NI HUZUNI: Vifo vilivyoshtua dunia mwaka 2025
Muktasari:
- Baadhi ya vifo hivyo, vilisababishwa na ajali, maradhi na vurugu, lakini vyote viliacha huzuni katika mioyo ya mashabiki wa michezo na burudani kwa ujumla.
MWAKA 2025 ni miongoni mwa miaka iliyobeba huzuni na mshtuko mkubwa kwa mashabiki wa michezo na burudani duniani. Huu ni mwaka ambao umeshuhudiwa baadhi ya mtukio makubwa ya kuhuzunisha ikiwemo vifo vya wachezaji na wasanii wakongwe.
Baadhi ya vifo hivyo, vilisababishwa na ajali, maradhi na vurugu, lakini vyote viliacha huzuni katika mioyo ya mashabiki wa michezo na burudani kwa ujumla.
Hapa tumekukusanyia matukio matano ya huzuni kwa mwaka huu.
KIFO CHA DHARMENDA
Msanii huyu wa maigizo kutoka India, Dharmendra alipoteza maisha Jumapili, Novemba, 24, 2025, akiwa na umri wa miaka 89 nyumbani kwake Juhu, Mumbai, India.
Alikuwa amebakisha siku chache kabla ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa ya kutimiza umri wa miaka 90 ambayo ilikuwa ni Desemba 8.
Mwigizaji huyo alikuwa akipatiwa matibabu kwa muda mrefu kutokana na matatizo ya pumu na mapafu na bada ya matibabu ya muda mrefu hali yake ilibadilika na akapoteza maisha.
Mwanzoni mwa Novemba 2025, Dharmendra alipelekwa Breach Candy Hospital huko Mumbai ambako alitibiwa kabla ya kurudishwa nyumbani kwake ambako pia alikuwa chini ya uangalizi wa madaktari, hata hivyo hali yake ilizidi kuzorota na mwisho umauti ukamkuta.
Mazishi yake yalifanyika maeneo ya Pawan Hans Crematorium, Mumbai, huku familia na mamia ya waigizaji wakihudhuria.
Makongwe wa tasnia ya uigizaji wa India kama Amitabh Bachchan, Salman Khan na Aamir Khan nwalikuwepo kumuaga mkongwe huyo.
AJALI YA DIOGO JOTA
Staa huyu wa zamani wa Liverpool na timu ya taifa ya Ureno, Diogo Jota alifariki dunia pamoja na mdogo wake, Andre Silva katika ajali ya gari huko Hispania Julai, 03, 2025.
Ajali hiyo ilizua mshtuko mkubwa kwa wapenzi wa soka duniani, kwani Jota alikuwa mmoja wa washambuliaji bora wa kizazi chake na ilikuja ghafla.
Jota ambaye ameacha watoto watatu alikuwa safarini kurejea England kwa ajili ya kujiunga na Liverpool ili kuanza maandalizi ya msimu huu na alitumia usafiri wa gari baada ya daktari kumshauri kufanya hivyo kutokana na changamoto za matatizo ya kiafya aliyokuwa nayo.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa polisi, gari lao lilipata hitilafu ya tairi barabarani maeneo ya Cernadilla, mkoa wa Zamora na likatoka nje ya barabara na kuwaka moto papo hapo, hali iliyosababisha vifo vya mastaa hao wawili papo hapo, kabla ya huduma za msaada kufika. Ripoti hiyo inadai ajali ilitokea kati ya saa 06:30 hadi 06:40 usiku.
Polisi walisema ushahidi unaonyesha Jota alikuwa katika mwendo kasi kabla ya tairi kupasuka na gari kuacha barabara.
Jota ameacha mke aitwaye Rute Cardoso ambaye alikuwa amemuoa siku 10 kabla ya ajali hiyo.
Wasanii, wachezaji, timu na mashirika mbalimbali yalionyesha kuumizwa sana na vifo hivyo na wote walituma salamu za rambi rambi kwenda kwa familia yake.
Ibada ya mazishi yake pamoja na mdogo wake ilifanyika Julai, 05, 2025 katika kanisa la Igreja Matriz de Gondomar, na baadaye akazikwa kwenye makaburi ya karibu na kanisa hilo pamoja na ndugu yake.
