MZEE WA UPUPU: Simba sawa, lakini Pamba inaongoza Bara Kimataifa

MAADA ya ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Horoya, meneja wa habari wa Simba, Ahmed Ally, alitania mbele ya waandishi wa habari kwamba ushindi wao ni mkubwa kwenye mashindano ya CAF, ukifuatiwa na ule wa Raja Casablanca dhidi ya Yanga 1998.

Hapa Ahmed hakuwa sahihi na wala hakuwa akimaanisha, bali alikuwa akiwatania watani wao wa jadi, Yanga SC. Ushindi mkubwa kama ule hauwezi kukamilika bila kuwatupia dongo watani kidogo. Simba hata ichukue ubingwa wa Afrika kwa kuwafunga Al Ahly 10-0, lakini mateso yataenda Jangwani kwa Yanga wala sio Cairo...na hata Yanga itakuwa vivyo hivyo. Huo ndiyo utani ulivyo!

Lakini ukiweka utani pembeni na ukaanza kuangalia takwimu na rekodi, utaona timu ya Pamba ya Mwanza bado inaongoza Tanzania kwa kupata ushindi mkubwa kwenye mashindano ya CAF.

Ushindi wa mabao 12-1 dhidi ya Anse-aux-Pins FC ya Shelisheli mwaka 1990, unabaki kuwa mkubwa zaidi kwa timu za Tanzania kimataifa. Pia ushindi huo wakati unapatikana ulikuwa rekodi ya Afrika, hadi mwaka 1994 ulipopigwa kikumbo.

Kwa ujumla Pamba ilishinda mabao 17-1 kufuatia ushindi 5-0 ugenini mjini Victoria. Ushindi huu wa jumla unabaki kuwa rekodi kwa mashindano yote ya CAF, siyo tu kwa Tanzania bali Afrika nzima.

Kwa hiyo ushindi wa Simba wa mabao 7-0 siyo mkubwa zaidi kama alivyosema Ahmed Ally lakini ni mkubwa zaidi katika hatua ya makundi kwa timu za Tanzania.

Kushinda 7-0 kwenye hatua ya makundi tena dhidi ya timu ambayo imezoea kucheza hatua hii ni jambo lisilo la kawaida.

Ifuatayo ni orodha ya 10 bora ya ushindi mkubwa kwa timu za Tanzania kwenye mashindano ya Afrika


1. PAMBA 12-1 ANSE-AUX-PINS FC - KOMBE LA WASHINDI 1990

Kombe la Washindi yalikuwa mashindano ya CAF kwa klabu za Afrika ambazo ni mabingwa wa Kombe la FA kwenye nchi zao. Kwa Tanzania, Kombe la FA lilikuwa likiitwa Kombe la Nyerere ambalo kwa sasa ndiyo Kombe la Shirikisho la Azam Sports.

Kombe la Washindi Afrika lilianza mwaka 1975, na ili kupata wawakilishi, Tanzania ikaanzisha mashindano ya Kombe la Nyerere mwaka 1974.

Mwaka 2003 CAF iliyafuta mash-indano hayo kwa kuyaunganisha na Kombe la CAF ambalolilianza 1992, na kuzali-wa mashindano ya Kombe la Shirikisho yanayoendelea hadi sasa.

Februari 18, 1990 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Pamba ambayo ilishiriki Kombe la Washindi kama mabingwa wa Kombe la Nyerere mwaka 1989 ilifanya mauaji ya kihistoria.

Ikiwa chini ya kocha Pius Nyamko akisaidiwa na Muhsin Maftah (wote marehemu) iliweka rekodi ya Afrika ambayo iliendelea kudumu hadi 1994 ilipokuja kuvunjwa na klabu ya Mbilinga ya Gabon iliyoicharaza Renaissance ya Chad kwa mabao 13-0.


2. TANZANITE STARS  10-0 MSUMBIJI KUFUZU KOMBE LA DUNIA 2014

Mwaka 2013, timu ya taifa ya Tanzania ya wanawake chini ya miaka 20, Tanzanite Stars iliwafunga wenzao wa Msumbiji 10-0 kwenye harakati za kufuzu Kombe la Dunia la 2014.


3. YANGA 8-1 ETOILE D'OR -LIGI YA MABINGWA 2009

Boniface Ambani akiwa kwenye ubora wake, aliiongoza Yanga kushinda 8-1 nyumbani huku yeye akifunga mabao manne. Huu ulikuwa mchezo wa mkondo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya ligi ya mabingwa Afrika.


4. YANGA 7-0 KOMOROZINE - LIGI YA MABINGWA AFRIKA 2014

Februari 8, 2014, klabu ya Yanga ilirekodi ushindi mwingine mkubwa kwenye mashindano ya Afrika pale ilipoifunga Komorozine ya Comoro mabao 7-0 uwanja wa Mkapa kwenye mchezo wa raundi ya awali.

Msimu huu utakumbukwa kwa mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa kufunga hat trick mbili dhidi ya Wacomoro hao; moja kwenye mchezo wa kwanza na nyingine kwenye mchezo wa marudiano.

