Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nassoro Hamduni: Hatatokea mwamuzi kama mimi

NASSORO Hamduni ni mwamuzi mkongwe nchini, ambaye amefanya mengi katika soka hususani fani yake ya urefarii, akipitia milima na mabonde katika miaka 39 aliyofanya kazi hiyo kabla ya kustaafu.

Ni miongoni mwa wanadamu wachache wacheshi, wenye ukarimu anapokutana na mtu na hachoshi kumsikiliza anapozungumza jambo lake ama kukufafanulia kile anachohitaji ukifahamu kutoka kwake.

Stori zake zinavutia na wakati wote mtajikuta mkicheka kwa hadithi nzuri anazosimulia hasa kuhusiana na maisha yake ya ujana na sasa na ndipo utakapogundua kwamba ni mtu wa aina gani.

Kwanza anakutana na mwandishi wa Mwanaspoti, baada ya salamu kilichofuata ni kumkaribisha kwenye chumba ambacho kilikuwa na waamuzi wote wa Ligi Kuu wakiendelea kukumbushwa mambo kadha wa kadha juu ya taaluma yao kabla msimu haujaanza.

Kwa ucheshi mkubwa anamtambulisha mwandishi kwa waamuzi hao na kusalimia nao na baadaye tulitoka nje kwa ajili ya kile kilichonipeleka kwake na hakuwa mgumu kusikiliza na kujibu.

Katika mahojiano hayo, aliyoyafanya na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Hamdani hakusita kwanza kusimulia moja ya tukio alilowahi kukutana nalo akiwa kazini. Kwa hakika katika kila kazi kunakuwa na changamoto zake ambazo baadhi unaweza kushinda na nyingine hutoboi kama watoto wa mjini wanavyosema.

“Nakumbuka kuna tukio moja lilitokea mwaka 1989 kulikuwa na mashindano ya Kombe la Muungano yalifanyika Zanzibar, sasa nilipotoka uwanjani yaani baada ya mechi nilirudi hotelini, nilipofika niliambiwa nina mgeni wangu alikuwa wa kike (taarifa kutoka mapokezi).

“Miaka hiyo hukukuwa na mambo ya simu na sikufahamu ni mgeni gani, niliambiwa tayari yupo chumbani kwangu, kweli nilipofika huko nikamkuta. Nilistuka kwasababu sikuwa nikimfahamu, nilishangaa kwamba mtu ambaye simfahamu ameruhusiwaje kuingia ndani kwangu. Je, kama alikuja kunidhuru?

“Nilipomuuliza kafuata nini, akasema eti ananifahamu kwa kazi yangu ninayofanya na amekuwa akivutiwa na ninachofanya uwanjani hivyo amehitaji tu kuja kuniona kama shabiki wangu na kufahamiana nami. Hofu niliyokuwa nayo ikaondoka nikamwambia nimefurahi kujua kwamba pia waamuzi tuna mashabiki. Baadaye akaaga akaondoka. Na tangu hapo sikuwahi kuonana naye tena. Hapo najaribu kusema kwenye kila kazi kuna changamoto zake ambazo mtu anaweza kukutana nazo, sasa namna ya kutatua ni mtu mwenyewe anavyoona atatue kikubwa ili zisikutoe kwenye maadili ya kazi.”

Hamduni ni Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi iliyo chini ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na ni kiongozi ambaye ana misimamo yake ya kazi, ilimradi hatoki kwenye msingi wa kazi yake pasipo kumwonea mtu yeyote.

Haya hapa ni kadha wa kadha kumhusu Hamduni;


REKODI YAKE HAIJAVUNJWA

Ni mwamuzi pekee aliyechezesha dabi nyingi za Simba na Yanga, akichezesha mechi 11 za watani hao wa jadi ambazo ni za mashindano ukiachana na zile za mabonanza.

“Nilichezesha kwa miaka 39, napenda kazi yangu maana ndiyo taaluma yangu na ndiyo maisha yangu. Haijawahi kutokea hadi sasa labda hapo baadaye mwamuzi kuvunja rekodi yangu ya kuchezea mechi 11 za dabi kama ilivyokuwa kwangu.

“Niliingia kwenye uamuzi kutafuta jina na heshima, kujiongezea kipato kilichokuwa halali ingawa kwa waamuzi wengi wa sasa hawaingii kujitafutia heshima wanatafuta kipato. Heshima haiwezi kuwepo kwa kutaka kipato, hapo ni lazima kimoja ukiache, mimi nilichagua heshima na kuacha kipato na sikufaidika na kipato.” anasema na kuongeza;

“Kwenye hii kamati nina mwaka wa tatu, lakini nilishakuwa mechi kamishna, mtathimini wa waamuzi, kama ingekuwa kwenye shirika la reli basi ingekuwa kuanzia kwenye chini hadi kuajiriwa kuwa meneja, hivyo nimefuata misingi yote kufika hapa.

