MTASINGWA: Mfalme wa dimba la chini azam, tumaini Stars

Muktasari:
- Kiungo huyo ni miongoni mwa wachezaji waliopikwa katika akademi ya Azam FC, kabla ya Machi 2019 kwenda Icenald kujiunga na KR Reykjavik hadi mwaka Oktoba mwaka huo akaenda Keflavik, Juni 1, 2020 akarejea KR Reykjavik, kabla ya kujiunga na Volsungur ÍF Februari mwaka 2021 ambako alipiga kazi hadi Janauri mwaka 2022 akarejea Azam FC.
ADOLF Mtasingwa Bitegeko. Amekuwa mhimili mkubwa kwenye safu ya kiungo Azam FC. Ni mmoja wa nyota wanaotajwa kufanya makubwa kwenye kikosi cha Taifa Stars baada ya kuitwa mara mbili na anatarajiwa kujumuishwa kitakapotangazwa na Kocha Hemed Seleman 'Morocco'.
Kiungo huyo ni miongoni mwa wachezaji waliopikwa katika akademi ya Azam FC, kabla ya Machi 2019 kwenda Icenald kujiunga na KR Reykjavik hadi mwaka Oktoba mwaka huo akaenda Keflavik, Juni 1, 2020 akarejea KR Reykjavik, kabla ya kujiunga na Volsungur ÍF Februari mwaka 2021 ambako alipiga kazi hadi Janauri mwaka 2022 akarejea Azam FC.
Ubora wake unatajwa umewafanya wachezaji wenzake wanaocheza nafasi ya kiungo hasa ukabaji wasubiri benchi kwani ameaminiwa zaidi na makocha waliomfundisha akianza na Youssoupha Dabo na sasa Rachid Taoussi na wote wamekuwa wakimtumia kikosi cha kwanza.
Msimu huu ubora wake umeongezeka na amejihakikishia namba kikosi cha kwanza kwenye mechi 23, akicheza 17 akitumika kwa dakika 1,394, ingawa hajafunga bao hata moja ila amehusika kwenye bao moja akitoa pasi iliyozaa bao.
Mwanaspoti linakuletea namna kiungo huyu alivyoonyesha ubora wake na kuaminiwa zaidi na kujitengenezea ufalme, huku wenzake wakianzia benchi au kuwasaidia katika maeneo yao hasa la beki kuokoa mashambulizi.

NDIO HUYU SASA
Mtasingwa ni mzaliwa wa Bukoba mwenye umri wa miaka 25. Ubora wake wa kusoma mchezo, kupokonya mipira na kuanzisha mashambulizi haraka umemfanya kuwa mchezaji muhimu Azam akichukua namba mbele ya nyota wa wageni.
Pia amekuwa akiaminika Taifa Stars na huenda akaweka historia ya kucheza Afcon 2025 na Chan 2025 kama atajumuishwa katika kikosi cha mwisho cha Tanzania. Katika mechi za kufuzu amekuwa mhimili mkubwa, akionyesha utulivu na umahiri wake wa kuzuia mashambulizi ya wapinzani.
AANZA NA MOTO AZAM
Msimu wake wa kwanza tu (2023/24) Azam FC alitumika kwenye mechi 13 na alicheza kwa dakika 643.
Itakumbukwa nyota huyu alikuwa ametoka kucheza soka nje ya nchi na huko alionyesha uwezo mkubwa wa kukaba na kusambaza pasi sahihi akiwa na Keflavik kabla ya kurejea KR Reykjavik Juni 1, 2020 alikodumu kwa msimu mmoja na kisha kujiunga na Volsungur ÍF Februari 2021.
Huko aliongeza uzoefu wake wa soka la kimataifa hadi Januari 2022, alipopata shavu la kujiunga na Azam FC na kuishika safu ya kiungo hadi sasa.

