Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MZEE WA FACT: Afrika sasa iwe na dirisha moja la usajili

Muktasari:

  • Wakati Rais wa nchi akiwa katika pilika pilika zote hizo, kuna rais mwingine kutoka ardhi hii adhimu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naye pia alikuwa kwenye pilikapilika.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alikuwa na ratiba ngumu sana mwishoni mwa Januari.

Aliongoza mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati uliofanyika Dar es Salaam.

Baada ya mkutano huo akakutana katika hafla ya chakula cha mchana na washiriki wa uokoaji kwenye jengo lililoanguka Kariakoo, katikati ya Novemba mwaka jana.

Huku hisia za watu zikirudi hadi Novemba wakati wa ajali ile, likatokea janga jingine kwa jengo la TRA kuungua moto hukohuko Kariakoo.

Wakati Rais wa nchi akiwa katika pilika pilika zote hizo, kuna rais mwingine kutoka ardhi hii adhimu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naye pia alikuwa kwenye pilikapilika.

Huyo ni mhandishi Hersi Said, ambaye ni Rais wa Chama cha Vilabu vya Soka Afrika, ACA.

Kiongozi huyu ni pia ni Rais wa klabu ya Yanga,  alikuwa na pilika pilika nyingi huko Morocco kwenye Mkutano wa Kamati Tendaji wa CAF, kuhakikisha soka la Afrika linapiga hatua.

Moja ya mambo yaliyofanyika huko ni kuondoa sheria ya CUP-TIED RULE.

Hii ni sheria iliyokuwa inazuia wachezaji waliosajiliwa dirisha dogo kuzichezea timu zao mpya kwenye mashindano ya CAF endapo walishacheza mashindano hayo wakiwa na timu zao za zamani.

Sheria hii ingepita mapema basi timu ya kwanza kufaidika nayo hapa nchini basi ingekuwa Yanga na mchezaji wao mpya kutoka DRC, Jonathan Ikangalombo Kapela.

Mchezaji huyo kutoka AS Vita Club ya Kinshasa, aliukosa mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya MC Alger kutokana na kubanwa na sheria hiyo.

Kwa hiyo kuanzia sasa sheria hiyo haipo na mchezaji wa dirisha dogo anaruhusiwa kuichezea timu yake mpya kwenye mashindano yoyote ya CAF hata kama alishacheza kwenye timu yake ya zamani.

Hongera nyingi sana CAF kwa kulifanyia kazi jambo hilo na kama ambavyo imesikika hapa nchini kwamba mhandisi Hersi Said amehusika kwa asilimia kubwa kufanikisha hilo kama mwenyekiti wa vilabu, hongera pia kwake.

Lakini hata hivyo, tusiishie hapo. Tatizo la usajili Afrika halikuwa hilo tu, bali pia vipindi vya usajili.

Kila nchi barani Afrika ina kipindi chake cha usajili kinachofahamika kama dirisha la usajili.

Kwa mfano, dirisha la usajili ya Tanzania lilifunguliwa Desemba 15, 2024 na kufungwa Januari 15, 2025.

Dirisha la usajili la majirani zetu Kenya limefunguliwa Januari 31, 2025 na litafungwa Februari 28, 2025.

Kwa hiyo timu ya Kenya ikija Tanzania kumnunua mchezaji maana yake timu ya Tanzania itashindwa kuziba pengo lake.

Hiki ndicho kinachokwenda kutokea Yanga, kama itakuwa kama inavyozungumzwa.

Klabu ya Al Ittihad ya Libya inataka kuwanunua nyota wawili, Aziz Ki na Clement Mzize.

Inasemekana Waarabu hao wameweka ofa kubwa ambayo Yanga wameshindwa kuikataa.

Sasa kama kweli itakuwa hivyo maana yake Yanga watashindwa kuziba nafasi zao...itakuwaje?

Afrika tunahitaji kuwa na dirisha moja la usajili kwa nchi zote ili linapofunguliwa wote wanasajili na kuziba mapengo.

Hivi ndivyo wanavyofanya wenzetu ambao tumekuwa tukiwaiga vitu vingi vizuri, kama kuondoa ile sheria, basi tuige na hili.

Kama kweli mhandisi Hersi alihusika na kubadilisha sheria ya CUP-TIED RULE,  basi afanye jambo na hapa.

Kama alihusika kwa sababu aliathirika na sheria ile kwa kuwa ilimzuia mchezaji wao mpya Jonathan Ikangalombo Kapela, basi waathirike tena kwa kuwakosa Ki na Mzize ili ahusike na kwenye hili.

