Mwamnyeto… Mlima wake Yanga na nini cha kufanya
Muktasari:
- Akisifika kwa urefu wake wa futi 6.1, nguvu ya mwili, na uwezo wa uongozi, Mwamnyeto amekuwa mhimili wa safu ya ulinzi na ameiongoza Yanga kutwaa makombe 11, akivunja rekodi za manahodha waliomtangulia.
BAKARI Mwamnyeto, amekuwa beki wa kiwango cha juu katika soka la Tanzania, akiandika historia kubwa ndani ya Yanga SC tangu Agosti 2020 alipojiunga akitokea Coastal Union ya Tanga kwa zaidi ya Sh200 milioni.
Akisifika kwa urefu wake wa futi 6.1, nguvu ya mwili, na uwezo wa uongozi, Mwamnyeto amekuwa mhimili wa safu ya ulinzi na ameiongoza Yanga kutwaa makombe 11, akivunja rekodi za manahodha waliomtangulia.
Hadi sasa katika kabati la Mwamnyeto ana makombe ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho, Ngao ya Jamii, Kombe la Mapinduzi na Toyota Super Cup alilolibeba Afrika Kusini wakati wa maandalizi ya kujiandaa na msimu.
Mwamnyeto amebeba mataji hayo na matatu ni ya ligi kuu, matatu ya Kombe la Shirikisho na Ngao tatu. Beki huyo amebeba Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho kwa misimu mitatu mfululizo kuanzia msimu wa 2021/22 hadi msimu uliopita wa 2023/24.
Pia nahodha huyo aliiongoza klabu hiyo kubeba ubingwa wa Kombe la Mapinduzi mwaka 2021 Zanzibar baada ya kuwafunga Simba kwenye penalti 4-3.
Usisahau beki huyo ambaye ni mwenyeji wa mkoa wa Tanga ameshinda Ngao mbili za Jamii katika mwaka 2021 na 2022 ambazo zote waliwafunga watani zao Simba kwa bao 1-0 na 2-1.
Katika mechi hizo mabao ya Yanga yote yalifungwa na straika Mkongomani, Fiston Mayele ambaye kwa sasa yuko Misri katika klabu ya Pyramid.
Pia Ramos huyo wa Bongo amebeba Ngao ya Jamii manzoni mwa msimu huu kwa kuichapa Azam FC kwa mabao 4-1 katila mchezo wa fainali kama ambavyo waliwafanyia Wasauzi, Kaizer Chiefs katika kombe maalumu la michuano ya kujiandaa na msimu la Toyota Cup.
Hata hivyo, mabadiliko ya kiufundi na ushi-ndani mkali kutoka kwa mabeki wenzake, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ futi 5.9 na Dickson Job futi 5.6 yameathiri nafasi yake katika kikosi cha kwanza. Hivi sasa Mwamnyeto amejikuta akitumiwa mara chache hususan katika mechi ambazo Job au Bacca hawapo.
Hali hii imeibua maswali juu ya nafasi yake, lakini kutokana na historia yake na uzoefu, bado ana uwezo mkubwa wa kurudi kwenye chati. Katika makala haya tunaangazia hatua za msingi ambazo Mwamnyeto anaweza kuchukua kurejea katika kikosi cha kwanza cha Yanga.
KIUFUNDI NA KIMWILI
Moja ya changamoto kubwa inayomkabili Mwamnyeto ni kasi ya mchezo wa kisasa na uwezo wa wachezaji wapinzani kuendesha mashambulizi ya haraka. Kwa sasa, Job na Bacca wameonyesha uwezo bora wa kukabiliana na changamoto hizi. Ili Mwamnyeto kushindana na mabeki hawa, ni muhimu ajitathmini kwa kina kuhusu uwezo wake wa sasa kiufundi na kimwili, na kuboresha maeneo yenye upungufu.
Kasi ni moja ya sifa muhimu kwa mabeki wa kisasa. Mwamnyeto anaweza kufaidika na mazoezi maalum ya kuimarisha kasi, kama vile, kufanya mbio fupi kwa kurudiarudia katika maeneo tofauti.
Mfano mzuri ni Virgil van Dijk wa Liverpool, licha ya kuwa na mwili mkubwa kama Mwamnyeto, aliboresha kasi yake kupitia mazoezi ya namna hiyo aliwahi kueleza katika moja ya mahojiano yake.
Jambo lingine muhimu kwa Mwamnyeto ni Stamina, kwa nini? mara nyingi inamwezesha beki kucheza kwa kiwango cha juu kwa dakika zote 90. Mwamnyeto anaweza kufanya mazoezi ya ‘endurance’ kama vile kukimbiea kwa muda mrefu kwa kwa kasi ndogo (long-distance running). Kufanya mazoezi ya mchanganyiko wa kasi (interval training) ili kuimarisha uwezo wa mwili.
UPUNGUFU WA KIMCHEZO
Mwamnyeto ana sifa ya kuwa kiongozi imara, lakini anatakiwa kuboresha maeneo ya kiufundi ambayo yanaweza kuwa yanamrudisha nyuma:
Mabeki wa kisasa wanatakiwa kuwa na uwezo wa kuanzisha mashambulizi kwa kupiga pasi sahihi kutoka nyuma. Mwamnyeto anaweza kuboresha hili kwa kufanya mazoezi ya kupiga pasi za mbali na za haraka kwa usahihi, akishirikiana na viungo wa timu.
