Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ngoma ngumu CAF, wakubwa wanabatuana kibabe

NGOMA Pict


ZIMEBAKI dakika 180 za michuano ya CAF sawa na mechi mbili kwa wawakilishi wetu wa Tanzania, Yanga, Simba, Azam na Singida Black Stars ili kuhitimisha hatua ya makundi msimu huu 2025-2026.


Mechi hizo mbili zilizobaki, zimebeba matumaini kwa wawakilishi watatu, Yanga inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Azam na Singida Black Stars zilizo katika Kombe la Shirikisho. Simba kwa upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika, imeumaliza mwendo.


Hesabu zilizopo hivi sasa ni kwamba, katika dakika hizo 180, Yanga ipo karibu zaidi kufuzu robo fainali kuliko wawakilishi wengine wa Tanzania kwani ikipata ushindi ugenini dhidi ya AS FAR Rabat, itakuwa imekamilisha mchongo wake bila ya kusubiri mechi ya mwisho nyumbani kukabiliana na JS Kabylie. Lakini hata ikitoka sare, bado itakuwa nafasi nzuri kutokana na rekodi yake ya mechi za nyumbani msimu huu kimataifa.

NGOM 01

MECHI YA KUIVUSHA YANGA

Wikiendi hii, Yanga itakuwa Morocco kucheza dhidi ya AS FAR Rabat, timu zote zina pointi tano, lakini Yanga ipo juu kutokana na kanuni za CAF zinazohusu timu zilizolingana pointi ambapo kitu cha kwanza kinachoangaliwa ni pointi zilizopatikana kwenye michezo waliyokutana kati ya timu zinazolingana, kitu ambacho kitaibeba Yanga kutokana na kushinda mechi ya kwanza nyumbani kwa bao 1-0.

Baada ya hapo, inaangaliwa tofauti ya mabao (goal difference) kwenye michezo waliyokutana timu zinazolingana. Kingine ni mabao yaliyofungwa kwenye michezo waliyokutana kati ya timu zinazolingana, huku mwisho ikiwa ni mabao ya ugenini yaliyofungwa kwenye michezo waliyokutana baina ya timu hizo.

Ukiangalia hayo yote, ikitokea wikiendi hii Yanga imepata sare dhidi ya AS FAR Rabat, kisha mechi za mwisho zote zikashinda, bado Yanga itakuwa juu yake.

Kwa sasa kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly inaongoza ikiwa na pointi nane, inafuatia Yanga (5), kisha AS FAR Rabat (5), huku JS Kabylie ikiburuza mkia ikikusanya pointi mbili.

Katika kundi hili, timu zote zina nafasi ya kufuzu robo fainali kulingana na pointi zilivyo, lakini JS Kabylie ina kazi kubwa ya kufanya ili kutoboa kwani mechi mbili zilizobaki dhidi ya Al Ahly (nyumbani) na Yanga (ugenini) ishinde zote, kisha iombe Yanga na AS FAR Rabat zisipate pointi tatu.

Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema: “Tuna kazi ya kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye mechi zetu mbili zijazo tukianza na FAR Rabat, tunatakiwa kwenda na akili ya ushindi hukohuko.

“Mchezo huo dhidi ya FAR Rabat ni sawa na kwamba tunakwenda kucheza fainali kuamua safari yetu ya kwenda hatua inayofuata, tukijua kwamba tukishinda tutafuzu.”

NGOM 02

Kundi B

                                P        Pts

1.Al Ahly                 4        8

2.Yanga                 4        5

3.AS FAR               4        5

4.JS Kabylie            4      2


RATIBA

Februari 6–8, 2026

JS Kabylie v Al Ahly

AS FAR v Yanga


Februari 13–15, 2026

Al Ahly v AS FAR

Yanga v JS Kabylie

NGOM 03

HESABU ZA SIMBA ZIMEFIA DAR

Sare ya mabao 2-2 iliyopata Simba juzi dhidi ya Esperance nyumbani, ndiyo imeondoa matumaini ya Simba kufuzu robo fainali kwa mara ya nane katika michuano ya CAF ndani ya misimu tisa kuanzia 2017-2018.