“Nimechezesha hadi mechi za kimataifa, kwenye hii kamati sijaingia kimakosa, najiona ni mtu sahihi kuwemo humu. Utulivu uliopo sasa sio sawa na siku za nyuma, kusimamishwa kwa waamuzi wengi lengo letu ni kuweka heshima kutokana na makosa yaliyokuwa yanajitokeza na kutaka kila mmoja afuate sheria na kanuni zinavyoeleza.” anasema Hamduni.


WAAMUZI WAONJA JOTO YA JIWE

Msimu uliopita waamuzi zaidi ya 20 walifungiwa kuchezesha mechi za Ligi Kuu Bara, Hamduni anafafanua.

“Kwanza tulichofanya kwenye Bodi ya Ligi ni kulinda heshima ya waamuzi wetu kwamba pale inapobainika wana makosa waturudishie, watuambie mwamuzi fulani hatuwezi kuwa naye basi tunamuondoa kwenye ratiba, bodi (TPLB) ndio wenye ligi yao, na sisi huwa tunawaombea kazi waamuzi wetu.

“Hivi unaweza kuwatupa waamuzi zaidi ya 20 na wana familia kweli wakae nje, sasa Katibu Mkuu wa TFF naye akikataa basi nakuwa sina namna, au bodi wakikataa basi hakuna cha kufanya, ndio maana unaweza kuona mwamuzi fulani hayupo kuchezesha mechi za ligi lakini anaonekana FA na mashindano mengine yaliyo chini ya TFF na sio bodi ya ligi.

“Kamati ya waamuzi haina mashindano, kamati zote zikimkataa nawarudishia FRAT (Chama cha Waamuzi Tanzania), ambao ndiyo wanachama wao, huwa tunakaa nao tunazungumza mengi.

“Huwezi kuzuia wala kuwalinda, waamuzi wana mawasiliano na watu wengi na huwezi kujua, ingawa tulibaini sasa baada ya lile sakasaka la kuvurunda. Ilibidi tu hatua zichukuliwe maana ulifanywa uchunguzi kiasi kwamba hata mimi ingeniletea shida maana ni kiongozi wao hivyo wangedhani hata mimi nahusika, ila pona yangu baada ya uchunguzi haikubainika lolote baya juu yangu.” anasema.


WANAWAKE WAPO JUU

Msimu uliopita waamuzi wa kike walionekana kuchezesha mechi zaidi ya wanaume, bosi huyo anaeleza sababu;

“Waamuzi wengi wa kike wamechezesha sana, katikati hapa mashindano yetu yalikumbwa na sintofahamu nyingi, kalamu zenu waandishi wa habari zimetusaidia kufanya kazi. Sintofahamu hiyo ndiyo ilitusaidia tutumie zaidi watoto wa kike kwanza ni wajasiri sana, wana hofu ya Mungu na wana roho ya ulezi.

“Tunawapongeza waamuzi wa kike na wametubeba, wamewapa sifa wanawake wote hawajawaamsha, tupo vizuri hatuwapendelei na wana uwezo mkubwa sana.

“Kuna binti mmoja nilimuona huko Moro hivi karibuni, niliona ana kipaji na ni hazina yetu, tunalenga misimu miwili ama mitatu kina Jonesia Rukyaa hawatakuwepo, ukiangalia hata sasa amerudi nyuma kidogo kwasababu ya familia na kwa asilimia kubwa mwanamke anapungua uwezo, na anafahamu kila chenye mwanzo kina mwisho.

“Hakuna asiyejua kuwa sisi Waafrika rasilimali yetu ni wazazi lazima atengeneze familia, hivyo lazima watengenezwe wengine, kwa kifupi msimu ujao mtegemee kuwa na waamuzi wengi wa kike ingawa hamtawapata kwenye Ligi Kuu kwanza, kuna kozi zinaendelea na waamuzi wengi wa kike wamejitokeza.”


JONESIA, TATU WAFUNIKA

Pamoja na kwamba wengi walifungiwa msimu uliopita lakini kinadada Jonesia Rukyaa na Tatu Marogo ndiyo waliochezesha mechi nyingi zaidi.

“Wamechezesha mechi nyingi tena zenye mwonekano kwasababu wengi walikuwa wamesimamishwa, waliosimamishwa ni taratibu za nje ya uwanja ndio ziliwaondoa na hatuwezi kuweka wazi. Wakati mwi-ngine tunapata taarifa kabla hata ya mchezo kuchezwa ingawa kuna vitu vingine havina ushahidi kuvithibitisha hasa kwenye mambo ya rushwa.”


Itaendelea kesho...