Katika hili mfano mzuri ni Gerard Piqué wakati akiwa Barcelona alikuwa akitumia uwezo wake wa kupiga pasi kuanzisha mashambulizi, jambo lililomfanya kuwa tegemeo licha ya mwendo wake wa taratibu uwanjani yani hakuwa na kasi.
Job na Bacca wanaonekana kufanikiwa katika kukabiliana na wachezaji wenye kasi kupitia mbinu bora za kukaba. Mwamnyeto anatakiwa kufanyia kazi jinsi ya kupunguza nafasi za wapinzani bila kufanya madhambi, kuboresha uwezo wa kushinda mipira ya juu kwa kutumia vyema urefu wake.
MAHITAJI YA MIFUMO
Kocha mpya wa Yanga, Sead Ramovic, anaweza kuwa msaada mkubwa kwa Mwamnyeto ikiwa beki huyo ataonyesha uwezo wa kuendana na mifumo tofauti ya kiufundi.
Mfumo wa Mabeki Watatu (3-5-2), mara nyingi unahitaji mabeki wa kati wenye nguvu na umakini wa juu. Mwamnyeto anaweza kushirikiana vizuri na Job na Bacca katika mfumo huu, kama ilivyokuwa dhidi ya Mamelodi Sundowns msimu uliopita.
Katika mfumo wa Mabeki Wawili wa kati (4-4-2), Mwamnyeto anaweza kushirikiana na mmoja kati ya Job au Bacca, hasa katika mechi ambazo zinahitaji uzoefu wa kukabiliana na mashambulizi ya wapinzani wenye nguvu.
UZOEFU NA HESHIMA YAKE
Mwamnyeto bado ana nafasi ya kutumia uzoefu na nafasi yake kama nahodha wa Yanga ili kurejea kwenye kikosi cha kwanza.
Moja kwa kuimarisha morali ya wachezaji wenzake. Hata akiwa benchi, Mwamnyeto anaweza kuonyesha uongozi wake kwa kuwapa morali wachezaji chipukizi na kushiriki kikamilifu katika mazoezi ya timu.
Kufanya Kazi Kwa Bidii Mazoezini. Wakati mwingine, juhudi na nidhamu zinaweza kumshawishi kocha zaidi ya vipaji pekee. Mwamnyeto anatakiwa aonyeshe bidii ya hali ya juu mazoezini, akionyesha kuwa bado ana uwezo wa kuchangia kikosi.
MECHI NDOGO
Mashindano Kombe la Mapinduzi, Kombe la FA au mechi za kirafiki ni fursa kwa Mwamnyeto kuonyesha uwezo wake na kushindana kwa nafasi. Mfano mzuri katika hili ni Sergio Ramos, hata alipokuwa akikosa nafasi Real Madrid, alitumia mashindano madogo kuthibitisha thamani yake kwa timu kabla ya kuachana na matajiri hao wa Hispania japo uwezo wa ushindani wa beki huyo katika nyakati zake za mwisho ulidhoofishwa na majeraha.
Mwamnyeto ni mmoja wa wachezaji wenye mafanikio makubwa ndani ya Yanga SC na Tanzania kwa ujumla. Licha ya kupoteza nafasi ya kuanza mara kwa mara, hii haimaanishi kuwa safari yake imefika mwisho.
Kwa kujitathmini, kurekebisha upungufu wake, kuendana na mifumo ya kisasa, na kutumia uzoefu wake, anaweza kurejea kwa nguvu kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga. Kwa umri wa miaka 29, bado ana miaka kadhaa ya kung’ara, na mashabiki wa Yanga anapaswa kuwa na matumaini kwamba Ramos wa Bongo bado ana mengi ya kutoa.
WASIKIE WADAU
Aliyewahi kuwa kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm alieleza Mwamnyeto ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa, lakini kwa sasa anakabiliana na changamoto ya ushindani wa nafasi ambayo anapaswa kuishinda.
“Mwamnyeto ana kila sifa ya kuwa beki wa kiwango cha juu. Hata hivyo, anahitaji kuboresha uwezo wake. Katika soka la kisasa, mabeki wa kati wanatakiwa kuwa sehemu muhimu ya uanzishaji wa mashambulizi. Nampa ushauri wa kupambana na kuhakikisha anakuwa kwenye mipango ya kocha mpya.”
Hans aliongeza kuwa Mwamnyeto anaweza kufaidika sana na mazoezi ya kutathmini uwezo wake binafsi, kama vile mbinu za kushinda mipira ya juu, kutumia vizuri urefu wake, na kujifunza kutoka kwa mabeki wengine.
Kwa upande wake, kocha wa zamani wa Gwambina na Mtibwa Sugar, Mohammed Badru alimsifu Mwamnyeto kwa uwezo wake wa uongozi na uzoefu mkubwa uwanjani lakini akasisitiza kuwa anatakiwa kurejesha nafasi yake kwa njia ya kujituma zaidi.
“Uzoefu wa Mwamnyeto ni silaha kubwa, lakini katika hali ya sasa anatakiwa kuonyesha kiwango kikubwa mazoezini na kwenye mechi ambazo anapata nafasi. Ushindani ndani ya Yanga ni mkali.”
Badru aliongeza kuwa; “Mwamnyeto anahitaji kuimarisha uwezo wake wa kupiga pasi sahihi na haraka. Anaweza pia kufanyia kazi uamuzi wake wa wakati, hasa linapokuja suala la kukabiliana na mashambulizi ya ghafla. Katika soka, heshima na nafasi zinashindaniwa kila siku, na ninahisi ana nafasi ya kurejea ikiwa ataweka juhudi zaidi.”