Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ngita: Kuna Prince Dube,Okello, Fei Toto na haya bara..!

Muktasari:

  • Ngita mwenye umri wa miaka 20 kutoka DR Congo, amefichua siri ya kuimarika ndani ya kikosi hicho akiwataja mastaa wawili wa Yanga, Prince Dube na Allan Okello kuwa wachezaji anaowaheshimu na kujifunza kutoka kwao.

WAKATI mastaa wengi wa kigeni wanaokuja Tanzania huhitaji muda mrefu kuzoea mazingira ya soka la ndani, mshambuliaji wa Azam FC, Jean Jacques Ngita ameanza kuonyesha dalili za kuwa mmoja wa washambuliaji wanaoweza kuacha alama kwenye Ligi Kuu Bara.

Ngita mwenye umri wa miaka 20 kutoka DR Congo, amefichua siri ya kuimarika ndani ya kikosi hicho akiwataja mastaa wawili wa Yanga, Prince Dube na Allan Okello kuwa wachezaji anaowaheshimu na kujifunza kutoka kwao.

Mshambuliaji huyo aliyetua Azam FC katika dirisha dogo la usajili akitokea Aris Limassol ya Cyprus, amekuwa na mwanzo wa kuvutia baada ya kupewa nafasi na kocha Florent Ibenge, na katika mechi za Ligi Kuu amecheza dakika 141 na kufunga mabao matano.

Mchezaji huyo alisajiliwa baada ya kuonyesha kiwango bora wakati wa Kombe la Mapinduzi 2026, ambapo benchi la ufundi liliona uwezo wake wa kupambana ndani ya boksi na kutumia nafasi. Uwezo huo ndiyo uliomfanya kuaminiwa na kupewa nafasi.


DUBE NI MFANO WA UTULIVU

Akizungumzia wachezaji wanaomvutia na ambao anajifunza kutoka kwao, Ngita hakusita kuwataja Dube na Okello ambao, kwa namna tofauti, wana majina na rekodi kubwa katika ligi msimu huu.

Kwa Ngita, ubora wa Prince Dube hauishii kwenye kufunga mabao pekee, bali namna ambavyo mshambuliaji huyo anavyoweza kubaki na utulivu wakati wote anapokuwa kwenye eneo la mwisho.

Anaamini uwezo wa kufanya maamuzi sahihi akiwa ndani ya boksi ni kitu kinachowatofautisha washambuliaji wakubwa na ndiyo jambo analojaribu kujifunza kutoka kwa Dube.

“Napenda sana anavyocheza mshambuliaji wa Azam zamani, Prince Dube. Aina yake ya uchezaji ni nzuri. Ni miongoni mwa wachezaji wanaojua kutulia eneo lao na kutumia nafasi. Kile anachokifanya Dube siyo kila mtu anaweza kuwa na utulivu wa akili na mwili kwa kiwango kile.”

OKELLO AMEMVUTIA NGITA

Mbali na Dube, Ngita pia anamtaja Allan Okello kama mmoja wa wachezaji wanaompa hamasa ya kuongeza kiwango chake.

Kwa mujibu wa mshambuliaji huyo, uwezo wa Okello wa kutafuta nafasi na kutumia vizuri mipira anayopata ni somo kubwa kwake akiwa bado anajenga jina kwenye soka la Tanzania.

“Kwa upande wa Okello ni kiungo hatari sana ambaye najifunza kutumia nafasi. Hawa wawili ni mastaa ambao najifunza vitu vingi kutoka kwao, licha ya kwamba ni wageni, ila wamefanikiwa kuteka soka la Tanzania kwa ubora wao.”


ALIVYOTUA AZAM

Ngita hakufika Chamazi kwa bahati, bali nyuma yake kulikuwa na mazungumzo na kocha Florent Ibenge ambaye aliona anaweza kuongeza kitu kwenye safu ya ushambuliaji.

