MTU WA MPIRA: Hili la Manara na Karia bado linafikirisha

Hii nchi kuna wakati uhuru umezidi. Mtu anaweza kuamka asubuhi na akamchafua mwingine bila watu kujali. Wengine wakasimama na kusheherekea kabisa.

Ni kama hiki kinachoendelea kwa aliyekuwa Msemaji wa Yanga, Haji Manara dhidi ya Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia.

Manara aliitisha mkutano uchwara na Waandishi wa Habari wiki iliyomalizika. Akaanza kumshambulia Rais wa TFF kama vile makombora ya Urusi yanavyotua mashariki kwa Ukraine.

Yaani mpaka unajiuliza uhuru huu umetoka wapi? Manara anapata wapi jeuri hii ya kumshambulia Karia pamoja na Waziri wa Michezo? Kuna kitu hakipo sawa.

Unaposimama na kutoa shutma dhidi ya mtu ni lazima uwe na ushahidi. Huwezi kusema tu kwa maneno ya kusikia. Lakini Manara amedhubutu kumshambulia Karia hadharani tena bila wasiwasi.

Mpira wetu umefikia pabaya sana. Manara ni sehemu ndogo sana ya mpira wa Tanzania. Ni kama uzi mmoja tu katika joho zima. Hata akitoka hakuna atakayejua.

Lakini mtu mdogo kiasi hicho anawezaje kushambulia mamlaka mpaka Wizara?

Unawazaje kumwambia Waziri wa Michezo kuwa alidanganywa na bahati mbaya hakufanya uchunguzi kujiridhisha? Kwamba alikurupuka?

Halafu Manara akatoa maelekezo kwa Waziri wa Michezo kama vile anaongea na shemeji yake nyumbani. ‘Kama ulivyozungumza kwa mbwembwe kuwa nifungiwe, kwa mbwembwe zilezile uende ukasimamie Kanuni zisajiliwe.”.

Huku ni kukosa adabu kulikopindukia. Unawezaje kufanya hivyo?

Hata hivyo pia katika hili lililotokea sasa la Manara, linapaswa kumfanya Karia ajitathmini. Kuna kitu hakipo sawa katika uongozi wake. Watu wanamuona kama mtu wa kawaida tu.

Rais wa soka kwenye nchi si mtu wa kawaida. Ana heshima zake. Ana mamlaka zake. Lakini huoni Karia akipewa hizo heshima. Anapaswa kutazama mwenendo wake.