Nenda Wasso! Simba na Yanga hazitakusahau

MWANDISHI WETU


AMEUMALIZA mwendo kibabe. Mwamba ameondoka. Ndio, Butu-Ingi Ramazan Waso Bakanga maarufu kama Ramadhan Wasso ameondoka. Hatutamwona tena.

Juzi ilikuwa ni siku ya majonzi kwa mashabiki wa soka nchini baada ya kusambaa kwa taarifa beki huyo wa zamani wa kimataifa wa Burundi aliyewahi kutamba na Inter Star ya Burundi, Simba, Yanga na Coastal Union amefariki dunia.

Taarifa ya kifo chake ilishtua kwa vile hakuna aliyekuwa na taarifa kama alikuwa mgonjwa. Lakini ndivyo hivyo tena, beki huyo Mrundi mwenye asili ya DR Congo ameiaga dunia akiwa Burundi wakati akipatiwa matibabu kwa kile kilichoelezwa alikuwa mgonjwa.

Utasema nini juu ya beki huyo wa kushoto aliyeweka heshima kubwa nchini hasa alipokuwa na kikosi cha Simba miaka ya 2000.

Hapa chini ni baadhi ya mambo ya kukumbukwa ya Wasso aliyoyafanya enzi za uhai wake katika soka la Tanzania, mara baada ya kutambulishwa na kufahamika zaidi akiwa na Inter Star ya Burundi kisha akaamua kuvuka mipaka 2001 kuja kujiunga na Simba.


MTU WA BAHATI

Beki huyo wa kushoto aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kukaba, kupandisha mashambulizi na kupiga krosi zenye macho atakumbukwa na wadau wa soka hususan wale wa Simba kwa jinsi alivyokuwa na zali na klabu hiyo.

Ni vigumu kuamini ukweli huu, lakini mara aliposajiliwa na Simba 2001, Wasso na baadhi ya mastaa wa timu hiyo waliirejeshea timu heshima kubwa ya kubeba mataji ambayo iliyasotea kwa muda mrefu na hadi anaondoka kitatanishi Msimbazi aliipa timu hiyo mataji zaidi ya 10.

Achana na mataji matatu ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2001, 2003 na 2007 akiwa na Simba, pia alitwaa mengine mawili akiwa na kikosi cha Yanga aliokaa nao kuanzia 2004-2006, lakini Simba ya Wasso iliweza kubeba Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame Cup) 2002 lililokuwa la mwisho kwa timu hiyo.

Kabla ya hapo Simba ililisotea kwa karibu miaka sita kwani ilitwaa mara ya mwisho 1996, lakini Wasso na wenzake walipambana na kuiwezesha kulibeba tena 2002 likiwa ni la sita kwa Simba na la mwisho hadi michuano hiyo ilipopoteza umaarufu wake.

Pia Wasso akiwa na wenzake waliiwezesha Simba kutwaa taji la Ligi Kuu ya Muungano, ililolikosa tangu ilipotwaa mara ya mwisho 1995 kwa kulibeba na kulitetea 2001 na 2002.

Simba ikiwa na Wasso pia ilitisha kwa kutwaa Kombe la michuano mipya ya Tusker Cup mara tatu mfululizo kuanzia 2001, 2002 na 2003 na alipotimkia Yanga 2004 Simba ililikosa taji hilo kabla ya kulibeba tena 2005 wakati akiwa bado na Yanga. Aliporejea tena Msimbazi kutoka Jangwani alipotwaa nao mataji mawili ya Ligi Kuu, Wasso alibeba ataji mawili - lile la 2007 ikiwa ni Ligi Ndogo, japo Yanga ilibeba taji la msimu wa 2007-2008 na kutetea tena 2008-2009 wakati akimalizana na Simba na kutua zake kwa Wagosi wa Kaya, Coastal Union aliyoichezea 2010-2011.

Kifupi, katika maisha ya kuzichezea Simba na Yanga, beki huyo wa zamani wa Bange Rouge ya DR Congo alitwaa zaidi ya mataji 11. Si mchezo!


KUIVUA TAJI ZAMALEK

Wasso ameondoka duniani, lakini ataendelea kukumbukwa kwa kuwa mmoja ya mastaa walioandika rekodi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2003.

Katika msimu huo, Simba ikiwa na kikosi kinachotajwa kuwa bora zaidi baada ya kile cha mwaka 1974 kilichofika nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa) na kile cha 1993 kilichofika fainali ya michuano ya Kombe la CAF, iliivua ubingwa wa Afrika, Zamalek ya Misri.

Katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya michuano hiyo, Simba ilishinda bao 1-0 lililowekwa kimiani na Emmanuel Gabriel ‘Batgol’, kisha Zamalek ikaenda kulipa kisasi mjini Cairo na kufanya pambano kuingia kwenye mikwaju ya penalti na Simba kushinda na kutinga hatua ya makundi.