Mshambuliaji huyo anasema baada ya kuvunja mkataba na klabu yake ya zamani, aliamua kuzungumza na Ibenge ambaye tayari alikuwa akimfuatilia.

“Mimi kabla ya kuja Azam nilizungumza kwanza na kocha Florent Ibenge. Alitaka nije hapa kwa sababu mkataba wangu katika timu niliyotoka tuliusitisha. Kwa hiyo, nilivyomalizana na wale nikampigia mwalimu.

“Nilifika Tanzania wakati Azam ikicheza michuano ya Kombe la Mapinduzi. Ndipo hapo niliingia kwenye kikosi moja kwa moja na mechi yangu ya kwanza ilikuwa nusu fainali dhidi ya Yanga.”


MAPOKEZI YA KUMPA UJASIRI

Licha ya kuwa mgeni na kuingia kwenye kikosi wakati wa mashindano makubwa, Ngita anasema mashabiki wa Azam walimfanya kujiamini mapema na kutokana na mapokezi hayo yalimfanya ajione sehemu ya timu muda mfupi baada ya kuwasili.

“Mashabiki walinipokea vizuri sana kama vile nilikuwa kwenye ligi muda mrefu. Ile mechi Yanga alitufunga kwenye hatua ya penalti. Tulitoka, lakini nilifurahi sana. Nilijiona mwanafamilia mapema mno.”

Kwa kuwa Azam ina wachezaji wengi wenye uwezo, Ngita anaeleza kuwa ushindani wa nafasi ni mkubwa na hakuna mchezaji anayeweza kujihakikishia kucheza bila kupambana.

Anasema kocha huangalia mwenendo wa mchezaji kuanzia mazoezini kabla ya kufanya maamuzi ya kikosi.

“Ushindani ni mkubwa sana. Kama kocha ataona unapambana ndani ya wiki nzima, basi atakupatia nafasi. Mwingine ataanza benchi na wiki inayofuata akiona uko chini, anaanza na mwingine.

“Kwa hiyo siyo uhakika sana kupata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza kila siku, kwa sababu kocha ana mambo yake ya muhimu ambayo anayazingatia kwenye kila mchezo kutokana na kiwango chako kuanzia mazoezini.”


KITAMBALA NI MWALIMU WA NGITA

Baada ya kuzungumzia wachezaji anaowaangalia kama mfano, Ngita pia amemtaja beki mwenzake Japhet Kitambala ambaye anasema wana historia ya kucheza pamoja kabla ya kukutana tena Azam.

Kwa mshambuliaji huyo, uwezo wa Kitambala kutuliza mpira na kufanya maamuzi akiwa nyuma ni kitu ambacho kinampa nafasi ya kujifunza zaidi kila siku akiwa mazoezini na uwanjani.

“Mimi Japhet nimecheza naye timu moja kabla ya hapa, kwa hiyo ni kama kaka kwangu na mara nyingi najifunza jinsi anavyocheza. Anajua sana kuutuliza mpira. Watu wote hapa kikosini wanajua hilo kwamba hakuna beki anayemsumbua.”

Licha ya kuanza vizuri ndani ya Azam, Ngita anakiri kuwa safari yake kwenye Ligi Kuu Tanzania haijawa rahisi kwa sababu amekutana na wapinzani wenye uwezo mkubwa hasa kwenye safu za ulinzi.

Anasema baadhi ya mechi zimemfundisha umuhimu wa kuwa makini na kutumia kila nafasi anayopata mbele ya lango.

“Mechi ngumu zaidi tangu nianze kuchezea Azam ni ile dhidi ya Mbeya City. Walikuwa na mabeki wasumbufu sana, lakini pia mechi ya Namungo na Pamba Jiji zilikuwa ngumu sana. Tulifunga dakika za mwisho.”


LIGI KUU BARA IMEMVUTIA

Baada ya kucheza soka nje ya nchi, Ngita anaona tofauti kubwa kati ya ligi mbalimbali alizowahi kukutana nazo.

