Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mustafa mdaka mishale wa Azam FC anautaka ubingwa Bara

MABOSI wa Azam FC hawakuwa na namna iliwabidi tu kuingia sokoni wakati wa dirisha dogo la usajili na kumvuta, Mohamed Mustafa kutoka Al-Merrikh SC ya Sudan kutokana na makipa wao chaguo la kwanza na la pili, Abdulai Iddrisu na Ali Ahamada kukumbwa na majeraha ambayo yatawaweka nje kwa kipindi kirefu.

Licha ya makipa hao kuondolewa kwenye usajili wa wachezaji wa Azam FC kutokana na majeraha, wataendelea kuwa chini ya timu hiyo huku wakiuguza majeraha yao pamoja na kwamba awali kulikuwa na tetesi huenda wakaachwa, hivyo baada ya kupona ndipo watakaa chini na waajiri wao ili kuona mustakabali wao.

Kuumia kwa wachezaji hao imekuwa fursa kwa Mustafa ambaye amesajiliwa kwa mkopo wa miezi sita, kipa huyo mwenye shauku ya kuanza kutumika kwenye michezo mbalimbali ya ushindani, ameongea na Mwanaspoti na kufichua anatamani kusajiliwa jumla baada ya muda wake wa mkopo kumalizika.

Mustafa amenogewa na maisha ya Tanzania, anaamini kupitia uzoefu alionao atakuwa msaada kwa timu hiyo kuhakikisha inafikia malengo iliyojiwekea.

“Nimepokewa vizuri sana na kupewa ushirikiano mkubwa na benchi la ufundi na wachezaji wenzangu na ninafuraha kuwa hapa kwa sababu Azam ni miongoni mwa klabu kubwa Tanzania, nimekuwa hapa kwa kipindi kifupi lakini Mwenyezi Mungu akipenda tutakuwa pamoja kwa kipindi kirefu zaidi,” anasema.


NI NADO, MANYAMA

Mustafa mwenye uwezo wa kuongea maneno machache ya Kiswahili, amewataja wachezaji wenzake Iddy Seleman ‘Nado’ na Edward Manyama ndio walimu wake na wamekuwa wakimfundisha kila siku maneno mapya wakiwa mazoezini.

“Hao ni wachezaji wachangamfu wamekuwa wakinitania na kunifanya kuhisi ni kama nipo nyumbani vile, wamekuwa wakinifundisha maneno ya Kiswahili, kwa sasa najua namna ya kusalimia, naamini nitajua zaidi kukiongea,” anasema. 

Kipa huyo mwenye miaka 28, ana uwezo mzuri wa kuongea Kiarabu maana ndio lugha ambayo imekuwa ikitumika zaidi Sudan ambako amezaliwa na kukulia na kucheza soka la kulipwa kwa miaka mingi akiwa na Al-Merrikh SC pamoja na Al-Ahli Atbara.


MIHOGO MITAMU

Mustafa ameshindwa kuficha miongoni mwa vyakula ambavyo tangu atue nchini amekuwa akipenda kula hata mara mbili kwa siku ni pamoja na mihogo.

“Napenda sana mihogo, nimekuwa nikitoka nje ili kuhakikisha napata hicho chakula, nimekuwa nikikila mara mbili kwa siku, hata nyumbani kwetu Sudan mihogo ipo lakini imekuwa ikitengenezwa kwa aina tofauti na huku, kule imekuwa ikipikwa kabisa na kuchanganywa na viungo vingine, ni mitamu balaa,” anasema.


SOKA LA BONGO

Kwa vipindi tofauti Mustafa anasema amewahi kuja Bongo na kucheza dhidi ya timu ya taifa ya Tanzania na dhidi ya Yanga kwenye michuano ya kimataifa.

“Najua mashabiki waTanzania wanapenda sana soka, nimeona hilo kwenye michezo yote miwili niliyokuja hapa, hii ni nchi nzuri ambayo soka lake limekuwa likikua kwa kasi sana,” anasema na kuongeza;

“Kucheza ligi ya Tanzania ni kitu ambacho nakisubiri kwa hamu kwa sababu ni ligi yenye ushindani na mvuto mkubwa kwa Afrika Mashariki, kuhusu presha ya mechi kubwa hata nikiwa Sudan nimezicheza sana kwa hiyo sidhani kama kutakuwa na kipya lakini nipo tayari kwa ajili ya kupata uzoefu mpya kwenye soka la Tanzania.”


ANAUTAKA UBINGWA

“Ninashauku ya kutwaa mataji nikiwa na Azam FC na kwa bahati nzuri nimeikuta timu ikiwa kwenye uelekeo mzuri, hivyo kama mchezaji mpya nawajibika kuongeza thamani kwenye kikosi na ndio sababu ya kusajiliwa kwangu ili kuwa sehemu ya mafanikio ya timu, nitajitoa kwa kadiri niwezavyo,” anasema na kuongeza;

“Najua sio kazi nyepesi kutwaa ubingwa kutokana na ushindani uliopo, lakini naamini tutafanikisha hilo kama timu, itakuwa fahari kwangu na kumbukumbu nzuri kwenye maisha yangu ya soka kama nitafanikisha hilo.”


SIMBA, YANGA

Mustafa ameziongelea Simba na Yanga kama timu kubwa na zenye historia ya aina yake kwenye soka la Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki lakini yeye yupo hapa kwa ajili ya Azam, hivyo anawachukulia kama wapinzani wake kwa sasa.

“Ni timu kongwe lakini soka siku hizi halipo hivyo, ubora umekuwa na nafasi kubwa zaidi ya ukongwe, naamini timu yangu ni bora na ndio maana nimeikuta ikiongoza msimamo wa ligi,” anasema kipa huyo wa kimataifa kutoka Sudan.