Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Masalanga: Yanga imenibadilisha maisha ndani na nje ya Uwanja

Muktasari:

  • Masalanga alijiunga na Yanga baada ya kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika nchini Morocco na kuonyesha kiwango cha juu.

GOLIKIPA wa Yanga, Hussein Masalanga anasimulia namna ambavyo  amejifunza vitu vikubwa kwa muda mfupi aliyoichezea klabu hiyo, aliyojiunga nayo Januari 18,2026 akitokea Singida Black Stars.

Masalanga alijiunga na Yanga baada ya kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika nchini Morocco na kuonyesha kiwango cha juu.

Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, Masalanga anasema kutokana na ukubwa wa Yanga, kuna vitu ambavyo anavizingatia ili kulinda brandi ya klabu hiyo, kwani endapo akifanya kitu ambacho siyo kizuri inakuwa haileti picha nzuri.

"Kwanza ni klabu inayowaza mambo makubwa hivyo inawajenga wachezaji wake kuwaza kwa ukomavu na kuwa profeshino zaidi, ingawa nikirejea mtaani kwangu maisha yangu ya kawaida sana, nashirikiana na jamii kwa kila kitu," anasema ambaye amekosa nafasi ya kucheza michezo mingi kwenye timu hiyo kutokana na ubora ambao umekuwa ukionyeshwa na kipa namba moja wa timu hiyo, Djigui Diarra.

 MAISHA NDANI YANGA

Kipa huyo mwenye vituko vingi nje ya uwanja anasema akiwa Yanga amejifunza namna kuishi kisasa, kuanzia mazoezi, mechi za ushindani wa namba na maisha ya kawaida, tofauti na awali ambapo alikuwa hafanyi baadhi ya vitu.

"Kitu kikubwa ni nidhamu ya muda kwa kila kitu, jambo lingine ni kila mchezaji anatamani kuitumikia timu kwa kiwango bora, haijalishi hapati nafasi ya kucheza  mara kwa mara wakati wa mazoezi kila mtu anapambana kama vile anakwenda kucheza kikosi cha kwanza," anasema na kuongeza;

"Nimejifunza upendo wa hali ya juu Yanga pamoja na umoja na mshikamano wa kupambania mafanikio ya timu, kifupi tunaishi kama ndugu."

Anasema wakati anajiunga na Yanga alipokelewa na Kibwana Shomari anayeishi naye kama ndugu akamuelekeza jinsi ya kuendana na maisha ya klabu hiyo.

"Kibwana, Dickson Job na Twalib Mshery, hao ni wadogo zangu, maana wote tumepitia katika kituo cha Soka cha Moro Kids, niliwatangulia miaka miwili mbele wakati naondoka wao walikuja  nyuma yangu, hivyo sikupata shida kuzoeana na nao nilipotua Yanga," anasema.

KUHUSU DIARRA

Anasema kwake anaiona ni bahati kucheza na kipa mkubwa kama Djigui Diarra kinara wa cleansheets 18 katika ligi iliyomalizika Juni 30 na kukiri kajifunza vitu vingi kutoka kwake.

"Nimejifunza kujiamini, kujua nafanya kitu gani kwa muda sahihi, Diarra ni miongoni mwa makipa wa kigeni ambao wana kila kitu kinachotakiwa kwa kipa wa kisasa, ndiyo maana anaweza akaanzisha mashambulizi, vivyo hivyo kwa Mshery pia anacheza soka la kisasa kama ambavyo anafanya Diarra," anasema Masalanga na kuongeza;

"Nakumbuka mechi yangu ya kwanza ilikuwa dhidi ya Pamba tulishinda mabao 3-0 ugenini, kipindi hicho Diarra alikuwa nyumbani kwao, alinitumia ujumbe wa kunitia moyo.

"Miongoni mwa maneno aliyoandika alisema: ''Nakuamini wewe ni kipa namba moja Tanzania, haijalishi unapitia changamoto gani, jiamini, umepata nafasi ya kuonyesha onyesha, timu inakutegemea, jitoe kwa nguvu zako zote, weka na umakini wa juu kuhakikisha Yanga inavuna pointi tatu."

KAULI YA GSM ILIMPA NGUVU

Anasema Yanga imemkutanisha na watu ambao hakutarajia angekaa nao na kupiga stori hata kwa dakika mbili tu, kama  mdhamini wa klabu hiyo, Gharib Said Mohammed 'GSM'.