Anasema moja ya vitu vinavyomvutia Tanzania ni namna ratiba na maandalizi ya mechi yanavyosimamiwa, jambo ambalo linampa mchezaji nafasi ya kujiandaa vizuri.

“Ligi ya huku ni nzuri. Kila kitu kiko kwenye ratiba. Kama kuna mabadiliko, basi mnaambiwa mapema. Kuna ligi zingine mpaka unafika uwanjani ndiyo mnaambiwa kwamba hakuna mechi wakati wewe umejiandaa kucheza. Kwa hiyo ni ligi nzuri Afrika.”

“Kule Ulaya wanafuatilia kila kitu kuanzia uwanja na mashabiki. Kuna wakati mvua ikiwa kali na mpira unadunda basi mnacheza, kama haudundi basi mchezo unasimamishwa mpaka itakapokatika.”

Kwa baadhi ya watu, Azam huonekana kama timu ambayo haina presha kubwa ikilinganishwa na Simba na Yanga, lakini Ngita anasema akiwa ndani ya klabu hiyo anaona tofauti.

Anaeleza kuwa presha ipo kutokana na malengo makubwa ambayo klabu imejiwekea, ila namna inavyowekwa ni tofauti na baadhi ya timu nyingine.

“Watu wengi wanaosema Azam haina presha ni wale wa nje, ila ukiwa ndani huwezi kusema hiyo kauli kwa sababu klabu ina malengo yake makubwa sana na mnatakiwa kuyatimiza, na wewe kama mchezaji unakuwa umejiwekea malengo ya kufunga mabao mangapi.

“Azam ni timu kubwa hapa Tanzania, haiwezi kukosa presha. Ila utofauti wetu na timu zingine ambazo unaona wanafokewa uwanjani, utaona tu kocha anaongea na sisi ila siyo kwa sauti kubwa.

“Utaona tu kocha anazungumza na wewe, kama hufuati unaona tu anakuweka nje. Kuna muda unakutana na mashabiki wanakwambia kwenye hiyo mechi mnayokwenda kucheza wanahitaji nini. Kwa hiyo presha kwetu ni matarajio makubwa, siyo kelele.”


IBENGE NI ZAIDI YA KOCHA

Ngita amempa sifa kocha wake, Florent Ibenge, ambaye anasema namna anavyowasimamia wachezaji wake inamfanya aonekane zaidi kama mzazi kuliko mwalimu wa kawaida.

Anasema Ibenge anajua namna ya kurekebisha makosa ya wachezaji bila kuwavunja moyo.

“Unajua kila mtu anajua kwamba hapa Azam tuna kocha mkubwa Afrika na yeye kwetu ni kama baba. Ukikosea haendi kwenye media kusema, ila atakuita na mtaongea na kusuluhisha kama mzazi.

“Kocha alizungumza na mimi kabla sijaanza kazi. Aliniambia ameniita Azam ili niongeze nguvu na nisaidiane na Kitambala tuweze kufanya jambo kubwa hasa kwenye eneo la mbele ambalo litasaidia kupata mabao mengi.”


FEI KAMPA PICHA YA MCHEZAJI BORA

Katika kipindi kifupi alichokaa Azam, Ngita anasema mmoja wa wachezaji ambao amekuwa karibu nao ni Feisal Salum.

Mbali na urafiki nje ya uwanja, anasema uwezo wa Fei akiwa na mpira ndiyo unaomfanya awe mmoja wa wachezaji wanaomvutia zaidi ndani ya kikosi.

“Hapa Azam mchezaji ambaye nilizoweana naye kwa haraka ni Feisal Salum. Huyo ndiyo mtu ambaye amezoeana na kila mtu hapa kikosini. Ni rafiki wa kila mtu, mcheshi na ana upendo sana.

“Lakini hata uwanjani ni mchezaji mzuri sana. Ni miongoni mwa wachezaji wazawa ambao wanaiwakilisha Tanzania vyema. Nadhani ni kiungo anayenivutia zaidi hapa Azam katika eneo hilo.”