BAJANA AMPISHA
Katika nafasi hiyo ya kiungo ya ulinzi, alikuwa anacheza Sospeter Bajana ambaye alikuwa nahodha na tegemeo katika kikosi hicho, akionyesha ukomavu mkubwa wa kupokonya mipira na kusaidia safu ya mabeki.
Hata hivyo, alikuwa nje kwa takriban miezi 10 kutokana na majeraha na alifanyiwa upasuaji wa maungio ya mifupa ya nyonga ya kulia na kushoto (pubis symphysis) na sasa kwa Mtasingwa ana kazi kubwa ya kufanya kulishawishi benchi la ufundi kumuamini na kurudi kwenye nafasi yake.
AKICHEZA SAMBAMBA NA AKAMINKO
James Akaminko ni kiungo wa kigeni aliyekuwa akitumika sambamba na Bajana na baada ya usajili wa Mtasingwa, uongozi ulikuwa unafanya mpango wa kuachana naye.
Hata hivyo, uongozi ulibadili gia na kuendelea naye kutokana na kukosekana kwa Bajana na amekuwa akicheza sambamba na Mtasingwa, huku wakitengeneza muunganiko mzuri katika safu ya ulinzi, huku Mtasingwa akiwa ni mzuri wa kukaba na Akaminko raia wa Ghana kutengeneza mashambulizi.
Hata hivyo, katika michezo ambayo itahitajika kiungo mmoja katika nafasi ya ukabaji, Akaminko atasubiri kwa Mtasingwa kutokana na ubora wake eneo hilo.

AWAPA PRESHA MEZA, ZAYDI
Yahya Zaydi amekuwa akicheza winga hadi kushuka eneo la ukabaji anakocheza Mtasingwa. Amekuwa pia akiaminiwa na makocha kutokana na uwezo wake lakini akibebwa zaidi na uwepo wa Mtasingwa.
Hakuwa sehemu ya kikosi kwa muda kutokana na kusumbuliwa na majeraha na haijawa mtihani kurudi kikosini kwani tayari ameanza kupata nafasi ya kucheza na amekuwa akionyesha uwezo mkubwa.
Kwa Ever Meza, ni kiraka ambaye mbali na kuwa kiungo mkabaji, ana uwezo wa kucheza kama beki wa kulia, upande ambao kwa Azam anatumika zaidi Lusajo Mwaikenda.
Meza ambaye ni kiungo alijiunga na Azam FC Julai 1, 2024 akitokea Amerika ya Kusini na alikuwa akiichezea Leones FC ya nyumbani kwao, Colombia.
Meza ana mtiani wa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara mbele ya Mtasingwa na Akaminko ambao wamekuwa wakipata zaidi nafasi katika mfumo wa 4-2-3-1.

NIDHAMU INAMBEBA
Akiwa kama kiungo mkabaji ameonyesha nidhamu ya kucheza katika nafasi yake na kuifanya safu ya kiungo kuwa na uweo wa kuzuia mashambulizi na kuwa mchezaji muhimu katika kikosi hicho na timu ya Taifa.
Anahakikisha kila wakati anasimama kwenye maeneo yatakayosaidia kusaidia ulinzi wa ziada kwa mabeki wa kati na kupunguza presha kwa mabeki wake kwa kuhakikisha mipira haipenyi kiurahisi kwenda eneo lao.
Mfano mzuri ni Azam ilipokosa huduma za wachezaji muhimu kama wazawa Yahya Zayd na nahodha Bajana, alichukua majukumu ya kuhakikisha hatari inadhibitiwa kabla haijafika kwenye safu ya mabeki.
ANASTAHILI MAKUBWA ZAIDI
Kutokana na kiwango chake kukua siku hadi siku na uzoefu alioupata tangu akicheza soka nje ya nchi, ni wazi siku moja atacheza timu kubwa zaidi ya Azam FC na timu nyingi za nje kuanza kumuulizia na anaweza akapata nafasi ya kucheza ligi kubwa zaidi.