"Kwa mara ya kwanza nilikutana na GSM wakati Yanga inacheza michuano ya kimataifa, ilikuwa Zanzibar, baada ya kusalimiana naye, alikuwa wa na watu ambao alikuwa anapiga nao stori kuhusiana na mambo mbalimbali ikiwemo kuniongelea mimi.

"Nilisikia akiwaambia huyo kipa ni mzuri, nimemfuatilia katika mechi za timu ya taifa, hivyo naomba mtunzeni na kumjenga kwa ajili ya faida ya taifa.

"Kauli yake ilinipa moyo sana, nikasema kama naweza kufuatiliwa na mtu mzito kama GSM napaswa kuzidisha mazoezi na nidhamu."

MEDALI NI SPESHO KWA MKEWE

Anasema kwa mara ya kwanza kuvaa medali ya ubingwa wa Ligi Kuu kaipata akiwa Yanga, lakini kwake anaitoa spesho kwa ajili ya mkewe :"Naishi Dodoma, nimeibeba na tayari nimemkabidhi mke wangu maana ananilelea watoto, anatunza mji nikiwa kazini.

Anaongeza:"Wakati nipo mbali yeye muda wote anasimamia vitu vyangu, ananiombea, ananishauri, mke wangu ni mshikaji wangu kama napitia kitu kigumu au cha furaha mtu wa kwanza kumwambia ni yeye, lakini  medali nyingine ni Mapinduzi, nikiwa Singida BS nimechukua ya ubingwa wa CECAFA na Kombe la FA ."

Pamoja na furaha aliyoipata akiwa na Yanga, lakini mechi iliyomuachia maumivu makali anaitaja ni dhidi ya Dodoma Jiji 3-2 Yanga, alitangulia kudaka Diarra akasikia vibaya akatoka akaingia yeye.

"Ilikuwa ni mechi ambayo tulitakiwa kushinda, lakini tukafungwa na ikawaumiza mashabiki sana, hiyo imebakia moyoni kwa maumivu," anasema Masalanga.

Kabla ya kwenda kujiunga Yanga, akiwa Singida BS aliwahi kumtabiria nahodha wa timu hiyo Job,  kwamba atafunga bao katika michuano ya kimataifa na ikawa hivyo, anasema na baada ya kuwa sehemu ya Wanajangwani amefanya mara nyingi.

"Mara ya mwisho nilimwambia Prince Dube kwamba nitamuombea dua atafunga dhidi ya JKT Tanzania mechi ya mwisho iliyotupa ubingwa,  baada ya hapo nikafanya dua na akafunga, akaniambia amefurahi," anasema.

Dube ambaye ameondoka Yanga akiwa amefunga 10 msimu uliopita wa ligi,  anamuelezea kama mchezaji aliyependa amani na kila mtu:" Namtakia kila lenye heri, ila ni mtu mwenye busara, mstaarabu naamini ataendelea kuwa mwema, huko alikokwenda."

TOP 4 YA MAKIPA

Anasema katika Ligi Kuu Bara makipa anaowakubali wa kwanza ni yeye mwenyewe, Diarra, Zuberi Foba wa Azam FC, Yona Amosi wa Pamba na Ramadhani Chalamanda wa JKT TZ.

"Ukiachana na makipa, washambuliaji ninaowakubali na waliwahi kunifunga baadhi ni Dube, aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele, Paul Peter (mabao tisa), Anwari Jabir wa Dodoma Jiji na wengine wengi,"


INSTAGRAMU YAKE KWA SASA

"Kabla ya kuja Yanga sikujua nilikuwa na wafuasi gani ila walikuwa kidogo, lakini kwa sasa naona ninawafuasi wengi nina 11.7K imetokana na timu ninayochezea," anasema Masalanga ambaye amecheza mechi tatu za ligi na mbili FA akiwa na Yanga.


JE, SOKA LIMEMLIPA

"Ingawa bado soka nalidai, lakini kwa sehemu limenifanyia mengi, nina nyumba, gari, hivyo vyote vimetokana na kazi hiyo, lakini kwa vijana ambao wanatamani kucheza mpira wasome kwanza ndipo waingie kucheza mpira," anasema.