KVZ ilivyoweka rekodi ikitwaa ubingwa Zanzibar
Muktasari:
- Mafanikio hayo yaliyokuja chini ya Kocha Hababuu Ali akisaidiana na Ali Khalid Omar 'Kisoda' yalikuwa na panda shuka nyingi kutokana na ushindani uliokuwapo katika mashindano hayo msimu huu.
KVZ imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) msimu huu baada ya kuifunga Kipanga mabao 4-2 kwenye Uwanja wa Mao A uliopo Unguja, juzi.
Mafanikio hayo yaliyokuja chini ya Kocha Hababuu Ali akisaidiana na Ali Khalid Omar 'Kisoda' yalikuwa na panda shuka nyingi kutokana na ushindani uliokuwapo katika mashindano hayo msimu huu.
KVZ imetwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza ikiweka rekodi ya kuwa miongoni mwa timu zilizobeba ubingwa wa ZPL tangu 1984 ilipoanzishwa michuano hiyo.
Katika mechi hiyo, mshambuliaji wa kikosi hicho Michael Joseph alinogesha ubingwa kwa kufunga mabao yote manne akiwafuta machungu mashabiki wa timu hiyo ambayo msimu uliopita ilikosa ubingwa kutokana na kuzidiwa idadi ya mabao ikiwa na pointi 62 sawa na Mlandege iliyofanikiwa kunyakua taji.
Timu hiyo imevunja rekodi ya msimu uliopita kwa kutwaa ubingwa ikikusanya pointi 67 tofauti ya alama tano na imefunga mabao 60 na kufungwa 31 katika mechi 30 ilizocheza.
Mara baada ya kutangazwa mabingwa, uongozi wa timu hiyo ulilishukuru benchi la ufundi na mashabiki kwa sapoti na uvumilivu vilivyofanikisha kutwaa ubingwa huo.
“Ndoto imetimia, ubingwa ni wetu! Asanteni wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki kwa sapoti isiyo na kikomo. KVZ bingwa,” ilieleza taarifa ya KVZ.
Kabla ya kuchukua ubingwa huo, KVZ msimu huu ilianza kwa kunolewa na Kisoda, kisha Malale Hamsini na kumalizia mikononi mwa Hababuu aliyefanikiwa kuandika historia. Siku chache kabla ya kutwaa ubingwa, Hababuu aliiambia Mwanaspoti kuwa kiu ya KVZ ni ubingwa na si kingine hivyo watahakikisha wanafanikisha hilo.
Akizungumzia ushindi wao wa mwisho, alisema: "Tulipambana ili timu isishuke kileleni hadi mwisho wa msimu tukichukua ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar na tumeandika historia ya kuchukua ubingwa kwa mara ya kwanza."
Katika mchezo mwingine, JKU iliyokuwa kwenye mbio za ubingwa ilishinda 3-1 dhidi ya Chipukizi kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.
Ushindi huo umeifanya JKU kumaliza ikiwa ya pili na tofauti ya pointi tatu na mabingwa wa msimu huu, ikifunga mabao 55 na kufungwa 18, huku Mlandege iliyo nafasi ya nne iliifumua New King 2-0 ambayo itaungana na Malindi, Junguni na New Stone Town kucheza Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao ilhali Wembe, Mwenge, Black Sailors na Raskazone zikipanda Ligi Kuu.
Mechi kati ya Polisi na Mafunzo ilimalizika kwa maafande kuchezea kipigo cha mabao 2-1 huku Zimamoto iliyomaliza nafasi ya tatu ikiilaza Malindi 2-0 ilhali Fufuni iliyoanza kwa kasi na kuporomoka hadi nafasi ya sita ikimaliza msimu kwa kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Uhamiaji iliyomaliza nafasi ya tano.