Matokeo hayo yameifanya Simba kukusanya pointi moja, ikiwa ni ya kwanza baada ya kucheza mechi nne ikiburuza mkia wa kundi D linaloongozwa na Stade Malien yenye pointi 8, huku Esperance ikifuatia na sita, kisha Petro Atletico (5).

Hesabu za Simba zimefia Dar kutokana na idadi ya mechi zilizobaki na pointi ilizokusanya kwani hata mechi ijayo ikifanikiwa kushinda ugenini dhidi ya Petro Atletico, itafikisha nne, kumbuka hapo tayari Stade Malien ina nane, hivyo Simba haiwezi kuzifikia kutokana na kwamba itabakiwa na mechi moja, ikishinda pia dhidi ya Stade Malien nyumbani, itakwamia saba.

Katika kundi hilo, kuna mchezo baina ya Esperance na Petro, timu zilizokaa kimtego hapo kati kuwania kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ndizo zilizoibania Simba.

Esperance yenye pointi sita, ikishinda mechi moja kati ya mbili, inafikisha tisa, Simba haiwezi kuzifikia.

Kwa upande wa Petro Atletico yenye pointi tano, ikishinda mechi moja kati ya mbili, inafikisha nane ambazo Simba haiwezi kuzifikia.

Mechi ya mwisho baina ya timu hizo ikimalizika kwa sare huku ikitokea mechi za wikiendi hii zimepoteza, itakuwa faida kwa Esperance itakayofikisha pointi saba ambazo Simba hata ikizifikia, itahukumiwa na kanuni ya walivyokutana (head to head) kwani ugenini Simba ilifungwa 1-0, nyumbani ikawa sare ya 2-2.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema: “Hatuna budi kusema kwamba msimu huu haukuwa mzuri kwetu, yale ambayo tumezoea kufanya kimataifa msimu huu Simba tumeshindwa kufanya. Ulikuwa msimu wenye presha kubwa, lakini ndiyo mpira wa miguu.

“Ukiangalia tumefanikiwa kucheza robo fainali mara saba lakini sasa hali imekuwa tofauti, hivyo kuna wakati lazima uanguke ili urejee kuwa bora zaidi.”

NGOM 04

Kundi D

                            P        Pts

1.Stade Malien        4        8

2.Espérance          4        6

3.Petro                  4       5

4.Simba                 4       1


RATIBA

Februari 6–8, 2026

Stade Malien v Espérance

Petro Atletico v Simba


Februari 13–15, 2026

Espérance v Petro

Simba v Malien

NGOM 05

VITA YA IBENGE NA NDUGU ZAKE

Kocha wa Azam, Florent Ibenge baada ya kuiongoza timu hiyo kupata ushindi wa pili mfululizo katika Kombe la Shirikisho Afrika mbele ya Nairobi United, kituo kinachofuata ni dhidi ya ndugu zake kutoka DR Congo, AS Maniema. Hapa Ibenge anakwenda kuzipambania pointi tatu dhidi ya ndugu zake ambapo kila mmoja anasaka nafasi ya kufuzu robo fainali.

Kwa namna kundi B la michuano hiyo lilivyo, Azam inatakiwa kupata ushindi utakaoiweka sehemu nzuri ikiwezekana nafasi ya pili kwani ikipata ushindi mzuri zaidi wa mabao 3-0, itaishusha AS Maniema.

Kwa sasa Azam ina pointi sita ikishika nafasi ya tatu, wakati AS Maniema inazo tisa ikikamata nafasi ya pili na vinara Wydad wana tisa pia.

Mechi ya kwanza, Azam ilifungwa 2-0 ilipoifuata AS Maniema, hivyo kutokana na kanuni zilivyo, Azam ili ikae juu ya Wakongomani hao, inatakiwa kushinda kwa tofauti ya mabao 3-0 wikiendi hii zitakapokutana kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, vinginevyo, hata ikishinda, bado itasalia nafasi ya tatu.

