Mtazamo kiafya aina ya mashabiki na tabia zao
Muktasari:
- Katika video iliyosambaa mitandaoni, Polisi walionekana kuwadhibiti vyema mashabiki hao na kufanikiwa kuwatia nguvuni wale waliokuwa vinara wa vurugu hizo.
JUMAPILI iliyopita, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kulikuwa na mechi ya marudiano ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika (CAF) ambapo Simba ilitoka sare ya mabao 2-2 na Esperance de Tunis.
Baada ya mechi hiyo kumalizika, kundi la mashabiki wa Simba walimzonga ghafla mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu, huku baadhi yao wakitishia kutaka kumpiga.
Tukio hilo lililazimisha Polisi wa kutuliza ghasia kuchukua hatua dhidi ya baadhi ya mashabiki hao waliodiriki kuonyesha viashiria vya kumfanyia vurugu na kumdhuru Mangungu.
Katika video iliyosambaa mitandaoni, Polisi walionekana kuwadhibiti vyema mashabiki hao na kufanikiwa kuwatia nguvuni wale waliokuwa vinara wa vurugu hizo.
Tukio hili la kumfanyia vurugu Mwenyekiti wa Simba halikubaliki katika medani ya soka. Vitendo hivyo havifai kwani vingesababisha vurugu kubwa ambazo zingeleta madhara kwa watazamaji.
Matukio kama hayo yanawekwa katika kundi la matendo ya kihuni katika soka. Ndiyo maana nchi zilizopiga hatua katika soka zina sheria kali za kudhibiti vitendo hivyo.
Vitendo vya kihuni ni pamoja na kuanzisha fujo, kurusha vitu viwanjani, kung’oa vifaa, kupigana, vitendo vya kibaguzi, ishara za kudhalilisha, kumulika miali ya tochi kwa wachezaji na matumizi ya lugha za matusi.
Kwa upande wa jicho la kitabibu, tukio hili linatukumbusha umuhimu wa kutoa ufahamu kuhusu aina za watazamaji na tabia zao, ambao baadhi yao ndio kama wale waliomfanyia vurugu Mangungu.
Ikumbukwe kuwa watazamaji wa mpira wa miguu ni watu wanaotazama mechi za soka ana kwa ana uwanjani au kwa mbali nje ya uwanja.
Mechi zinazoongoza kwa kutazamwa ni zile zinazohusisha soka la wanaume, hasa katika ligi kuu za nchi na mashindano makubwa ikiwamo Klabu Bingwa Afrika (CAF).
Ni tofauti na mashabiki ambao huwa na uhusiano wa kihisia na timu zao, huku watazamaji waungwana wakiwa waangalizi wasioegemea upande wowote. Maelfu ya watu hujazana viwanjani na wanaweza kugawanywa katika makundi mbalimbali.
Ndiyo maana unapokata tiketi ya kutazama mpira hupewa uchaguzi wa eneo la kukaa, na mara nyingi hutolewa ushauri kuhusu eneo linalokufaa kulingana na aina yako kama mtazamaji.
UMUHIMU WA WATAZAMAJI
Watazamaji ni muhimu kwa angahewa ya uwanja kwani mara nyingi hushangilia, kupunga mikono na kupiga makofi ili kuunga mkono timu zao.
Wao huwa chachu ya ushindi kwa timu, wakileta hamasa na ari ya kucheza kwa bidii kwa wachezaji hata pale timu inapokuwa imefungwa.
Watazamaji huchukua nafasi kubwa viwanjani kwa kulipa viingilio na kukaa kwenye viti vilivyopangwa kuzunguka uwanja ili kuwawezesha kutazama kwa wigo mpana.
Mara nyingi huelezewa kama hadhira au umati, na hutengeneza mazingira makubwa yaliyojaa watu, kama ilivyo kwa Uwanja wa Benjamin Mkapa unaobeba zaidi ya watazamaji 60,000.
Wingi wa watazamaji kwenye viwanja vya soka ni faida kubwa kiuchumi, lakini pia ni silaha muhimu katika saikolojia ya kandanda. Ushangiliaji huweza kumfanya mpinzani awe na hofu na hivyo kuvuruga umakini wake kiakili.
Mfano wa uwanja maarufu duniani kwa angahewa ya kipekee ya watazamaji ni dimba la Anfield, uwanja wa Klabu ya Liverpool ya England.
