Mtoto wa Matumla apewa KO ya Mama

Muktasari:
- Mtoto huyo wa Rashidi aitwaye Amiri Rashid Matumla atakuwa miongoni mwa mabondia watakaozichapa, lakini jina lake likiwa miongoni mwa yanayotarajiwa kutawala.
Februari 22, mwaka huu kwenye Ukumbi wa City Centre, Magomeni, Mafia Boxing inatarajia kufanya pambano lingine kubwa la Knockout ya Mama, huku mtoto wa bondia mkongwe zamani, Rashid Matumla ‘Snake Man’ akipewa kucheza pambano kuu.
Mtoto huyo wa Rashidi aitwaye Amiri Rashid Matumla atakuwa miongoni mwa mabondia watakaozichapa, lakini jina lake likiwa miongoni mwa yanayotarajiwa kutawala.
Mwanaspoti linakuchambulia mabondia watakaopanda ulingoni kwenye pambano hilo litakalokuwa na mapambano 11 ambalo limeanza kuwa gumzo kwa mashabiki wa mchezo kutokana na kuwepo mtoto wa Matumla ambaye amekuja na moto mkubwa kwenye mchezo huo.

Matumla vs Amavila
Kwa mujibu wa mtandao wa Boxrec, Amiri ambaye pia anafahamika kama Matumla Jr ndiyo kwanza amefikisha umri wa miaka 20, lakini rekodi yake ikiwa ni moto wa kuotea mbali kutokana na kufanya vizuri katika mapambano yake.
Matumla Jr anatarajia kupanda ulingoni dhidi ya Paulus Amavila kutoka Namibia katika pambano la raundi nane la uzani wa super walter huku likiwa ndilo kuu ‘main card’. Rekodi zinaonyesha Matumla ambaye baba yake mzazi pamoja na familia wana rekodi nzito na mchezo huo, amecheza mapambano sita ambayo sawa na raundi 33.
Matumla Jr amefanikiwa kushinda yote sita kati ya hayo mawili akishinda kwa Knockout huku akiwa hajawahi kupigwa wala kutoka sare katika pambano lolote kwa mujibu wa Boxrec.
Bondia huyo mwenye hadhi ya nyota mbili anashika nafasi ya tatu nchini katika mabondia 52 wa uzani wa middle licha ya pambano lake lijalo kupigania kwenye uzani wa super walter wakati duniani akiwa wa 167 katika mabondia 1957.
Wakati mpinzani wake, Paulus Amavila kutoka Namibia amecheza mapambano 13 sawa na raundi 69, amefanikiwa kushinda mapambano 10 kati ya hayo matano ni knockout, amepigwa mara mbili kati ya hizo moja ni kwa knockout na sare mara moja.
Katika pambano hilo, Amavila atapanda kwa kilo moja zaidi kutoka kilo 69 ya Walter hadi super walter ya kilo 70 wakati Matumla atapunguza kilo mbili kutoka 72 hadi kilo 70 ya super walter na vita itapigwa wakiwa kwenye kilo sawa.
Mchanja vs Amukwa
Bingwa wa WBO Global nchini, Mchanja Yohana atapanda ulingoni dhidi ya Jafet Amukwa kutoka Namibia katika pambano la raundi nane ambalo litapigwa kwenye uzani wa fly.
Mchanja atapanda ulingoni kwenye pambano hilo akiwa amecheza mapambano 26 sawa na raundi 145 akiwa ameshinda 19 kati ya hayo 13 ni kwa knockout, amepigwa mara sita bila kuwepo knockout na ametoka sare mara moja.
Bondia huyo kwa sasa amefikisha hadhi ya nyota mbili na nusu akiwa anashika namba moja nchini katika mabondia 45 wa uzani wake wakati duniani akiwa wa 39 katika mabondia 781.
Lakini mpinzani wake kutoka Namibia, Amukwa amecheza mapambano 16 na amefanikiwa kushinda tisa kati ya hayo matatu ni kwa knockout, amepigika mara sita kati hizo mbili ni kwa knockout huku akitoka sare mara moja.