Wydad imebakisha hatua chache za kufuzu robo fainali, ikishinda mechi ijayo dhidi ya vibonde Nairobi United wanaoburuza mkia bila pointi, itakuwa imefuzu. Mechi hiyo itapigwa nchini Kenya.

Hata kama ikizikosa pointi tatu za mechi hiyo, itasaka moja pekee mbele ya Azam katika mechi ya mwisho itakayochezwa nchini Morocco ili ifuzu, hivyo Waarabu hao suala la kufuzu hatua inayofuata, limekaa vizuri.

NGOM 06

Kundi B

                             P        Pts

1.Wydad                 4        9

2.Maniema             4       9

3.Azam                  4        6

4.Nairobi Utd         4        0


RATIBA

Februari 8, 2026

Nairobi United v Wydad AC

Azam v Maniema Union


Februari 15, 2026

Wydad AC v Azam

Maniema v Nairobi United

NGOM 07

HAPA HAKUNA MWENYEWE

Singida Black Stars yenye pointi nne ikiburuza mkia, ikichanga vizuri karata zake inatoboa, inachotakiwa ni kushinda mechi ijayo wikiendi hii nyumbani dhidi ya vinara wa kundi C la Kombe la Shirikisho Afrika, CR Belouizdad iliyokusanya pointi tisa.

Mechi nyingine itazikutanisha AS Otoho yenye pointi sita ikishika nafasi ya pili itakapokuwa nyumbani kucheza dhidi ya Stellenbosch iliyokusanya pointi nne ikikamata nafasi ya tatu. Kitendo cha CR Belouizdad kuichapa Stellenbosch nyumbani na ugenini, kimewabeba Waarabu hao kuongoza kundi, hivyo Singida ina kazi ya kufanya kwani mechi ya kwanza ilipokwenda Algeria, ilifungwa 2-0.

Singida Black Stars ikiuvuka mtihani huu, inapaswa pia kuichapa Stellenbosch mechi ya mwisho ili imalize kundi na pointi kumi zinazoweza kuivusha endapo AS Otoho na Stellenbosch zikipoteza angalau mechi moja tu kati ya mbili zilizobaki.

NGOM 08

Kundi C

                                 P       Pts

1.Belouizdad           4       9

2.AS Otoho             4       6

3.Stellenbosch       4        4

4.Singida BS           4       4


RATIBA

Februari 8, 2026

Singida BS   v CR Belouizdad

AS Otohô     v Stellenbosch


Februari 15, 2026

CR Belouizdad        v AS Otohô

Stellenbosch          v Singida BS



TIMU ZINAVYOPANGWA KUNDINI

Timu hupangwa kulingana na pointi (pointi 3 kwa ushindi, pointi 1 kwa sare, pointi 0 kwa kipigo). Endapo timu zitafungana kwa pointi, vigezo vifuatavyo hutumika kwa mpangilio huu (Kanuni III. 20 & 21):

(i) Pointi zilizopatikana kwenye michezo waliyokutana kati ya timu zinazolingana;

(ii) Tofauti ya mabao (goal difference) kwenye michezo waliyokutana kati ya timu zinazolingana;

(iii) Mabao yaliyofungwa kwenye michezo waliyokutana kati ya timu zinazolingana;

(iv) Mabao ya ugenini yaliyofungwa kwenye michezo waliyokutana kati ya timu zinazolingana;

(v) Endapo timu zaidi ya mbili zimelingana, na baada ya kutumia vigezo vyote vya ana kwa ana bado kuna timu zinaendelea kulingana, vigezo vyote vya timu zilizokutana vilivyo juu vitatumika tena mahsusi kwa kundi hilo dogo la timu zinazolingana;

(vi), Tofauti ya mabao katika michezo yote ya kundi; (vii) Mabao yaliyofungwa katika michezo yote ya kundi; (viii) Mabao ya ugenini yaliyofungwa katika michezo yote ya kundi; (ix) Kupigwa kura (drawing of lots).