Afrika inahitaji kuunganisha mpira wake kwa nyanja zote ili biashara ifanyike bila shida.

Kuna vitu vingi sana havijakaa sawa kwenye mpira wetu, yakiwemo mambo yaliyo nje ya uwezo wetu sisi kama watu wa mpira, kama usafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine.

Timu za kutoka Afrika Mashariki haziwezi kwenda moja kwa moja Afrika Kaskazini kama Morocco au Tunisia ni hadi ziende Ulaya ua Asia.

Lakini hili halipo ndani ya uwezo wa Hersi wala CAF wenyewe ni juu ya uwezo wao.

Ila haya mambo mengine yapo ndani ya uwezo wao moja kwa moja, ni suala tu la utashi.

Kwa mfano mashindano makubwa ya mataifa ya Afrika kuchezwa Januari, hili jambo bado linatakuwa kuangaliwa zaidi na zaidi.

AFCON ya mwaka huu itaanza Desemba 21 kwa wenyeji Morocco kufungua Dimba na Comoro.

CHAN ilipangwa kuanza leo, Februari 3, kama siyo kubadilishwa ratiba kutokana na kuchelewa kwa maandalizi ya wenyeji.

Desemba, Januari na Februari ni kipindi cha katikati ya nisimu ya soka duniani kote, kuweka mashindano kama AFCON katika wakati huu ni kutengeneza migogoro na vilabu duniani.

Wachezaji wa Afrika wanasajiliwa na klabu za Ulaya kwa mfano na wanategemewa.

Wakati misimu yao inachanganya huku wakiwategemea wachezaji kutoka Afrika, utasikia AFCON inakuja na wanaondoka...vilabu vinaathirika.

Matokeo yake baadhi ya vilabu husita kusajili wachezaji wa Afrika kwa kuhofia kuwakosa kila baada ya Januari moja.

Mivutano kati ya  CAF na vilabu vya Ulaya imekuua ikijirudia kila wakati lakini Afrika bado haitaki kubadili utaratibu.

Zaidi ya kuvutana na vilabu vya Ulaya, pia ratiba za ligi za Afrika zinavurugika sana na mashindano makubwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka.

Hebu fikiria ligi ya Tanzania ilitakiwa kurudi Machi baada ya mechi za Desemba endapo CHAN ingefanyika Februari.

Januari na Februari zingepita wima wima, mambo gani haya.

Kwa hiyo wakati tunawapongeza CAF kwa kufanikisha jambo moja, tuwakumbushe na mengine kama haya.

UEFA kwa mfano, waliiondoa sheria ya CUP-TIE RULE tangu mwaka 2018 kwa maana kwamba sheria mpya ikaanza kutumika msimu wa 2018/19.

Wachezaji wa kwanza kufaidika na sheria hii walikuwa wale waliosajiliwa dirisha dogo la Januari 2019 na timu zilizotinga hatua ya 16 bora.

Mmojawapo ni Frenkie de Jong aliyejiunga na Barcelona akitokea Ajax ambako alishacheza hatua ya makundi.

Kama ambavyo Jonathan Ikangalombo Kapela wa Yanga amekuwa mmoja wa wachezaji wa mwisho kubanwa na sheria hii, Philippe Coutinho naye ni mmoja wa wachezaji wa mwisho kubanwa na sheria hii barani Ulaya.

Alisajiliwa na FC Barcelona kutokea Liverpool ambako alishacheza hatua za awali.

Mmoja wa wachezaji waliokatiliwa vibaya na sheria ya CUP-TIED RULE ni El Phenomenon,  Ronaldo de Lima wa Brazil.

Mwaka 2007, aliununua mkataba wake na Real Madrid ili ahamie AC Milan ya Italia.

Lakini alihama akiwa ameshacheza mechi za awali za Ligi ya Mabingwa na Real Madrid hivyo akashindwa kuichezea AC Milan kwenye mashindano hayo.

AC Milan ikabeba ubingwa wa Ulaya huku yeye akiwa hahusiki na ndiyo kombe pekee ambalo hakuwahi kushinda.

UEFA pia waliondoa sheria la goli la ugenini kuanzia msimu wa 2021/22. CAF bado wanayo.

Nadhani kidogo kidogo sheria zitabadilika kurahisisha mchezo na kuufanya uwe bora zaidi.

Kwa pamoja tuujenge mpira wetu Afrika!