MAISHA BONGO YAMEMKUBALI

Mbali na soka, Ngita anasema mazingira ya maisha Tanzania yamempa nafasi ya kuzoea haraka ukilinganisha na alikotoka.

Anaona tofauti hasa kwenye gharama za maisha na upatikanaji wa mahitaji ya kila siku.

“Hapa Tanzania maisha ni rahisi sana ukilinganisha na nilikotoka Kongo, vyakula na kila kitu. Kule kwetu vitu ni gharama. Sisi tunaona hivyo kwa sababu tumetumia pesa ya kule na huku ndiyo maana tunajua.”

Kwenye suala la chakula, Ngita anafichua kuwa bado hajabadilika sana na vyakula vya asili kwani ugali na maharage ndiyo vimeendelea kuwa sehemu ya mlo wake.

“Wali na ugali, maharage, kwa sababu watu wanalima mahindi kule kwetu. Licha ya kwamba huku wengi hawapendi ugali, lakini mimi ndiyo chakula changu pendwa, maharage yasikosekane. Nakula vitu vingine kama chipsi ila siyo sana.”

Mshambuliaji huyo pia anazungumzia suala la mkataba wake ambao ulikuwa wa muda mfupi ndani ya Azam, huku akiacha wazi uwezekano wa kuendelea kubaki Chamazi.

“Januari nilisaini mkataba wa miezi sita kuitumikia Azam, ambapo mwezi huu wa Juni ndiyo namaliza. Kama nitaongea basi mtaona tu na ikitokea nafasi hiyo basi nitapenda sana kuendelea kubaki kwenye hiki kikosi.”


SIMBA NA YANGA NI MECHI ZA PEKEE

Ngita anakiri kuwa mechi dhidi ya Simba na Yanga huwa na uzito wake kutokana na ukubwa wa timu hizo na namna zinavyojiandaa zinapokutana na Azam.

“Watu wote wanajua timu kubwa Tanzania ni Simba na Yanga. Hatupanii tunapocheza na klabu yoyote kati ya hizo, ila inakuwa mechi ngumu kwa sababu zimekutana timu zote kubwa na ngumu.

“Halafu siyo sisi tu tunaojipanga sana, hata wao wanajifua kwa sababu wanajua Azam anakuja, lazima wajipange na wakifanya mchezo basi tutawafunga. Tunakutana wote tuna nguvu, hatuendi kupiga pasi tu.”

Baada ya kuanza vizuri, Ngita ameweka wazi kuwa bado ana kiu ya kuongeza mabao kabla ya msimu kumalizika.

Anataka kufikisha idadi ambayo itaonyesha thamani yake ndani ya kikosi cha Chamazi.

“Mpaka msimu unamalizika nataka niwe na mabao 10 kwa sababu tumebakiwa na mechi tano. Nataka kufunga angalau bao moja kila mchezo, ingawa ligi ni ngumu na tuna kazi kubwa kumaliza mechi zilizosalia na mashindano ya FA pia.”


MAISHA YAKE NJE YA UWANJA

Licha ya kuwa mchezaji wa kiwango cha juu, Ngita anasema maisha yake nje ya uwanja ni ya utulivu na mara nyingi hupendelea kupumzika kuliko kwenda kwenye starehe.

Anasema maisha hayo yanamsaidia kuwa tayari kwa majukumu ya uwanjani.

“Mimi ni mtu wa kukaa sana ndani. Kama siku sina mechi, nikitoka mazoezini basi naenda zangu nyumbani. Nawaita marafiki zangu wa hapa Azam, wanakuja kucheza ‘game’, lakini siyo kwenda sehemu za starehe.

“Utulivu unamsaidia mkubwa mchezaji. Tunafanya mazoezi magumu sana, kwa hiyo kula vizuri na kupumzika ndiyo kunamfanya mchezaji aweze kucheza mechi vizuri akiwa na nguvu za kutosha.”