MTU WA MPIRA: Nabi ni kocha bora zaidi kuwahi kutokea Yanga?

YANGA ipo kwenye kilele cha mafanikio. Imebeba taji la Ligi Kuu Bara ikiwa na michezo miwili mkononi. Imebeba taji hilo kwa mara ya pili mfululizo.  Hilo ni taji la 29 kwa timu hiyo tangu ligi hiyo ilipoasisiwa mwaka 1965.

Huko Afrika Yanga imefuzu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Ni mara ya kwanza katika historia yao. Ni mara ya kwanza katika historia ya soka la Tanzania. Achana na mjadala unaendelea juu ya Simba kufika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993. Hapa tunzungumzia Kombe la Shirikisho Afrika lililoasisiwa mwaka 2004 baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuunganisha Kombe la CAF na Kombe la Washindi. Kombe la CAF liliasisiwa mwaka 1992 baada ya don wa Kinigeria aliyekuwa mfanyabiashara na mwanasiasa mashuhuri nchini humo, Mashoud Abiola kabla ya CAF kulibariki hadi 2003 lilipozikwa rasmi kuzaliwa Kombe la Shirikisho Afrika.

Hakuna aliyefikiri kama Yanga wangefika hapa leo. Walianza kampeni yao ya CAF kwa mguu mbaya msimu huu.

Wakaondoshwa na Al Hilal mapema katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Hawakuonekana kama wana jipya sana katika mashindano hayo.

Wakaangukia kwenye Kombe la Shirikisho. Nako hawakuanza vizuri. Walipopata suluhu hapa nyumbani dhidi ya Club Africain ya Tunisia, wengi tuliamini shughuli yao imeishia hapo.

Hata hivyo upepo ukabadilika ghafla. Walipofuzu hatua ya makundi bado hakukua na imani kubwa kwao. Walionekana ni kama wamebahatisha.

Yanga ilikuwa imekaa miaka minne bila kufika hatua ya makundi. Ungewazaje kwamba wanaweza kutamba kwenye Kundi ambalo TP Mazembe alikuwepo?

Mara mbili za mwisho kufuzu hatua ya makundi hawakuwa na jipya. Walimaliza kama vibonde wa kundi. Mara ya mwisho wakiwa na timu za Rayon Sports ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya na USM Alger y Algeria bado walimaliza mkiani.

Hivyo mwaka huu Hakuna aliyewapa nafasi kubwa sana. Cha kustaajabisha wakamaliza kama vinara wa kundi.

Ukiachana na mafanikio ya kufika fainali, kinachovutia kwa Yanga ni namna wanavyocheza kwa nidhamu kubwa.

Wakiwa na mpira ni Hatari sana. Wanapiga pasi za kutosha. Wanashambulia kwa mipango. Wakiwa hawana mpira wanakaba kwelikweli. Hawampi mpinzani nafasi yoyote ya kupumua.

Wakipokonya mpira wakati wanashambuliwa ni hatari sana katika mashambulizi ya kushtukiza. Kumbuka walivyowafunga TP Mazembe hapa Dar es Salaam.

Fikiria namna walivyofunga magoli yote mawili ugenini dhidi ya Marumo Gallants. Kasi ya Fiston Mayele na Kennedy Musonda ilimaliza mechi.

Yanga walipopora mpira walishambulia kwa kasi kubwa mithili ya Mwanadamu aliyekutana na Simba.

Kwa namna Yanga inavyocheza sasa watu wameaza Kuhoji endapo Nabi ndiye kocha bora zaidi kuwahi kutokea Yanga?

Ameweka rekodi ya kushinda ubingwa bila kupoteza mchezo hata mmoja. Ni rekodi kubwa sana. Nani alitegemea hili? Hakuna.

Ni rekodi kubwa sana kutwaa ubingwa bila kupoteza mchezo. Na Yanga hawakuishia hapo wamekwenda hadi mechi 48 bila kupoteza. Ni timu chache duniani zimewahi kufanya hivyo.

Mbali na rekodi hiyo, chini ya Nabi Yanga imetwaa mataji mawili ya Ligi Kuu, moja la Kombe la Shirikisho Azam (ASFC) na mawili ya Ngao ya Jamii.

Mwaka huu tayari ipo fainali ya Kombe ASFC na pia ipo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ni wazi kuwa Nabi amefanya kazi kubwa sana kuwarejesha Yanga katika kilele cha mafanikio yao.

Kabla yake walikuja makocha kadhaa lakimi wakashindwa. Huyu Cedric Kaze ambaye anamsaidia Nabi leo alishindwa kutamba vilivyo. Wakamwondoa kabla ya kumrejesha tena.

Kabla ya hapo alikuja kocha mmoja Mserbia, naye hakuwa na jipya. Wakamtimua ndani ya muda mfupi tu.

Kabla yake alikuwa Luc Eymael ambaye naye hakuwa na jipya sana. Wakamtimua.

Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kocha anayetajwa angalau kuwa na mafanikio makubwa Yanga ni Hans Van Pluijm. Huyu alitamba zaidi msimu wa 2015/16.

Ndiye kocha wa kwanza kuifikisha Yanga hatua ya makundi ya CAF baada ya miaka 19. Yanga yake ilikuwa tishio sana. Hata hivyo hawakufikia mafanikio ya Yanga ya sasa.

Nani anastahili kuwa kocha bora wa nyakati zote Yanga? Ni mjadala mpana sana.