MZUKA WA GOFU- Shabir: Elimu ya gofu ina umuhimu

TAALUMA ni jambo la msingi sana kwa vijana, vikiambatana na nidhamu na uaminifu, vinaweza vikawasaidia kufikia mafanikio yao.

Mzuka wa Gofu kupitia gazeti la Mwanaspoti limefanya mahojiano na mchezaji wa gofu wa ridhaa, Shabir Abji ambaye ni Mkurugenzi wa New Africa Hotel na Mwenyekiti wa Shule za Aghakhan anayeeleza umuhimu wa elimu kwa vijana unavyohitajika.

Shabir anaulizwa kupitia macaddy ambako kuna vijana wengi ni kipi amekiona na anadhani kinapaswa kufanyiwa kazi, anajibu; “Kuna wakati unatamani utoe msaada, ila unakuta wengi hawana ujuzi, jambo ambalo linanisikitisha.”

“Kama binadamu najiuliza, siku caddy hajafanya kazi, anaendeshaje maisha ya familia yake, natamani itokee kwenye familia zao, watoto wawekeze nguvu kwenye elimu, sina maana kazi yao mbaya la hasha, kazi yao ni muhimu sana.”

Anaeleza asilimia kubwa wamemaliza darasa la saba na wanategemewa kwenye familia, hivyo wakaona wafanye kazi ambazo zipo mbele yao japo naona kuna kitu kinahitajika zaidi.

“Kwenye gofu ukiwa na fani ni rahisi sana, kupata watu wa kukushika mkono, kwa maana kukutafutia kazi ambayo unaweza kuifanya,” anasema.

Jambo lingine analolisisitiza, Shabir ni uaminifu na nidhamu kwani uzoefu wake kwenye mchezo huo, umemsaidia kuwajua watu ni wa aina gani.

“Mchezo wa gofu kuna wakati tunapiga stori, ni rahisi kuwafahamu watu wanavyochukulia mambo, pia kujua uaminifu wao ni wa kiasi gani, ngumu kumchukua mtu kumpa nafasi fulani kama utagundua siyo mwaminifu wala hana nidhamu,” anasema.

UGONJWA WA KISUKARI

Anasema miaka 25 iliyopita aligundulika ana ugonjwa wa kisukari na madaktari walimshauri kufanya mazoezi ya kutembea sana, akaona kwenye gofu ni sehemu sahihi.

“Nisingeweza kufanya mazoezi ya kutembea barabarani kawaida, hilo niliona linashindikana, ila nina rafiki yangu aliniambia twende kwenye mchezo wa gofu huko kutakufaa na baada ya kwenda siku ya kwanza tu nikapapenda,” anasema na kuongeza;

“Umekuwa mchezo ambao umenisaidia sana kiafya na unapunguza matumizi makubwa ya dawa, sijasema nimeacha kumeza, ila nikifanya mazoezi inapungua kwa sababu unaweza ukatembea kilomita saba jambo ambalo ni nzuri kiafya bila kujali umri.”

Licha ya mchezo huo kuuchukulia kumsaidia kushusha sukari ila anasema umemsaidia kunyakuwa mataji mengi kwani hadi sasa ana handcup 8, japo anatamani kushusha hadi kupata handcup 0 ambazo ndizo wanazotumia kuchezea kwa upande wa mapro.

Mbali na hilo anamtaja mchezaji kijana wa klabu ya Dar es Salaam Gymkhana, Victor Joseph ana uwezo na anapaswa kupewa sapoti endapo ataongeza elimu ya mchezo huo japo kituo cha gofu Afrika Kusini wanaangalia vigezo tofauti na kucheza.

Pia hajasahau kwa upande wa wanawake akiwataja kina Madina Idd na Hawa Wanyeche ambao anawaona wanafanya vizuri huku akiamini endapo wataendelea hivyo watafika mbali zaidi japo amewataka kuongeza zaidi elimu na fani nyingine ya mchezo huo.

Jambo lingine wanalotarajia kulifanya kwa mwaka huu ni kuwekeza nguvu shuleni, ili kupata watoto angalau wanaoonyesha wanaweza kucheza kisha wawaendeleze.

“Mwaka huu utakuwa wa tofauti sana, watoto wakijifunza mapema ni ajira pia kupitia taaluma zao ama ujuzi itakuwa rahisi kwao kupata kazi, tunajaribu kufanya utaratibu wa kuwaleta watalamu zaidi kutoka nje ili kuwajengea uwezo vijana wetu.”