika vizuri na wachezaji wapya wanakuja kuongeza kitu na kwa pamoja tupo tayari kuwatumikia Wananchi.”


VIONGOZI WANASEMAJE?

Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said ameeleza kuwa makubwa aliyoyafanya miaka ya nyuma ilikuwa ni kama trela tu la muvi na sasa anaenda kuifanya timu hiyo kuogopwa Afrika nzima.

“Hadi sasa Yanga ndiyo timu kubwa Tanzania, tunataka kwenda kushindana na mabingwa wenzetu wa Afrika nzima. Ili kukamiliasha hilo tumeandaa mipango mikubwa kushirikiana na wadhamini wetu na msimu huu tutakuwa bora zaidi ya msimu uliopita,” anasema Hersi.

Kwa upande wa Makamu wa Rais wa timu hiyo, Arafat Haji anasema; “Msimu huu Yanga Princess isipochukuwa ubingwa niulizwe mimi. Nitasimama kidete kuhakikisha heshima iliyonayo timu kubwa inaenda hivyo hivyo kwa timu zetu zote za vijana sambamba na wanawake,” anasema Haji.

Yanga ndio mabingwa mara nyingi zaidi wa Tanzania wakibeba mataji 28 na msimu huu itashiriki kwenye ligi za ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Advertisement