Amukwa mwenye hadhi ya nyota moja anashika nafasi ya nne katika mabondia 10 wa uzani wake Namibia wakati duniani akiwa wa 201 kati ya mabondia 781.
Mtangi vs Mahesh
Mara ya mwisho kuonekana ulingoni ilikuwa Agosti 10, mwaka jana baada ya hapo akapotea mazima bondia Richard Mtangi ‘Duma’ kabla kupata nafasi ya kuonyesha makali yake dhidi ya Digari Mahesh wa India.
Mtangi atapanda ulingoni kwenye pambano hilo la raundi nane akiwa na rekodi ya kucheza mapambano tisa, amefanikiwa kushinda saba kati ya hayo sita ni knockout, amepigwa mara moja huku akitoka sare mara moja.
Mtangi anacheza kwenye uzani wa middle akiwa na hadhi ya nyota mbili, anashika nafasi ya pili katika mabondia 52 wa uzani huo wakati duniani akiwa wa 126 katika mabondia 1957.
Wakati mpinzani wake raia wa India anayecheza kwenye uzani wa light akiwa na hadhi ya nyota moja, amecheza mapambano 17, ameshinda 11 kati ya hayo saba ni kwa knockout, amepigwa mara tano kati ya hizo mbili ni kwa knockout na ametoka sare moja.
Richard vs Makovola
Oscar Richard kijana wa kutoka Naccoz Gym, atapanda ulingoni kwenye jukwaa hilo dhidi ya Bongani Makovola katika pambano la raundi nane, uzani wa light.
Richard mwenye rekodi ya kucheza mapambano 24 akiwa ameshinda 14 kati ya hayo manne pekee ameshinda kwa pointi, amepigwa mara nane huku akitoka sare mara mbili.
Bondia huyo wa uzani wa feather akiwa na hadhi nyota moja na nusu anashika nafasi ya sita katika mabondia 57 wa uzani wake nchini wakati duniani akishika nafasi ya 318 katika mabondia 1778.
Mpinzani wake kutoka Zimbabwe, Bongani Makovola mwenye hadhi ya nyota, moja na nusu, amecheza mapambano kumi, akishinda sita kati ya hayo matatu kwa knockout na amepigwa mara nne.
Makovola anakamata nafasi ya pili katika mabondia watano wa uzani wake nchini Zimbabwe wakati duniani akiwa 234 katika mabondia 1133.

Chino vs Assumani
Said Chino ‘Buldog’ ambaye ni bingwa wa IBA Inter-continental atapanda ulingoni dhidi ya Gael Assumani kutoka DR Congo katika pambano la raundi nane, uzani wa Light.
Chino mwenye rekodi ya mapambano 38, akishinda 24 kati ya hayo 15 ni kwa Knockout na akiwa amepigwa mara 12 kati ya hizo tatu ni kwa knockout huku akitoka sare mara mbili. Bondia huyo kwenye uzani wa light, anashika nafasi ya tatu katika mabondia 107 wakati duniani akiwa 123 katoka mabondia 2481.
Mpinzani wake Gael Assumani wa DR Congo, yeye amecheza mapambano tisa, amefanikiwa kushinda nane kati ya hayo sita ni kwa knockout, amechezea kichapo mara moja kwa Knockout.
Nchi DR Congo akitokea kwenye mji Goma wenye machafuko kwa sasa, ndiye bondia namba moja katika mabondia kumi wa uzani huo wakati duniani akiwa 261 katika mabondia 2481.
Kalolo vs Kananji
Kalolo Amiri Chaubaya ambaye ni bingwa wa PST Tanzania, atapanda ulingoni dhidi ya Mussa Kananji wa Malawi.
Kalolo mwenye rekodi ya kucheza mapambano 12, akiwa ameshinda 11 kati ya hayo sita ni kwa knockout na ametoka sare moja, anakamata nafasi ya tatu katika mabondia 51 wa bantam wakati duniani akiwa wa 47 katika mabondia 1133.
