Nado winga Azam anayewaza makubwa

Muktasari:

HAIKUWA rahisi jina la Iddy Nado kuwa kubwa miongoni mwa wadau wa soka nchini kwani staa huyu wa Azam FC alitoa jasho, hakukata tamaa na aliamini ipo siku atatambulisha madini yaliyopo mguuni kwake.

HAIKUWA rahisi jina la Iddy Nado kuwa kubwa miongoni mwa wadau wa soka nchini kwani staa huyu wa Azam FC alitoa jasho, hakukata tamaa na aliamini ipo siku atatambulisha madini yaliyopo mguuni kwake.

Harakati za kukuza jina lake zilianzia kucheza ndondo alikoonekana na viongozi wa Mbeya City msimu wa 2017/18, lakini hakuishia hapo alijituma zaidi hadi Azam FC ikatamani huduma yake.

Mwanaspoti lilifunga safari kumfuata Nado kambini kwao Chamanzi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kuzungumza naye mambo mawili - matatu kuhusiana na safari yake ya soka.


ALIPOANZIA

Winga huyu alianza kufahamika zaidi katika mashindano ya mtaani maarufu kama ‘Ndondo Cup’ 2015 wakati huo akiwa anaichezea timu ya Makumba FC ya Ilala.

Makumba ni timu ya wauza vifaa vya magari na katika msimu huo Nado aliiongoza kushika nafasi ya tatu, huku yeye akiibuka mchezaji bora wa mashindano ya Ndondo Cup mwaka huo.

Mwaka 2016 alihamia timu ya Misosi FC iliyokuwa na makazi yake mitaa ya Tandale. Akiwa na Misosi walifanikiwa kufika hatua ya nusu fainali na kucheza mechi ya kuwania nafasi ya tatu walikofungwa na Makumba FC mechi ambayo Nado hakucheza.

Sababu ya kutocheza wakati wa mchezo huo alijisikia vibaya kucheza dhidi ya timu ambayo msimu mmoja nyuma ilimpa nafasi na akafanikiwa kuwa mchezaji bora wa mashindano.

Msimu wa 2017 alichezea tena Misosi FC na safari hii aliiongoza kuwa mabingwa wa michuano hiyo na bBaada ya msimu huo kwisha alisajiliwa na Mbeya City kwa ajili ya msimu wa Ligi Kuu Bara 2017/18.


MKOPI AMVUTA MBEYA CITY

Baada ya kuitumikia michuano ya Ndondo CUP, Nado anasema alipata dili la kujiunga na Mbeya City msimu wa 2017/18 kutokana na kiwango bora alichokionyesha wakati huo akiwa na Misosi FC, huku akimtaja nyota wa Tanzania Prisons, Mohamed Mkopi kumsaidia katika usajili ule.

“Mkopi ndiye alinifanya nifike Mbeya City kwa sababu wakati anasajiliwa pale akitokea Tanzania Prisons aliwaambia mabosi wanichukue na wakafanya hivyo,” anasema.

ALIANZA KWA MAJARIBIO MBEYA CITY

Nado anasema licha ya Mkopi kuwaambia ubora wake wamchukue, lakini mabosi hawakumwamini moja kwa moja kwani walitaka waendelee kumpa muda mwingi zaidi wa kucheza.

“Sikuwa na mkataba wakati najiunga, bali nilianza kucheza kwa majaribio ya wiki mbili mpaka pale viongozi walipojiridhisha na kunipa mkataba wa kuitumikia klabu yao,” anasema.


MECHI NA AZAM YAMPA MKATABA

Nando aliuwasha mwingi na anakumbuka katika mchezo dhidi ya Azam FC hapo ndipo alipolamba dume.

“Nakumbuka wakati Mbeya City wanatambulisha jezi kwa msimu ule, walicheza mchezo wa kirafiki na Azam FC. Baada ya mchezo ule ndipo viongozi walipoweza kunipa mkataba wa kuitumikia rasmi klabu hiyo,” anasema.


AZAM NJIA SAHIHI

Licha ya wachezaji kadhaa kutengeneza ufalme wa kutohama klabu walizozitumikia kwa muda mrefu, ila kwa Nado ni tofauti kwani anaamini Azam ni njia ya kufika mbali zaidi ya alipo.

“Nina malengo makubwa ya kucheza klabu kubwa zaidi ya hapa, hivyo naamini hapa Azam ni njia yangu sahihi ya kutimiza malengo niliyojiwekea kwa sababu bado sijaridhika.”


UPAMBANAJI SILAHA YAke

Azam ni timu ambayo imekuwa na maingizo mengi ya wachezaji wa kigeni, lakini kwa Nado hilo halimpi presha kwani anaamini ana uwezo wa kupambana nao.

“Najivunia kuwa mpambanaji asiyekata tamaa. Uwepo wa wageni ni jambo zuri linalonipa changamoto ya kupambana na kufanya vizuri zaidi na kuendelea kupata nafasi na kuisaidia timu,” anasema.


AZAM NOMA, UBINGWA NI SUALA LA MUDA

Azam imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara moja tu msimu wa 2013-14 wakati huo ikiwa na kocha Joseph Omog tangu ilipopanda Ligi Kuu 2009, lakini Nado anaamini msimu huu timu hiyo inaweza kuwa bora zaidi kutokana na maandalizi iliyoyafanya.

“Sina muda mrefu, ila viongozi wako siriazi sana tofauti na miaka ya nyuma jambo ambalo ulikuwa hulipati, kitu kinachoonyesha kabisa kuwa wanataka makombe kwa kuwa uwezo wa kuyachukua tunao na sasa kazi ni kwetu wachezaji na benchi la ufundi kuhakikisha tunaleta makombe hapa,” anasema.

