Prime
MTU WA MPIRA: Tunachojidanganya wabongo kuhusu kwenda kucheza Ulaya

MASHABIKI wa soka wa Bongo wanapenda uongo na ndio sababu tunatumia muda mwingi kudanganyana. Ndio maana ni rahisi kusikia wakisema Taifa Stars imefuzu fainali za Afcon 2023 kwa sababu imeachiwa na Algeria, lakini wakashindwa kutoa uthibitisho.
Kuna wengine wanaenda mbali na kusema eti ni kwa vile kocha Adel Amrouche anatokea Algeria, hivyo alifanyiwa ‘mandingo’ kusudi CV yake itakate zaidi, lakini ukimuuliza una ushahidi katika hilo ataishia kucheka na kukomalia hilo. Na kama wameisikia ile kauli iliyotolewa na kocha Milutin Sredojevic ‘Micho’ aliyekuwa akiinoa Uganda kabla ya kutumuliwa kuwa Algeria iliibeba Tanzania watakazia hapo.
Uongo katika soka la Kibongo ni kawaida, kwani utasikia Yanga imemfunga KMC kwa sababu mwamuzi kahongwa. Simba imeshinda Mtibwa Sugar eti waliachiwa na blahblah za hapa na pale. Wengine wanajua wanatuongopea, lakini hawajali kwa vile wanajua hata sisi tunapenda stori za uongo uongo.
Ni kama vile tunavyokuwa tukisikia kila mara juu ya taarifa za mchezaji flani za hizi za mitaa ya klabu za Karikaoo kwamba anajiandaa kutimka kwenda kucheza soka Ulaya. Kuna wakati iliwahi kuvumishwa kwamba kiungo Said Ndemla aliyekuwa akikipiga Simba enzi hizo, eti angeachana na timu hiyo kwa alikuwa anajiandaa kwenda kucheza Ulaya.
Lakini baada ya miaka kwenda na kumshuhudia Ndemla akihama kutoka timu moja hadi nyingine bila kuwa na uhakika wa kucheza kikosi cha kwanza kwa timu alizopita, utaishia kucheka tu.
Kelele kwa sasa zimekuwa nyingi baada ya Dismas Novatus kutua Shakhtar Donetsk ya Ukraine akitokea Ubelgiji. Kuna watu wanaona ni kazi rahisi na kuanza kuwahesabia mastaa wengine wa Kibongo kwenda kucheza huko.
Wengi wa mashabiki hao waongo waongo huwa wanaona Ulaya kama ni sehemu ambayo mchezaji anaweza kwenda tu kwa kuwa ametaka kwenda. Hatutaki kuzungumza ukweli.
Katika hali ya kawaida mchezaji ambaye hana nafasi katika kikosi cha kwanza cha timu ya Ligi Kuu Bara anawezaje kwenda kucheza Ulaya? Ama ni Ulaya nyingine tofauti na hii ambayo naifahamu mimi.
Kwenda kucheza Ulaya sio kazi rahisi. Sio sehemu ambayo kila mtu anaweza kwenda kucheza. Hii ndio sababu hadi sasa Tanzania yenye watu zaidi ya milioni 60 tuna wachezaji wachache wanaocheza huko. Kuna Mbwana Samatta, Dismas na wale wengine waliopenya kwa kupata koneksheni zao na ndugu wanaishi huko miaka nenda hasa wale wanaotokea Zenji. Ulaya ni pagumu kwelikweli.
Sehemu pekee ambayo mchezaji anaweza kuamua kwenda kucheza soka muda wowote ni Uarabuni maana huko kuna michuano hata isiyokuwa na kichwa wala miguu. Waarabu wanapenda soka na kwao kuwalipa wachezaji ili wacheze kombe la mafuta mtaani kwao sio tabu.
Hii ndio sababu hadi Danny Lyanga aliyekuwa hana nafasi Simba alishakwenda Uarabuni na akacheza. Hiyo ndio sababu Mrisho Ngassa alishindwa maisha Sauzi, lakini alienda Uarabuni na akacheza. Hii ndio sehemu pekee nyepesi kucheza soka. Kwa sasa Saudia Arabia inaweza kuleta ugumu kutokana na fedha ilizomwaga na kuleta mastaa wenye majina makubwa kutola Ulaya na Latin Amerika.
