Nenda Kuka fundi wa mpira

MWANDISHI WETU


WIKI moja tu tangu familia ya michezo hususan soka kupata pigo baada ya beki wa zamani wa kimataifa aliyewika Simba na Yanga, Ramadhani Wasso kufariki dunia akiwa kwao Burundi, wikiendi iliyopita familia hiyo ilipata pigo jingine kwa Abbas Kuka naye kukumbwa na mauti na kuzikwa jana.

Kwa watoto wa miaka ya 2000 wanaojifanya wajuaji ni ngumu kumjua fundi huyo wa mpira aliyevuma na Simba na Nyota Nyekundu, ila jamaa alikuwa fundi kwelikweli na bishoo flani hivi aliyependa kupiga pamba za kipapaa hata alipostafu soka miaka ya mwishoni ya 1990.

Majina halisi yalikuwa ni Abbas Sais Mhunzi, lakini alifahamika zaidi kama Abbas Kuka ikiwa ni mmoja wa nyota maarufu waliowahi kukipiga Simba na aliyekuwa kwenye kikosi kilichoweka rekodi katika michuano ya CAF mwaka 1979.

Kiungo huyu mkabaji alimudu pia kucheza kama beki wa kati enzi za uhai wake kuanzia miaka ya katikati ya 1970 hadi alipostaafu akiwa na timu iliyofutika kwenye ulimwengu wa soka, Nyota Nyekundu alipewa jina la Kuka likitoolewa kutoka neno la Cooker ambalo limaana na mpishi.

Kuka alikuwa mpishi wa mipira kwa wenzake, alikuwa akiupiga mwingi na licha ya kutangulia mbele ya haki baada ya kuzikwa jana jioni, mkongwe huyo ataendelea kukumbukwa kwa kipaji alichokuwa nacho na namna alivyokitumia kuizisaidia timu alizozitumikia enzi za uhai wake.

Kwa wanaokumbuka katika mahojiano maalumu aliyowahi kufanya na Mwanaspoti kupitia Mwandishi Nguli nchini, Ezekiel Kamwaga alifunguka mambo mengi juu ya safari yake ya soka na matukio ambayo yalibaki kichwani mwake, likiwamo la kuiduwaza Mufurila Wanderers ya Zambia ikiwa kwao kwa kupindua meza ya kipigo cha 4-0 ilichopewa Simba nyumbani na kuwafumua Wazambia hao 5-0.

Pia aliweka bayana juu ya kifo cha mchezaji mwenzake aliyekuwa akishea chumba kimoja kambini, Hussein Tindwa aliyeanguka uwanjani wakati wa mechi za CAF dhidi ya Racca Rovers ya Nigeria na kufariki dunia akiwa njiani kuwahishwa Hospitali ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.


KIFO CHAKE

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa watu wa karibu wa Kuka, waliliambia Mwanaspoti ngwiji huyo wa soka alianguka akiwa msikitini juzi huko Magomeni na kuzikwa jana na katika kumuenzi tumeamua kukumbushia machache aliyowahio kuhojiwa enzi za uhai wake wakati tukimtakia kila la kheri katika safari yake ya kwenda mbele ya haki, kwani kila nafsi ni lazima itaionja mauti.


HISTORIA CAF

Kuka aliyekuwa anajipenda kwelikweli na kuutunza mwili wake, kiasi hata alipostaafu hakuwa na mwili mnene. Alikuwa na mwili mkavu usio na kitambi ikiwa ni miaka mingi ya utamaduni wa kula kwa adabu na mazoezi tangu angali akiwa mchezaji.

Mwenyewe aliwahi kujifananisha na aliyekuwa kiungo wa Simba, Taddeo Lwanga wakati akifanyiwa mahojiano hayo wakati kiungo huyo Mganda akiwa Msimbazi, lakini akasema yeye (Kuka) alikuwa fundi zaidi.

Kuka alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika historia ya Simba. Yeye alishiriki katika mechi mbili ambazo historia yake haitafutika katika dunia ya soka la Tanzania. Alishiriki katika pambano la mwaka 1979 jijini Lusaka, Zambia, ambako Simba iliweka historia ambayo haijavunjwa hadi leo barani Afrika kwa kuifunga Mufulira Wanderers mabao 5-0.

Kwa matokeo hayo, Simba iliitoa mashindanoni Mufulira – ambayo ilishinda katika mechi ya kwanza iliyochezwa Dar es Salaam kwa kuifunga Simba mabao 4-0. Kuka hajasimuliwa kuhusu mechi hii, alikuwa sehemu ya waliocheza.

Historia ya pili ambayo Kuka anayo kwa Simba, alikuwa uwanjani Mei 13, 1979 wakati mchezaji mwenzake Hussein Tindwa, alipoanguka ghafla uwanjani katika mechi dhidi ya Racca Rovers ya Nigeria na kufariki dunia wakati akipelekwa kutibiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Tindwa anabaki kuwa mchezaji pekee wa Simba kufia uwanjani katika historia ya klabu. Ni msemo maarufu unaotumiwa na wachezaji, washabiki na viongozi wa klabu mbalimbali kuwa wako tayari kufia uwanjani lakini ni Tindwa peke yake ambaye hili limemkuta kwa vitendo.

Hapa ndipo hasa nilipoanzia mazungumzo yangu na Kuka.