Watazamaji wa hapo ni mashabiki wa kipekee kutokana na aina ya ushangiliaji wao. Hawajali wakiwa wamefungwa au wameshindwa; wao huimba na kuhamasisha dakika zote.
AINA ZA WATAZAMAJI NA TABIA ZAO
Wenye shauku; hawa ni wale waliowekeza hisia kwa kiwango kikubwa katika timu zao. Hapa nchini hujulikana kama mashabiki kindakindaki, na wengi wao ni wanachama wa klabu.
Vikundi vya hamasa; hawa hujipanga katika makundi ya kuimba, kucheza ngoma na kutumia tarumbeta ili kutoa hamasa kwa timu. Ni aina ya watazamaji wenye ushawishi mkubwa kutokana na maandalizi yao, na wakati mwingine hulipwa na klabu kwa kazi ya kuhamasisha.
Mashabiki wahuni
Hawa ni watazamaji wanaopenda timu zao kwa hisia kali lakini huwa chanzo cha fujo. Wanahusishwa na vurugu, machafuko na uvunjifu wa sheria.
Aina hii ndiyo ambayo Mwenyekiti wa Simba alikutana nayo na waliodiriki kumtolea maneno makali na kutaka kumpiga.
Mashabiki wahuni hawajali kuvunja sheria hata mbele ya Polisi, na wakati mwingine hujaribu kupambana nao wanapochukuliwa hatua. Mara nyingi hukaa katika jukwaa la mashabiki wa timu yao pekee.
Watazamaji waungwana; hawa ni wahudhuriaji wasioegemea upande wowote, wanaotazama mechi kwa ajili ya kufurahia, kuburudika, kustareheka na hata kutalii. Mara nyingi hupendelea kukaa katika jukwaa la V.I.P au jukwaa la mchanganyiko.
CHANZO CHA TABIA ZA VURUGU
Kuboronga kwa waamuzi au maamuzi yanayoonekana kutokuwa ya haki ni mojawapo ya chanzo cha vurugu. Mfano ni fainali ya AFCON 2025 kati ya Morocco na Senegal.
Mipango mibovu ya viwanja na maandalizi duni ya mashindano pia huchangia vurugu. Katika fainali ya UEFA 2022/2023, waandaaji walilaumiwa kama chanzo cha vurugu zilizotokea nchini Ufaransa.
Timu kufanya vibaya, rushwa na uongozi mbovu ni sababu nyingine za hasira kwa mashabiki wenye hisia kali, hasa wanapoona mambo hayaendi vizuri huku viongozi wakishindwa kuwajibika.
Ushabiki uliopitiliza na hamu ya kutambulika husababisha baadhi ya mashabiki kushikamana sana kihisia na timu zao, hali inayoweza kuchochea vurugu.
Aina za uchokozi ni pamoja na matusi ya maneno, kurusha vitu kama chupa au miale ya moto, matumizi ya miale ya mwanga, uharibifu wa mali na mapigano.
Kushindwa kwa usalama, kama usimamizi duni wa umati, ulinzi hafifu na mipango mibaya, mara nyingi hurahisisha kutokea kwa vurugu.
Mvutano wa kitamaduni au kisiasa katika mechi zenye hisia za utaifa pia unaweza kusababisha vurugu, mfano mechi kati ya Argentina na Brazil au Uingereza na Ujerumani.
Ugomvi wa makundi ya wahuni wenye visasi ni jambo la kawaida katika soka, ambapo vikundi hivyo huchokozana kuanzia mitaani hadi ndani ya uwanja.
Kamari pia ni chanzo kingine, kwani kupoteza fedha huwafanya baadhi ya mashabiki kuathirika kihisia na hatimaye kujihusisha na vurugu.
MBINU ZA KUDHIBITI WAHUNI
Katika nchi zilizopiga hatua kiteknolojia, unapokata tiketi huweka taarifa binafsi kama namba ya pasipoti, jambo linalosaidia kuwatambua watazamaji.
Viwanja vikubwa huwa na kamera za usalama zinazofuatilia mwenendo na tabia za mashabiki, na hivyo kubaini wahuni mapema na kuchukua hatua.
Sheria zinazotungwa huwa kali; mfano katika Ligi Kuu England, mashabiki waliowahi kufanya makosa makubwa hufungiwa kuingia viwanjani maisha yao yote.
Pia, kuwatenganisha mashabiki kulingana na aina zao husaidia kudhibiti vurugu, ambapo mashabiki kindakindaki wenye hisia kali hawachanganywi na aina nyingine za watazamaji.