FOREMAN
George Foreman, ambaye ni bingwa wa zamani wa ngumi za uzito wa juu na mshindi wa medali ya dhahabu ya Olimpiki, alifariki dunia Machi, 21, 2025 akiwa na umri wa miaka 76.
Familia yake ilitangaza kifo hicho kupitia ujumbe kwenye akaunti yake rasmi ya Instagram, wakisema kwamba alifariki kwa amani akiwa ameungana na wapendwa wake. Sababu maalum ya kifo chake haikuwekwa wazi, isipokuwa familia ilisisitiza alifariki dunia kwa amani.
"Mioyo yetu imehuzunika. Kwa masikitiko makubwa tunatangaza kuondoka kwa mpendwa wetu George Edward Foreman Sr., aliyefariki dunia kwa amani Machi, 21, 2025 akiwa amezungukwa na wapendwa wake,” ilisema taarifa ya familia.
Foreman alijulikana si tu kama bingwa wa dunia mara mbili, bali pia kama bingwa wa Olimpiki na mmoja wa wanamichezo waliowahi kutamba ulimwenguni. Baada ya kustaafu, aliendelea kufanya kazi mbalimbali za kusaidia jamii, kutumikia kanisa na kufanya biashara zake binafsi.
VURUGU ZA INDIA
Baada ya timu ya Kriketi ya Royal Challengers Bengaluru (RCB) kushinda ubingwa wao wa kwanza katika ligi ya Kriketi ya India (IPL) mwaka 2025, mashabiki wengi walikusanyika kusherehekea ushindi huo wa kihistoria nje ya Uwanja wa M. Chinnaswamy, Bengaluru, India.
Sherehe hii ilifadhiliwa na klabu pamoja na vyombo vya serikali kama tukio la umma kwa mashabiki na wadau wengine wa mchezo wa kriketi na zilifanyika Juni, 04, 2025 jioni.
Mamia na maelfu ya mashabiki walifika nje ya uwanja na maeneo ya karibu ili kupata nafasi ya kuwaona wachezaji pamoja na kushiriki sherehe za ushindi.
Iliripotiwa idadi ya watu iliyokusanywa ilikuwa kati ya 200,000 hadi 300,000, ikizidi uwezo wa eneo hilo, ambalo kwa kawaida lina uwezo wa kuchukua watu 35,000 tu.
Kwa sababu ya msongamano uliozidi kuwa mkubwa kutokana na idadi kubwa ya watu waliokuwa wanalazimisha kuingia ndani ya uwanja, milango iliharibiwa na watu wakaanza kuingia ndani hali iliyosababisha kukanyagana na jumla ya watu 11 waliripotiwa kufariki papo hapo huku wengine takriban 60 wakipata majeraha na kupelekwa hospitali lakini baadhi yao wanadaiwa kuwa walifariki huko.
UEFA ILILETA TAHARUKI UFARANSA
Mnamo Mei 31 hadi Juni, 01, 2025, PSG ilishinda Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League) kwa mara ya kwanza katika historia yake, ikiifunga Inter Milan mabao 5‑0 kwenye fainali iliyochezwa jijini Munich.
Kushinda taji hilo kulizua shauku kubwa kwa mashabiki wa klabu hiyo waliokuwepo jijini Munich na wale waliobaki Ufaransa.
Kesho yake mamia na maelfu ya mashabiki walikusanyika katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Paris, hususani Champs‑Élysees na karibu na uwanja wa Parc des Princes, kusherehekea ushindi huo mkubwa.
Baada ya usiku wa sherehe, baadhi ya maeneo hasa mitaa ya jiji yalibadilika, kulikuwa na wizi wa mali na mabasi kuchomwa moto.
Kikosi cha jeshi la polisi kiliingia kati ili kudhibiti idadi kubwa ya watu iliyokuwa mitaani waliokuwa wakifanya vurugu ikiwemo kuwasha moto vitu na kurusha fataki.
Watu wawili wanadaiwa aliuawa wakati sherehe zikiendelea.
Zaidi ya watu 192 walijeruhiwa, pia takribani watu 500 walikamatwa na polisi maeneo mbalimbali ya Ufaransa, hasa jijini Paris, ikiwa ni harakati za kudhibiti vurugu.
KIFO CHA HULK HOGAN
Hulk Hogan naye alifariki dunia Julai, 24, 2025 akiwa na umri wa 71 katika nyumba yake huko Clearwater, Florida, Marekani.
