Prime
‘Half time’ Simba ya Mo, ‘second half’ Simba ya Mangungu
NILIKUWEPO uwanjani jana wakati kipindi cha kwanza kilipokwenda kuwa zawadi kwa tajiri Mohamed Dewji. Halafu ghafla kipindi cha pili kikaenda kuwa mateso kwa Mwenyekiti wa timu, Murtaza Mangungu. Aliondolewa uwanjani kwa vurugu. Polisi waliitetea roho yake.
Hadi kufikia mapumziko ilikuwa raha tupu. Simba walikuwa wanaongoza mabao 2-0. Raha iliyoje. Mabao mawili ya Shomari Kapombe na Yusuf Kagoma. Mabao mawili yaliyofungwa kwa vichwa katika mitindo tofauti.
Shomari alijikuta katika boksi kwenda kufanya kazi ambayo kwa muda mrefu imewashinda kina Jonathan Sowah na Suleiman Mwalimu. Kagoma alikuwa ameichupia krosi fupi katika lango hilo la kaskazini kama mkizi vile.
Wakati wa mapumziko katika korido za Uwanja wa Mkapa mazungumzo ya mashabiki hayakumhusu Murtaza Mangungu. Yalihusu Esperance angekiona ‘cha mtema kuni’ katika kipindi cha pili. Kwamba mabao yangeongezeka na Simba walikuwa wanamfundisha mtani namna ya kumfunga Mwarabu katika ardhi ya Tanzania.
Kumbuka siku moja kabla, Yanga walikuwa wametoka sare na Al Ahly pale Unguja. Mpaka hapo jina la Mangungu halikuwepo katika mdomo wa mashabiki wa Simba ambao zaidi walikuwa wanadai walikuwa wanataka kupindua meza kibabe kwa kubeba pointi tisa za haraka haraka katika mechi hizi za marudiano.
Kitu walichokisahau ni ukweli, hadi wakati wanafunga mabao mawili, Esperance ndio walikuwa timu bora uwanjani. Umiliki wao wa mpira ulikuwa wa hali ya juu. Utulivu wao ulikuwa wa hali ya juu. Ilionekana kama vile walikuwa wamefungwa mabao ya ajabu ajabu kipindi cha kwanza.
Walirudi kipindi cha pili wakiwa na umiliki uleule wa mpira. Na ghafla na wao walizawadiwa bao la ajabu ajabu tu na Alassane Kante ambaye alirudisha pasi fupi iliyonaswa na mfungaji Aboubacar Diakite aliyemzunguka kipa na kufunga kwa utulivu.
Baadaye tena, fundi wa mpira, mgongoni jezi namba 7, Kouceila Boulia aliunasa mpira kando ya boksi la Simba, akampunguza mlinzi wa kwanza, akampunguza mlinzi wa pili, akafunga kwa ‘cave’ kama wanavyofanya kina Bukayo Saka, Mohamed Salah na Lionel Messi kule kwa wenzetu.
Uwanja ulikuwa kimya. Ungeweza kuangusha sindano na ukaisikia. Na baadaye kidogo Esperance walipata penalti. Kama sio Hamza Jlassi kuupeleka mpira jukwaani ule upande wa kusini basi Simba ingekuwa imefungwa mechi ya nne mfululizo katika kundi lao.
Na hapa ndipo jina la Mangungu lilipoanza kusikika tena. Na hapo ndipo Mangungu akakumbana na dhahama nje ya uwanja. Timu inapofungwa lawama huwa anapelekewa yeye. Timu inaposhinda wanasifika mafundi wa timu kama Libase Gueye alivyosifiwa wiki iliyopita kwa bao lake dhidi ya Mashujaa.
Shughuli ya Simba ikaishia hapo. kifupi ni Simba out. Amekwishatolewa. Ana mechi mbili mkononi tukianzia safari yake ya kwenda Luanda Angola kucheza na Petro de Luanda wikiendi ijayo. Safari ndefu ya kujichosha isiyo na maana tena kwa Simba.
Stade de Mallen tayari ana pointi nane ambazo Simba hawezi kuzifikia. Mechi ijayo atakwenda zake Tunisia kucheza na Esperance katika pambano ambalo Esperance akipata sare tu basi atakuwa amepita mbele ya Simba maana hata mechi za wenyewe kwa wenyewe kati yao na Simba zinawabeba Esperance.
Petro de Luanda yenye pointi tano inahitaji sare tu au ushindi dhidi ya Simba ili Simba isiweze kufikia pointi zake. Kuna vita kubwa kati ya timu tatu za kundi hilo kugawana nafasi mbili za juu lakini Simba haonekani kuhusika.
Kwa nini Simba imefika hapa? Ni matunda ya mambo mengi. Kwanza kabisa kuwa na kikosi kipya kila mara. Wakati mmoja wa mabosi wa Simba, Crescentius Magori alipowaahidi mashabiki katika siku ya Simba (Simba day) ya msimu huu ingekuwa ya moto, hakujua miezi michache ijayo ingekuwa na wachezaji wengine wengi wapya.
Simba bado haijatulia na bado haijatengeneza timu yao ya msingi. Watani zao wana timu yao msingi. Yanga huwa ni wajanja. Huwa wanachemsha katika baadhi ya sajili ambazo zimeshindwa moja kwa moja kuikamata timu kama tulivyoona kwa Mamadou Doumbia, Bala Conte, Andy Boyeli na wengineo.
Hata hivyo, wageni wakionekana kuwa na wakati mgumu, wao wanarudi kwa wachezaji wao ambao wamekaa kikosini kwa siku nyingi na wanaifahamu timu. Akina Pacome Zouzoua, Maxi Nzingeli, Dube Abuya, Mudathir Yahaya na wengineo.
Simba iliondokewa na msingi wake uliotawala soka. Hata Clatous Chota Chama ambaye alikuwa msingi wa timu akaondoka halafu amerejea tena jana alionekana kutokuwa katika makali yake. Maarifa yake hayakuendana na kasi yake ya mchezo. Alikuwa taratibu na alikuwa mkimya uwanjani.
Kwa sasa Simba ielekeze nguvu zake katika kujenga timu nyingine imara chini ya Steven Berker. Wakati mwingine usilazimishe mambo. Unahitaji kurudi nyuma na kutafakari. Hii siyo Simba bora kuwahi kutokea Msimbazi kiasi kwamba shabiki anaweza kujilaumu sana kwa kuambulia pointi moja katika mechi nne.
Sherehe zilikuwa kubwa kwamba Simba alikuwa amekaa katika kundi jepesi huku mtani wake akiwa na kundi la Waarabu watupu lakini ukweli umejionyesha, hali imekuwa tofauti. Uimara wa watani katika kundi la waarabu umewapa Yanga pointi tano katika mechi nne. Udhaifu wa Simba katika kundi jepesi umewapa Simba pointi moja katika mechi nne.
Mpira ni mchezo wa wazi. Kinachonekana kwa sasa Simba ina wachezaji wenye vipaji lakini bado hawajaunganishwa katika uthubutu wa kuwapa jeuri mashabiki na mabosi wao. Ni muda wa kujenga timu sasa. Hata mechi yao ya mwisho dhidi ya Stade Mallen nayo itumike kuwa sehemu ya kuchunguza vipaji vilivyopo Afrika Magharibi.