MZEE WA UPUPU: Walter Bwalya alivyomponza Kalusha Bwalya

KALUSHWA 'The Great Kalu' Bwalya, ni mwanasoka bora na mwenye mafanikio zaidi kuwahi kutokea Zambia.

Kama sio ile ajali ya ndege ya mwaka 1993 iliyogharimu maisha ya kikosi chote cha Zambia (kasoro yeye na Charles Musonda), basi yawezekana Zambia ingeweka historia kwenye Kombe la Dunia la 1994.

Kalusha ambaye wakati huo alikuwa akisakata kambumbu nchini Uholanzi kwenye klabu ya PSV, alikubaliana na kocha wa timu ya taifa kwamba wakutane Senegal ambako walikuwa wacheze mechi ya kufuzu Kombe la Dunia.

Yeye atoke Ulaya na wenzake watoke Zambia, lakini yeye akafika salama ila wenzake wakapata ajali wakiwa Gabon na kuangamia wote.

Charles Musonda, baba yake na Charly Musonda aliyekuwa mchezaji wa Chelsea, alikuwa majeruhi hivyo hakwenda timu ya taifa. Wakati huo alikuwa akisakata kabumbu Ubelgiji.


TURUDI KWA BWALYA

Baada ya kustaafu soka, akawa kocha wa timu ya taifa ya Zambia na baadaye Rais wa chama cha soka cha nchi hiyo, FAZ, kuanzia 2008 hadi 2016.

Katika utawala wake ndiyo Zambia ilishinda ubingwa wa AFCON 2012. Lakini licha ya mafanikio hayo, akashindwa uchaguzi wa 2016 kwa Andrew Kamnanga.

Bwalya alishindwa kwa kura 13, akipata 156 na mpinzani wake kupata 163.

Hiki kilikuwa kitu cha kushangaza sana. Gwiji kama yeye ambaye pia ameipatia nchi yake kombe kubwa walilokuwa wakilihitaji kwa miaka mingi, anakuja kushindwa uchaguzi.


NI HIVI

Mwaka 2013, mchezaji mmoja kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, aliyeitwa Freddy Tshimenga aliyejiunga na klabu ya Forest Rangers ya Ndola Zambia.

Bahati mbaya sana timu hiyo ilishuka daraja lakini yeye alikuwa sehemu ya wachezaji waliokuwa na msimu mzuri.

Ili kurudi kwenye ligi kuu, klabu hiyo ikamuomba mchezaji huyo kuwasaidia kupata wachezaji kutoka kwao (Lubumbashi) ambao wanaweza kuirudisha timu ligi kuu.

Tshimenga akawaleta wachezaji wawili; Heritier Swabwa Binene na Idris Ilunga Mbombo.

Binene akasaini Forest Rangers lakini Mbombo akakataa baada ya kuona ofa aliyopewa ilikuwa ndogo. Haikuwa ndogo kuliko makubaliano bali kuna timu nyingine ilikuja, Kabwe Warriors, na kutoka ofa kubwa zaidi.

Warriors, moja ya timu za Zambia, nayo ilikuwa kwenye wakati mgumu ikipambana kurudi ligi kuu.

Wachezaji hawa wakafanya vizuri sana na timu zao na kuzisaidia kurudi ligi kuu.

Mbombo akiwa na Warriors, alifunga mabao 36...akawa habari kubwa sana.

Timu kubwa za Zambia; Zesco, Nkana na Power Dinamo, zikaanza kupigana vikumbo kumuwania.

Rais wa Chama cha Soka cha Zambia, Kalusha Bwalya, akaona kitu kwa vijana hawa. Akataka awachukue waichezee timu ya taifa ya Zambia.

Akawaambia atawalipa pesa nyingi ili wabadili majina yao na kuchukua majina ya kizambia.

Wote wakakubali lakini wakasema wawasiliane kwanza na familia zao nyumbani. Familia ya Idris Mbombo ikakataa, lakini ya Heritier Binene ikakubali.

Binene akatoka Ndola hadi Lusaka kwenye ofisi za makao makuu ya FAZ, kukamilisha dili.

Kufika huko akapewa jina jipya la Walter Bwalya....bila shaka sasa umeshamjua!

Walter ni jina la Kiingereza ambalo katika ulimwengu wa kifaransa ndiyo Heritier. Na Bwalya ni jina la Kalusha mwenyewe...kwa hiyo alimpa jina lake.

Hiki kilikuwa kipindi cha kuelekea uchaguzi wa 2016 na habari zikavuja kwamba Kalusha anafanya udanganyifu huo.

Hapo ndipo Andrew Kamnanga., mfanyabiashara mkubwa nchini humo, alipojitosa kumng'oa Kalusha madarakani.

Akaitumia kashfa hiyo kama fimbo, na kweli ikamchapa Bwalya. Ilikuwa kashfa kwa sababu nyaraka nyingi za uraia wa wachezaji hao zilighushiwa ili waonekane raia wa kuzaliwa wa zambia, siyo wa kuhamia.

Nyaraka za hospitali, shule na kila kitu...ilikuwa kashfa kubwa sana.

Ingekuwa nchi zilizoendelea, au Kalusha asingekuwa mtu anayeheshimika kama alivyo, yawezekana angeishia jela kwa kughushi nyaraka za serikali.

Baada ya Kalusha kushindwa uchaguzi, ule mpango wa uraia wa Binene, au Walter Bwalya kwa jina lake jipya, ukakwama.

Na haikuishia tu kukwama, ilienda mbali zaidi hadi kutishia kumkamata au kupigwa marufuku kuingia nchini humo.

Bahati njema ukubwa wa Kalusha ukasaidia. Rais wa wakati huo wa Zambia, Edigar Lungu, alisimama imara kiuhakikisha Bwalya analindiwa heshima yake.

Lakini, hata hivyo nafasi yake kama Rais wa chama cha soka cha nchi ikaenda na maji.

Miaka mingi baadaye, Walter Bwalya akaitwa timu ya taifa ya DRC na kuitumikia, lakini naye jina lake la Heritier Binene likaenda na maji.

Kwa sasa Freddy Tshimenga anaitumikia klabu ya Red Arrows ya mjini Lusaka, Idris Ilunga Mbombo yupo Azam FC ya Tanzania na Walter Bwalya yuko Saudi Arabia kwenye klabu ya  Al Qadsiah, kwa mkopo akitokea Al Ahly ya Misri.