Hogan alifariki baada ya kuugua kwa muda maradhi kadhaa ikiwemo. Chanzo cha kifo chake kinatajwa kuwa ni mshtuko wa moyo, alioupata asubuhi ya siku hiyo alipokuwa akifanyishwa mazoezi ya viungo.
Aliwahishwa hospitali lakini ilishindikana kuokoa uhai wake.
Bingwa huyu wa zamani wa mieleka pia alikuwa na saratani ya damu pamoja na matatizo ya uti wa mgongo.
Mkongwe huyu aliyejulikana kwa jina lake la utani la “The Hulkster”, alikuwa mmoja wa wachezaji maarufu na wenye ushawishi mkubwa katika historia ya mchezo wa mieleka.
Alijenga umaarufu mkubwa katika miaka ya 1980 hadi 1990, alipotwaa mataji kadhaa ya WWE.
KUPIGWA RISASI KWA MCHEZAJI ECUADOR
Beki wa kushoto Mario Pineida, 33, alipigwa risasi na kuuawa mchana wa Desemba, 17, huko Guayaquil, Ecuador.
Mchezaji huyo ambaye kwa wakati huo alikuwa akiitumikia Barcelona Sporting Club ya Ecuador wakati anapigwa risasi alikuwa pamoja na mwenza wake, ambaye pia alifariki papo hapo, pamoja na mama yake aliyepata majeraha na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Shambulio hilo lilitokea katika kitongoji cha Samanes 4, mbele ya eneo la kibiashara na watu wawili waliokuwa kwenye pikipiki waliwafyatulia risasi kwa staa huyo na familia yake.
Polisi wa Ecuador waliizingira eneo la tukio na kuanza uchunguzi ili kuwatambua wahusika na kubaini chanzo cha uhalifu huo. Barcelona Sporting Club ilitoa taarifa rasmi kuthibitisha kifo cha mchezaji huyo baada ya shambulio hilo.
Klabu ya Fluminense, ambayo Pineida aliwahi kuichezea kwa mkopo mwaka 2022 na kushinda taji la Campeonato Carioca, nayo ilituma salamu zao za rambirambi kufuatia kifo cha mchezaji huyo.
Tukio hilo lilitokea saa 9:53 alasiri kwa saa za Guayaquil, wakati Pineida alipokuwa akifanya manunuzi katika duka la kuuza nyama.
Mashuhuda walisema wauaji walisogea dukani hapo, wakafyatua risasi na kutoweka eneo la tukio.
Mchumba wa mchezaji huyo Gisella Fernández, alifariki dunia papo hapo kutokana na majeraha aliyoyapata.
Mama yake Pineida alinusurika lakini alihitaji matibabu ya haraka hospitalini. Mamlaka zimethibitisha tukio hilo linachukuliwa kama shambulio lililopangwa.
Saa chache kabla ya mauaji hayo, rais wa Barcelona Sporting Club, Antonio Álvarez, alikuwa ametangaza mchezaji mmoja wa kikosi hicho alikuwa ameomba ulinzi maalumu kutokana na vitisho vya kuuawa alivyokuwa akipokea. Ingawa hakumtaja mchezaji huyo kwa jina wakati huo, ushahidi unaonyesha alikuwa akimzungumzia Pineida.
Juzi, ilitoka taarifa polisi inashikilia watu wawili wanaohusishwa kufanya tukio hilo.
KIFO CHA DENIS LAW
Gwiji huyu wa soka wa zamani wa timu ya taifa ya Scotland na Manchester United, alifariki dunia akiwa na umri wa 84, January 17, 2025 nyumbani kwake huko Aberdeen nchini Scotland.
Law alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu, akisumbuliwa na matatizo ya moyo na magonjwa mbalimbali.
Denis Law, aliyekuwa akijulikana kwa jina la utani “The King”, alikuwa mshambuliaji mahiri mwenye uwezo mkubwa. Alijiunga na Manchester United mwaka 1962 na kuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya klabu hiyo chini ya kocha maarufu Sir Matt Busby.
Katika kipindi chake Old Trafford, Law alifunga mabao 230 katika mashindano yote, akishinda mataji makubwa ikiwemo Ligi Kuu England na FA Cup. Mwaka 1964, alitwaa tuzo ya Ballon d’Or na kuwa mchezaji pekee wa Scotland kuwahi kushinda tuzo hiyo.