Prime
Muvi nzima ya Aisha Mnunka Simba

Muktasari:
- Agosti Mosi, mwaka huu, Mwanaspoti iliripoti nyota huyo wa timu ya taifa (Twiga Stars) ametoroka kambini ikiwa ni siku chache tangu atoke kwenye majukumu ya taifa.
HATIMAYE ile muvi ya mshambuliaji wa Simba Queens imemalizika baada ya mchezaji huyo kukubali yaishe na kurudi unyamani.
Agosti Mosi, mwaka huu, Mwanaspoti iliripoti nyota huyo wa timu ya taifa (Twiga Stars) ametoroka kambini ikiwa ni siku chache tangu atoke kwenye majukumu ya taifa.
Inaelezwa hadi sasa nyota huyo yuko kambini na wenzake kujiandaa na Ligi itakayoendelea Januari 21 baada ya kikao cha mwisho cha Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji.
Mwanaspoti ambayo tangu mwanzo iliripoti jambo hilo imekuchambulia muvi nzima ilivyoanza hadi kutamatika.

KUTOROKA KAMBINI
Picha lilianza Agosti mwaka jana baada ya Mnunka kumaliza majukumu ya timu ya taifa, Twiga Stars, na alipaswa kurejea kambini lakini hakuonekana.
Simba ilikuwa inajiandaa na michuano ya CECAFA kwa wanawake ambayo ilikuwa inachezwa Addis Ababa nchini Ethiopia.

Ndani ya wiki moja ambayo Simba ilikuwa kwenye maandalizi nyota huyo hakutokea na hata simu yake ikipigwa haikupatikana.
Baada ya kufika Ethiopia viongozi wa Simba kupitia kwa mratibu wake, Selemani Makanya walitangaza nyota huyo bado hajaonekana.

KUFICHWA NA TIMU
Mwanaspoti ilifahamu moja ya sababu za Mnunka kutoroka kambini ni moja ya timu iliyopanda daraja ilimsajili kimya kimya.
Mbali na kumsajili alifanya mazoezi na timu hiyo iliyompa ahadi ya kumnunulia nyumba ya kuishi, gari pamoja na simu nzuri ya kutumia, ambavyo vyote mchezaji aliridhia.
Hata hivyo, ahadi hiyo haikutimia kwani mmoja wa kiongozi wa timu hiyo aliliambia Mwanaspoti kuwa wanapitia kipindi kigumu cha ukata hivyo wameshindwa kumpa mahitaji hayo.
Baada ya Mnunka kukaa kambini kwa takribani miezi mitano akifanya mazoezi nao, mshambuliaji huyo akauomba uongozi huo aondoke baada ya mambo kuwa magumu.

JUHUDI ZA SIMBA
Sasa baada ya kutangaza kwa umma kwamba nyota huyo bado hajaaonekana na wenzake, Simba ikaanza kumtafuta kupitia mawasiliano yake ya simu lakini nayo haikufua dafu kwani alizima.
Simba haikuishia hapo, iliendeleza juhudi za kumtafuta meneja wa mchezaji huyo ambaye naye pia hakuwa anapatikana ndipo ikakimbilia TFF kushtaki.
Agosti 19 Mabingwa hao watetezi wa Ligi ya Wanawake, Simba Queens wakatangaza kuwa wamepeleka barua kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kushtaki juu ya utoro wa nyota wake huyo.

KAMATI YAMALIZA KAZI
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa kwa mara ya kwanza Desemba 12 kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kupitia Mwenyekiti wake, Said Soud.
Baada ya kusikilizwa Mwenyekiti Soud aliamuru pande zote mbili zikae mezani na kumalizana juu ya sakata hilo.
Na baada ya kikao hicho kilichofanyika TFF Karume jijini Dar es Salaam baadhi ya viongozi wa Simba walionekana kuridhia mazungumzo na mchezaji wao.
“Sisi Simba tulikuwa walalamikaji na upande wa mchezaji wameomba tukae tuzungumze hivyo kamati imetoa nafasi kwao tujadili kwa pamoja,” alisema mmoja wa viongozi wa Simba ambaye hakutaka jina litajwe
Uamuzi uliofanywa na kamati umemfanya Mnunka kukubali yaishe na kurudi kambini kumalizia mkataba wake unaotamatika mwishoni mwa msimu huu. Ishu iliyobaki ni kuona kama straika huyo wa mabao kama ataongeza mkataba ama ataondoka bure.