Mpinzani wake Mussa Kananji wa Malawi amecheza mapambano mawili pekee ambayo yote ameshinda kwa pointi, anakamata nafasi ya kwanza katika mabondia watatu wa uzani wa bantam wakati duniani ni 307 katika mabondia 1133 wa uzani huo.
Bonabucha vs Mchanjo
Hapa kuna vita ya kali kati ya George Bonabucha dhidi ya Haidary Mchanjo kutokana na wote kuwa mabondia wakali nchini.
Bonabucha mwenye rekodi ya kucheza mapambano nane, ameshinda saba kati ya hayo mawili kwa knockout na amepigwa mara moja. Bonabucha hajapanda ulingoni kwa zaidi ya mwaka sasa.
Lakini Haidary Mchanjo ambaye rekodi yake inasoma amepigana mapambano 37, amefanikiwa kushinda 19 kati ya hayo saba ni kwa knockout na amepigwa mara 11 kati hizo moja kwa knockout huku akitoka sare moja.
Mchanjo anakamata nafasi ya tatu kati ya mabondia 59 wa super bantam wakati duniani akiwa wa 324 katika mabondia 1377 huku pambano lao likitarajiwa kuwa la raundi sita.
Magoma vs Chisolola
Abdurhaman Magoma ambaye ni mtoto wa bondia wa zamani, Shaban Magoma atapanda ulingoni dhidi ya Tamiwe Chisolola wa Malawi.
Bondia huyo ni mwenye rekodi ya kucheza mapambano matano, akishinda matatu kati ya hayo moja kwa knockout akiwa wa nane kwenye mabondia 45 wa uzani wa fly na duniani akiwa 191 katika mapambano 781.
Mpinzani wake amecheza mapambano tisa kati ya hayo ameshinda moja huku akipigwa saba kwa knockout na ametoka sare moja. Watacheza raundi sita kwenye uzani wa fly.
Chaka vs Sinkala
Bondia Isaack Chaka atapanda ulingoni dhidi ya Joseph Sinkala katika pambano la raundi sita, uzani wa middle. Chaka atapanda ulingoni akiwa na rekodi ya mapambano matatu ambayo ameshinda wakati mpinzani wake akiwa amecheza mapambano 27, ameshinda 14 kati ya hayo saba ni kwa knockout, amepigwa mara 12 kati hizo sita ni kwa knockout.
Twaha vs Lubega
Bondia Abdallah Twaha atapanda ulingoni dhidi ya Ahmed Lubega wa Uganda katika pambano la raundi sita uzani wa welter.
Twaha mwenye rekodi ya kucheza mapambano sita na ameshinda yote kati ya hayo manne ameshinda kwa Knockout wakati mpinzani wake, amecheza mapambano saba.
Ameshinda sita kati ya hayo moja kwa knockout na amepigwa pambano moja, watapanda ulingoni kwenye uzani wa welter, pambano la raundi sita.
Mbabe vs Kaonga
Mtaalamu Dullah Mbabe ndiye amekabidhiwa kufungua mapambano ya utangulizi ya Knockout ya Mama kwani atapanda ulingoni dhidi ya Mbachi Kaonga katika pambano la raundi sita, uzani wa super middle.
Mbabe mwenye rekodi ya kucheza mapambano 51, akiwa ameshinda 35 kati ya hayo 30 kwa knockout na amepigwa mara 14 kati ya hizo tatu kwa knockout na ametoka sare moja.
Bondia huyo anashika nafasi ya tisa katika mabondia 35 wa uzani wake nchini wakati duniania akiwa wa 287 katika mabondia 1726 huku akiwa na umiliki wa nyota moja na nusu.
Lakini kwa upande wa Mbachi Kaonga wa Zambia amecheza mapambano sita, ameshinda matano kati ya hayo manne kwa knockout amepigwa moja kwa knockout.
Kaonga ndiye bondia pekee wa uzani wa super middle nchini Zambia, lakini duniani anashika nafasi ya 300 katika mabondia 1726 huku akiwa na nyota moja.