MTU WA MPIRA: Unamuacha Ntibazonkiza, unamsajili Kisinda?

KAMA kuna kituko kingine kikubwa kimefanyika mwaka huu ni hiki hapa.
Ni hiki cha Yanga kuachana na Saido Ntibazonkiza na kwenda kumsajili Tuisila Kisinda. Ulikuwa ni uamuzi wa ovyo kweli kweli. Yanga walituaminisha kuwa Saido amechoka na ni mzee. Inataka wachezaji vijana wenye kasi zaidi. Watu wakasubiri.
Yanga ikamrejesha Kisinda. Nini kimetokea? Ni mchezaji anayekimbia tu bila mahesabu. Mchango wake kwenye timu umekuwa mdogo kuliko udogo wenyewe.
Saido akachagua kwenda pale Geita. Akakiwasha sana. Simba ikamuona kama mchezaji wa timu kubwa.
Pale Geita, Saido alikuwa ndiye roho ya timu. Aliamua washambulie vipi. Akawabeba kwenye mabega. Akatoa pasi za mabao na kufunga. Watu wakabaki wanajiuliza Yanga ilimuachaje?
Lakini hiki alichofanya juzi Ijumaa kwenye mechi yake ya kwanza pale Simba ni matusi makubwa sana kwa Yanga. Ni kama waliuza bastola wakanunua panga.
Saido bado ni mchezaji mkubwa. Sina mashaka na atakachofanya pale Simba. Ana akili kubwa ya mpira. Ana utulivu mguuni. Anakaa kwenye nafasi na anafunga.
Ukweli mchungu ni kwamba kila Simba inapocheza, itakuwa ni maumivu makubwa kwa Yanga kuona Saido akiwa kwenye kilele cha ubora wake.