“Nakumbuka tukio zima la kifo cha Tindwa kana kwamba lilitokea jana. Kwanza nikwambie mimi Hussein alikuwa rafiki yangu na mara nyingi tulikuwa tukilala chumba kimoja wakati Simba ilipokuwa kambini,” alinukuliwa kwenye mahojiano na Kamwaga na kuongeza;

“Yeye, kama mimi, alikuwa akicheza kama mlinzi wa kati na ndiyo sababu ya kuwa na urafiki wa karibu. Siku anafariki dunia tulikuwa tunacheza mashindano ya Klabu Bingwa ya Afrika baada ya kuwatoa Mufulira. Tulicheza na Racca Rovers kutoka Nigeria waliokuwa mabingwa wa nchi hiyo wakati huo.

“Simba iliweka kambi Kibaha kujiandaa na mechi. Mimi nakumbuka tangu asubuhi Hussein hakuwa na furaha. Nilimuuliza asubuhi mbona leo umeamka kama vile hauna furaha au kuna kitu kimekutokea? Alinijibu hana tatizo lolote na hajui kwa nini yuko hivyo.

“Tulikwenda kucheza mechi ile na alipangwa kama mmoja wa walinzi wa kati. Alicheza vizuri tu na nakumbuka tatizo lilitokea karibu kabisa na muda wa mapumziko. Ulipigwa mpira wa juu naye akaruka kuokoa na kuanguka chini. Nakumbuka ule mpira ulipookolewa tu ndiyo mwamuzi akapuliza kipyenga cha mapumziko.

“Wakati tunatoka kwenda vyumbani kwa ajili ya mapumziko, nilimuuliza marehemu Mohamed Kajole ‘Machela’, nini kimetokea kwa sababu Tindwa hakuwa ameamka. Kajole alitujibu kwa ishara tu alikuwa na kizunguzungu. Tukajua ni jambo la kawaida tu na atapata nafuu. Hakupata nafuu na tukaja kuambiwa baada ya mechi kumalizika alifariki dunia wakati anapelekwa hospitali.

“Maana yake, wakati sisi tunaendelea na mechi pale Uwanja wa Uhuru (zamani Uwanja wa Taifa), mwenzetu alikuwa anapigania maisha yake na kukata roho. Sitasahau hali ya huzuni kwangu, wenzangu na mashabiki baada ya msiba huo. Alikufa akiwa kijana kabisa,” alisimulia Kuka.


KIPAJI HALISI

Kuka ni mmoja wa vijana wadogo wa Dar es Salaam waliokuwa wakienda kucheza soka katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa miaka ya 1970. Huko kwenye soka la watoto ndiko kipaji chake kilipoonekana hadi kuchukuliwa kuchezea kikosi cha vijana cha Simba mwaka 1972 na baadaye kupata nafasi katika kikosi cha wakubwa.

Wakati kina Kuka wakiibuka, Simba ndio ilikuwa imetengeneza kikosi kinachohesabika kuwa ndiyo bora zaidi katika historia ya klabu. Kama isingekuwa fitna za Wamisri mwaka 1974 kwenye mechi dhidi ya Mehalla El Kubra, huenda Simba ingetwaa ubingwa wa Ligi ya Klabu Bingwa Afrika wakati ule.

Langoni kulikuwa na Athumani Mambosasa, anayetajwa kama kipa bora kabisa kuwahi kuzaliwa Tanzania. Mabeki wa pembeni walikuwa watu wa aina ya Shabani Baraza na Mohamed Kajole – beki tatu ambaye inaelezwa hana mfanowe katika historia ya kabumbu hapa Tanzania.

Timu ilijinasibu kwa kuwa na watu wa aina ya marehemu Willy Mwaijibe – kwa mara nyingine, winga wa kulia ambaye mfanowe hakuna tangu kuumbwa kwa Tanzania. Na bado walikuwapo nyota wengine wa kiwango cha juu kabisa kama akina Adam Sabu, Dilunga na wengine.

“Haikuwa mchezo kwa mchezaji kutoka timu yoyote, achilia mbali sisi wa timu ya watoto kuja kucheza Simba wakati ule. Ushindani ulikuwa mkali kiasi kwamba siku nawe ukiambiwa sasa uko tayari kuvaa jezi ya timu ya wakubwa, ujue kweli wewe umeiva,” anasimulia Kuka.


MAISHA BAADA YA SIMBA

Mwanzoni mwa miaka ya 1980, Kuka aliamua kuachana na soka na kujikita katika ajira yake serikalini. Kwa miaka yao, ilikuwa jambo la kawaida kwa mchezaji mpira kuwa na ajira nyingine kwa sababu mchezo wenyewe ulikuwa wa ridhaa tu.

Miaka takribani mitano baada ya kuamua kustaafu, alifuatwa nyumbani na mmoja wa wachezaji wenzake wa zamani wa Simba, Omar Mahadhi, akimtaka ajiunge na klabu ya Nyota Nyekundu. Mahadhi alikuwa ameanza ukocha na kufundisha klabu hiyo iliyotokana na mgawanyiko uliotokea ndani ya Simba.

Mahadhi alimwambia alikuwa anamwona mazoezini anakofanya na aliamini bado ana uwezo wa kucheza soka katika kiwango cha ligi daraja la kwanza wakati ule. Kwa sababu ya urafiki na kuheshimiana kwao, Kuka akakubali.

Ndiyo ukawa mwanzo wa kuanza si tu kuchezea Nyota Nyekundu, lakini kuiongoza pia kama nahodha.

Kuka alistaafu rasmi kucheza soka mwanzoni mwa miaka ya 1990 na alikuwa anaishia eneo la Magomeni, jijini Dar es Salaam hadi mauti yalipomkuta juzi na kuzikwa jana.