Kutinga makundi, iliifanya Simba kuwa klabu ya pili ya Tanzania baada ya watani wao Yanga, kufanya hivyo ikiwa ya kwanza 1998 mara michuano hiyo ilipobadilishwa mfumo kutoka ile ya Klabu Bingwa Afrika 1997.

Kitendo hicho cha Simba ya kina Wasso kuting makundi, ilidumu kwa muda wa miaka 15, kabla ya timu hiyo kutinga hatua hiyo tena 2018-2019 na kupenya hadi robo fainali, wakati huo tayari beki huyo akiwa ameshastaafu kucheza soka.


CHENGA YA MSIMBAZI

Wasso ambaye rekodi zinaonyesha amezaliwa Agosti Mosi, 1984, japo wanaomjua wanasema alizaliwa 1975 atakumbukwa na viongozi na mashabiki wa Simba kwa chenga aliyowapiga 2004.

Akiwa amejijengea heshima kubwa katika nafasi ya beki wa kushoto alikuwa ni panga pangua, mwishoni mwa msimu wa 2003 aliwapiga chenga mabosi wa Simba kwa kugoma kuongezewa mkataba mpya kwa madai amepata timu ya kucheza soka la kulipwa huko Ubelgiji.

Kama ilivyo utamaduni wa Simba kutowawekea kauzibe wachezaji wanapopata dili za nje, ilimruhusu kuondoka na baadhi kupanga kumsindikiza Uwanja wa Ndege, lakini jamaa hakuwa na safari wala nini ila aliibukia Jangwani kujiunga na Yanga.

Usajili wale ulileta mzozo kiasi cha Simba kulalamika Chama cha Soka Tanzania (FAT, sasa TFF) lakini haikufua dafu na jamaa alivaa uzi za rangi za Kijani na Njano za Yanga, japo hakuwa na bahati na klabu hiyo kulinganisha na Simba. Sio Wasso tu waliolalamikiwa na Simba msimu huo, pia kulikuwa na beki Ramadhan Rashid ‘Carlos’, Wakongo Pitchou Kongo, Patrick Kataray na Aloo Kuzulu Ziwanuka.

Kuondoka kwake ghafla kuliipa kazi kubwa Simba kusaka beki wa kushoto hadi ilipowanasa kina Juma Jabu, Nassor Masoud ‘Chollo’ hadi leo ikiwa na Mohmmed Hussein ‘Tshabalala’ ambao hata hivyo, waliachwa mbali na beki huyo Mrundi kwa aina ya uchezaji kuanzia ukabaji, nguvu, akili na kasi pamoja na uwezo aliokuwa nao katika kupiga krosi na kuisaidia timu kutengeneza mashambulizi.

Mwaka huo wa 2004, kwa bahati mbaya zaidi, Simba ilitetea taji la Ligi Kuu kwa mara ya pili mfululizo na Wasso akiwa na Yanga walitoka kapa.

Beki huyo alipoteza ile kasi aliyokuwa nayo na haikuwa ajabu alipomaliza mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo, aliamua kujisalimisha tena Msimbazi 2007 na kuicheza kwa misimu miwili hadi 2009 akitwaa nayo taji moja la Ligi Ndogo na kukimbilia Coastal Union iliyokuja kumtema 2012 na kuamua kustaafu kabisa kucheza soka la ushindani na kudili na mambo binafsi ikiwamo uchambuzi wa soka akitumika zaidi na kituo cha Televisheni za Tv3.


MKONGOMANI

Mashabiki wengi wa soka hawakuwa wanafahamu kama Wasso alikuwa ni Mkongomani, ila ukweli jamaa jina lake halisi lilikuwa ni Mutu- Ungi ‘Ramazan’ Waso Bukanga aliyezaliwa 1975, japo pasipoti yake ilikuwa ikisomeka ni 1984.

Soka lake lilianzia katika klabu ya Bange Rouge  1994 na kudumu nayo hadi 1998 kabla ya kuvuka mpaka kuingia Burundi alikobadilisha pia uraia wake mara alipojiunga na Inter Star aliyokaa nayo kuanzia 1999-2000 na kuonwa na Simba iliyomvuta 2001.

Kifupi, Wasso imebaki historia tu, kwani mwamba ameondoka akiwa katika ardhi ya nchi aliyoitumikia kimataifa kupitia timu ya taifa ya Burundi ‘Intamba m’Urugamba kati 2002-2007.

Hakuna kauli nyingine ya kumtakia Wasso zaidi ya kusema kila la heri katika safari yake ya Ahera akiwa ameondoka ndani ya mwezi unaofanana na jina lake, yaani Mfungo wa Ramadhani. Kwa hakika sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.