Simba na Yanga zimekuwa zikitawala kwenye soka la Bongo ukilinganisha na Azam ambayo pia ina wachezaji nyota na rasilimali za kutosha, jambo hilo linamuumiza sana Nado kitu ambacho anaamini utafikia muda kupindua meza na Azam kufanya vizuri zaidi.

“Kila jambo ni mipango ya Mwenyezi Mungu, hivyo binafsi naona wakati wetu utakapofika tutachukua ubingwa. Ujue kila msimu tunatamani kufanya hivyo, lakini mambo yanabadilika lakini nadhani msimu huu tunayo nafasi ya kutwaa ubingwa.”


NITAIPAMBANIA AZAM

Msimu uliomalizika Nado ni mchezaji mzawa aliyehusika katika mabao mengi akihusika nayo 18 - akifunga mabao 10 na kutoa asisti nane sawa na John Bocco wa Simba aliyefunga mabao 16 na kutoa asisti mbili kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliomalizika na ametamba msimu huu kufanya vizuri zaidi ya hapo.

“Mimi ni mpambanaji, nataka kufunga mabao mengi zaidi msimu ujao ili niweze kuisadia timu yangu kutwaa ubingwa ambao ndio malengo yetu makuu,” anasema.


NDONDO NI

SEHEMU YA VIPAJI

Kama alivyotokea kwenye soka la mchangani, winga huyo anazitaka klabu za Ligi Kuu Bara kutafuta wachezaji wa ndani na kuacha kukimbiliwa nje.

“Wapo wachezaji wengi kwenye michuano ya ndondo kwa mfano Manzese, Tandale, Mbagala na sehemu mbalimbali ambao wana uwezo ila wanakosa tu fursa ya kuchukuliwa kwenye klabu kubwa na kuonyesha vipaji vyao,” anasema.


SAPOTI ya wazazi

Wapo baadhi ya wazazi hawawapi watoto wao msaada au kutowaunga mkono wanapokuwa na jambo lao, lakini Nado anasema hilo hakulipitia.

“Wazazi wangu waliniunga mkono kucheza mpira kwani waliamini nina uwezo wa kufika mbali na kufanikiwa kwenye maisha, hivyo safari yangu haikuwa ngumu jambo ambalo lilinipa nguvu kubwa ya kupambana.”


wakali wake

Nado anasema wapo wachezaji wengi waliomvutia kucheza soka hadi kufika hapo alipo na miongoni mwao ni winga Mrisho Ngasa aliyechezea klabu mbalimbali hapa nchini zikiwemo Simba, Yanga na azam FC pamoja na kiungo Mzanzibar Khamis Mcha aliyechezea klabu za Miembeni SC, Zanzibar Ocean View, Azam FC na sasa Dodoma Jiji.


Asichosahau

Mchezaji huyo anasema wakati yupo Mbeya City kulikuwa na kiongozi aliyekuwa anamkatisha tamaa kwani alikuwa akimwambia kuwa bado uwezo wake ni mdogo.

“Niliumia sana kwa sababu niliona kama anataka kunirudisha nilipotoka. Jambo hilo liliniuma kwa sababu alikuwa akinisema mbele ya viongozi wengine waliokuwa wakiamini uwezo wangu,” anasema.


NJE YA SOKA

Licha ya kipaji kikubwa alichonacho kucheza soka, Nado anasema anapenda sana kusikiliza muziki na kuangalia ngumi.


LUIS NOMA

Nado anasema staa aliyeichezea Simba msimu uliopita Luis Miquissone ambaye kwa sasa yupo Al Ahly ya Misri ndiye aliyekuwa akimpa changamoto kila walipokutana uwanjani.

“Ukiangalia msimu ulioisha nilimzidi bao moja na yeye alinizidi asisti moja, hivyo kila mechi anayocheza lazima niangalie kafanya nini ili nifanye bora zaidi yake jambo ambalo lilikuwa likinipa changamoto,” anasema.


WASIKIE wadau

Kocha Mkuu wa Azam, George Lwandamina anamzungumzia Nado kuwa ni mchezaji mwenye nidhamu, anayejituma mazoezini sambamba na kufuata maelekezo.

“Nado ni mzawa anayecheza kama wachezaji wa kigeni. Ana uchu na mafanikio, pia nidhamu yake ni kubwa na anafuata maelekezo vyema. Pia yupo tayari kukosolewa muda wowote na hiyo ndio inamfanya azidi kung’ara,” anasema Lwandamina.

Mchezaji wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ anasema kiwango anachoonyesha Nado kinaashiria kuwa anatamani kufika mbali zaidi ya hapo alipo.

“Ni mpambanaji sana, ingawa kuna muda unaona kabisa timu inamuangusha, lakini anajitangaza vizuri kwenye medani ya soka,” anasema Mogella.

Kocha msaidizi wa Simba Queens, Matty Mseti anasema huu ni wakati kwa mchezaji huyo kutafuta changamoto mahala pengine kutokana na kiwango ambacho amekuwa nacho katika miaka ya hivi karibuni.

“(Nado) anapoelekea ataonekana wa kawaida licha ya upambanaji wake, hivyo ni wakati kwake wa kutafuta timu nyingine tofauti na Azam, hususan nje ya nchi,” anasema kocha huyo.

Imeandikwa na DAUDI ELIBAHATI, RAMADHAN ELIAS NA CHARITY JAMES