MTU WA PWANI: Miguu ya Diarra inawapa somo makipa wetu

Muktasari:

JIONI ya Septemba 25 mwaka huu kipa Djigui Diarra wa Yanga aliwapa darasa wachezaji wa Simba juu ya madhara ya kujisahau pindi mpira unapokuwa mikononi mwa kipa wa timu pinzani.

JIONI ya Septemba 25 mwaka huu kipa Djigui Diarra wa Yanga aliwapa darasa wachezaji wa Simba juu ya madhara ya kujisahau pindi mpira unapokuwa mikononi mwa kipa wa timu pinzani.

Wakati wachezaji wa Simba wakirudi upande wao taratibu huku wakiwa hawajakaba wapinzani baada ya kufanya shambulizi langoni mwa Yanga, Diarra ambaye mpira ulikuwa mikononi mwake alipiga pasi ya mbali kwa mguu wake iliyopita vichwani mwa nyota wa Simba na kutua kwa winga Farid Musa.

Farid ambaye alipokea pasi hiyo ndefu kutoka kwa kipa wake akiwa upande wa kushoto, alifanya uamuzi wa haraka wa kuingia kwa kasi katika eneo la hatari la Simba na kumpasia Fiston Mayele ambaye hakufanya ajizi kwa kuunganisha moja kwa moja pasi hiyo na kuifungia bao pekee Yanga ambalo liliwapa taji la Ngao ya Jamii.

Ni bao lililotokana na uharaka wa Diarra katika kuanzisha mpira ambao ulikuwa mikononi mwake mara baada ya kuona wapinzani bado hawajawa tayari kwa shambulio la haraka baada ya kufanya shambulizi langoni mwako.

Kitendo cha Simba kufungwa bao lile kilikuwa ni ishara tosha ya tatizo halisi la timu za Kitanzania kujisahau nyakati kadhaa za mchezo hasa pale wanapomaliza kufanya shambulizi kutokana na hisia mpira ulio upande wa adui hauwezi kuwa na hatari kwao.

Huwezi kulibishia hili kwa sababu Simba ndio timu iliyofanikiwa zaidi katika soka la Tanzania katika miaka ya hivi karibuni kwenye mashindano ya ndani na yale ya kimataifa hivyo inategemewa wachezaji wake wawe na kiwango cha juu zaidi cha umakini (concentration) pindi wawapo uwanjani hivyo kama walizidiwa ujanja na Diarra maana yake hata kwa timu nyingine tatizo hilo lilikuwepo.

Siku mbili baada ya bao hilo lililotokana na shambulizi la Diarra dhidi ya Simba kwenye Ngao ya Jamii, kipa wa Mbeya City, Haruna Mandanda yeye akajibu mapigo kwa kufanya zaidi ya kile kilichoonyeshwa na kipa wa Yanga.

Mandanda yeye alisaidia kupatikana kwa bao pekee la ushindi kwa timu yake dhidi ya Prisons baada ya kupiga pasi ya mwisho kwa mshambuliaji Peter Mapunda aliyeukwamisha mpira huo wavuni katika dakika za lala salama ambazo kila mmoja aliamini mechi hiyo ingemalizika kwa sare tasa.

Oktoba Mosi, kipa wa Simba Aishi Manula naye akafuata nyayo za wenzake kwa kushiriki katika kupika bao pekee lililowapa ushindi ugenini dhidi ya Dodoma Jiji, baada ya mpira mrefu aliompigia Chris Mugalu kuunganishwa na mshambuliaji huyo kwa kichwa kwenda kwa John Bocco aliyeukwamisha wavuni.

Inawezekana kile ambacho kilifanywa na Diarra siku ile ya Ngao ya Jamii, kilizifungua akili timu na zikajifunza kipa mbali na jukumu la kulinda lango, anaweza kuwa mwanzilishi mzuri wa mashambulizi na chanzo cha mabao kwa timu.

Pengine kabla ya hapo hili halikufanyiwa kazi na timu zetu jambo lililosababisha zisinufaike na mashambulizi ya namna hiyo ambayo yanaanzishwa na makipa.

Ukienda kutembelea na kujionea mazoezi ya timu nyingi za Ligi Kuu hapa nchini, ni vigumu kuona makipa wakifanyishwa program za kuwajengea uwezo wa kuanzisha mashambulizi ama kushiriki katika mchezo kama wachezaji wengine.

Makipa wengi wamekuwa wakifanyishwa mazoezi ya kudaka na kuruka kuokoa mipira inayotokea pembeni au mashambulizi ya ana kwa ana na sio yale ya umiliki wa mpira kwa miguu yao na kuichezea ambayo ndio mahitaji ya soka la kisasa.

Labda kuanzia sasa makipa wa timu zetu wataanza kunolewa kimbinu ili wawe na ubora na ufanisi mkubwa katika kushiriki mchezo hasa kuanzisha mashambulizi kama alivyofanya Diarra na baadaye Mandanda kisha Aishi Manula.

Pia huenda baada ya mabao hayo matatu, timu zetu zitapata somo kwamba umakini ndani ya uwanja unapaswa kuwepo katika dakika zote za mchezo hadi pale filimbi ya mwisho inapopulizwa pasipo kujali aina ya matokeo na mahali ambako mpira upo.

Haya ni matokeo ya kuwa na wachezaji wa kigeni ambao wana vitu vya ziada ambavyo mwisho wa siku vinasaidia kuendeleza soka letu na sio kuja nchini kupoteza muda na kula fedha huku wakiwa hawana mchango wowote.