Hat-trick hizo mbili zikamfanya Ngassa awe na mabao sita na kuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika, akilingana na wengine watatu El Hedi Belameiri wa ES Setif ya Algeria, Haythem Jouini wa Esperance ya Tunisia na Ndombe Mubele wa AS Vita ya DRC.

Miaka michache baadaye CAF ikafuta utaratibu wa kuhesabia mabao ya raundi za mchujo kabla ya hatua ya makundi kwenye orodha ya kuwania mfungaji bora wa mashindano ya klabu.


5. SIMBA 7-0 HOROYA - LIGI YA MABINGWA AFRIKA 2022/23

Huu ndiyo ushindi uliosababisha makala hii. Simba wakiwa kwenye windo la robo fainali walifanya kisichotarajiwa kwa kuwachapa Horoya, moja ya timu zilizozoeleka kwenye hatua ya makundi.

Wakiongozwa na mzaliwa wa mji mdogo wa Nchanga aliyeamua kuweka makazi yake mjini Ndola, ambaye Tanzania inamfahamu kama Mwamba wa Lusaka kimakosa, Clatous Chama, Simba walikuwa katika ubora wa hali ya juu sana.

Ushindi wa Simba ni wa pili kwa ukubwa ukilingana na ule wa Asec Mimosas dhidi ya CR Belouizdad mwaka 2001, kwenye hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Afrika.

TP Mazembe ya DRC inaongoza kwa ushindi wake wa 8-0 dhidi ya Club Africaine ya Tunisia, mwaka 2019, katika siku ambayo Simba ilifungwa 5-0 na Al Ahly.


6. ETOILE D'OR  0-6 YANGA-LIGI YA MABINGWA AFRIKA 2009

Baada ya ushindi wa 8-1 nyumbani, Yanga wakenda kushinda 6-0 ugenini kwenye mchezo wa marudiano, huku Mrisho Ngassa akifunga mabao matatu, katika moja ya rekodi za kushangaza. Katika mchezo wa kwanza, Ngassa alifunga bao moja na Ambani kufunga manne, safari hii Ngassa alifunga matatu na Ambani moja.


7. D’AGOSTO 2-6 NAMUNGO- KOMBE LA SHIRIKISHO 2021

Ikishiriki kwa mara ya kwanza mashindano ya kimataifa, Namungo ilitumia vizuri uwanja wa nyumbani uliokuwa ugenini kikanuni kushinda 6-2 dhidi ya timu ngumu ya D’Agosto ya Angola.

Huu ulikuwa wakati wa mlipuko wa Uviko-19 na nchi nyingi zilikuwa na sheria ngumu ikiwemo Angola. Kutokana na matatizo ambayo Namungo walikutana nayo ugenini hadi mchezo kushindwa kufanyika, CAF iliamua mechi zzote mbili zifanyike Tanzania na huu ukawa mchezo wa kwanza ambao Namungo walihesabisabika kuwa ugenini.


8. MUFULIRA WANDERERS 0-5 SIMBA - KLABU BINGWA1979

Huu ni moja ya ushindi wa kushangaza zaidi kwenye historia ya soka duniani. Simba waliingia kwenye mchezo huu wa ugenini wakitoka kupoteza 4-0 nyumbani.

Lakini katika hali ya kushangaza, walipindua matokeo mjini Ndola na kushinda 5-0 hivyo kusonga mbele katika raundi ya pili.

Ni bahati mbaya sana kwamba katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili dhidi ya Raccah Rovers ya Nigeria mjini Dar es Salaam mchezaji mmoja wa Simba, Hussein Tindwa, alianguka uwanjani na kupoteza maisha.


9. ANSE-AUX-PINS FC 0-5 PAMBA - KOMBE LA USHINDI 1990

Huu ulikuwa mchezo wa ugenini baada ya kuwa tumeshanda huko namna Pamba ilivyoshinda 12-1 katika uwanja wa nyumbani.


10. Al NASSIR 0-5 AZAM FC - KOMBE LA SHIRIKISHO 2013

Baada ya kushinda 3-1 nyumbani, Azam FC walienda ugeniniSudan Kusini kurudiana na Al Nassir na kushinda 5-0 mjini Juba. Yote kwa yote, ushindi wa Simba wa 7-0 dhidi ya Horoya unafuta machozi ya vichapo klabu hiyo ya Msimbazi imevipata kwa siku za hivi karibuni kwenye mashindano ya Afrika


AS Vita 5-0 Simba - Ligi ya Mabingwa 2019, AL Ahly 5-0 Simba - Ligi ya Mabingwa 2019, Kaizer Chiefs 4-0 Simba - Ligi ya Mabingwa 2021

Lakini zaidi ni vile vipigo vya kuumiza dhidi ya UD Songo na Jwaneng Glaxy katika uwanja wa nyumbani. Japo vipigo vile haviingii kwenye orodha ya vipigo vikubwa, lakini ni vipimo vyenye kuumiza zaidi kwa sababu hakuna aliyetarajia kutokea e yaliyotokea, tena kwa Mkapa.