Ndio maana Simon Msuva na umahiri wake wote alishindwa kuingia Ulaya akaenda Saudia, lakini fedha zilivyoanza kumwagwa na Wasaudia amerejea Afrika Kaskazani. Ametua Algeria baada ya awali kusajiliwa Morocco.
Hii Ulaya tunayoambiwa anaweza kwenda George Mpole au Kibu Denis sio mchezo, labda kama anaenda kucheza muziki. Ili mchezaji akacheze Ulaya ni lazima awe amekamilika. Ni lazima awe na kipaji halisi cha soka na awe anacheza kwa kiwango cha juu kwa uwiano sawa na kwa muda mrefu. Ni lazima awe na nidhamu ya ndani na nje ya uwanja.
Ni lazima awe anajitambua kwelikweli. Pia amecheza soka kwenye nchi zenye kutambulika kwa ubora. Ndivyo alivyopenya Samatta baada ya kukinukisha TP Mazembe ya DR Congo kisha akaenda Genk ya Ubelgiji kabla ya kutua Aston Villa ya England, akapita Uturuki na sasa yupo Ugiriki. Novatus alianzia Israel kisha sasa Ubeligiji, halafu Ukraine akijiandaa kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ukikosa kitu kimoja kati ya hivyo, ni vigumu kwenda kutamba Ulaya. Haruna Moshi ‘Boban’ alikuwa na uwezo mkubwa uwanjani, lakini maisha ya nje ya uwanja yalimbana na akarudi mapema tu. Emmanuel Okwi pamoja na kipaji chake anasugua benchi pale Denmark. Ulaya sio mchezo mchezo ati.
Thomas Ulimwengu na uwezo wake. Na nguvu zake pamoja na kasi yake yote bado hakupata timu Ulaya akazunguka Algeria, Sudan kisha karudi DR Congo na sasa yupo Singida Fountain Gate. Pamoja na kipaji chake, lakini Ulimwengu alienda mara kadhaa kufanya majaribio katika klabu kadhaa Ulaya ili kupata nafasi. Kumbuka hapa tunamzungumzia Ulimwengu ambaye alikuwa na nafasi katika kikosi cha kwanza cha TP Mazembe iliyotwaa Kombe la Shirikisho Afrika.
Ni Ulimwengu ambaye alikuwa na nafasi katika kikosi cha kwanza cha Mazembe iliyotwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Ni Ulimwengu mwenye wasifu wa kutisha, lakini kwenda Ulaya imemkataa.
Hata wachezaji wamekuwa wakitudanganya wanapokwenda kufanya majaribio nje. Wanakuja na hadithi kwamba amefuzu majaribio, lakini amerudi ili kuweka mambo sawa. Hata hivyo, huu ndio uongo ambao Watanzania wanaupenda. Tunapenda kujidanganya na mwisho wa siku tunaishi katika uongo.
Wachezaji wetu mahiri bado wanafeli majaribio katika klabu za Afrika Kusini na DR Congo halafu tunatamani waende kucheza Ulaya. Kama unashindwa kushindana na nyota wa hapa Afrika, utawezaje kwenda kucheza Ulaya. Sio kama Ulaya kuna maajabu, lakini ili kupata nafasi ni lazima mchezaji awe amedhamiria kweli na sio mchezaji mwenye viwango vya homa ya vipindi. Mechi hii yupo, mchezo ujao anakuwa wa hovyo. Soka la kulipwa nje ya nchi linahitaji kujitoa na kujituma.
Je, ni mchezaji gani wa Tanzania ambaye anafanya mazoezi saa sita au zaidi kwa siku? Jibu ni jepesi tu, hakuna. Kama hakuna, ni nani ataweza kwenda Ulaya? Ndio maana tunaendelea kupigwa kamba na hizi ishu za wachezaji kutaka kwenda kucheza Ulaya, lakini wakijua kabisa wanatupiga kamba.