Msimu wa mbio, rekodi
Muktasari:
- Haukuwa msimu rahisi kutokana na ushindani mkubwa ambapo kila timu ililazimika kuvuja jasho kujiwekea rekodi bora, lakini zingine zikajikuta zimeanguka baada ya kuvuna pointi chache zilizowaondolea nafasi ya kusalia na kuendelea na msimu mwingine.
MSIMU wa 2025-26 umetamatika juzi baada ya kila timu kukamilisha michezo yake 30 iliyotakiwa kucheza ndani ya msimu mmoja, ambapo bingwa alijulikana mwishoni mwa ligi. Yanga ilibeba taji lake la tano mfululizo, huku timu mbili zikishuka daraja moja kwa moja.
Haukuwa msimu rahisi kutokana na ushindani mkubwa ambapo kila timu ililazimika kuvuja jasho kujiwekea rekodi bora, lakini zingine zikajikuta zimeanguka baada ya kuvuna pointi chache zilizowaondolea nafasi ya kusalia na kuendelea na msimu mwingine.
YANGA UBINGWA MGUMU
Ikiwa imechukua ubingwa wa tano mfululizo, Yanga ukiwauliza ubingwa upi umewatesa basi utakuwa huu, kutokana na namna ilivyoupigania kutokana na changamoto za ubora wa kikosi chao msimu huu ulivyoishi.
Yanga haikuwa bora msimu huu kutokana na kikosi chake kupungua upana na kubaki chembamba baada ya wachezaji wengi iliosajili kushindwa kufanya vizuri na kubaki benchi, wengine wakiondolewa.
Mabingwa hao wamechukua taji hilo wakitumia wachezaji wengi waliowatumia misimu iliyopita, ambao walikuwa wamechoka kutokana na matumizi mengi, lakini walilazimika kuitetea klabu yao kutokana na kukosekana kwa chaguo jingine.
SIMBA ILIZINDUKA
Msimu huu tena Simba ilikosa kombe likienda kwa mtani wake mkubwa Yanga. Wekundu hao walianza mzunguko wa kwanza kwa uchovu mkubwa, lakini kuanzia mzunguko wa pili mambo yakabadilika baada ya kufanya vizuri kwenye usajili wa dirisha la Januari.
Simba ilishinda mechi nyingi chini ya kocha Steve Barker ambaye mchezo wake wa kwanza ulikuwa dhidi ya Mtibwa Sugar Januari 28, 2026 ambapo Wekundu hao walicheza jumla ya michezo 25, wakishinda 18, wakitoa sare saba na kukusanya jumla ya pointi 61.
Simba ndiyo timu iliyoipa Yanga presha kubwa ya ubingwa wa msimu huu, ambapo mwishoni timu hizo zilitofautiana kwa pointi mbili pekee, tofauti na msimu uliopita ambapo zilikuwa pointi nne.
BINGWA MECHI YA MWISHO
Kama ilivyokuwa msimu uliopita, msimu huu pia bingwa alipatikana kupitia mchezo wa mwisho wa ligi, na Yanga tena ikibeba taji hilo ikikimbizana na Simba waliomaliza nafasi ya pili.
Itakumbukwa msimu uliopita, kutokana na sintofahamu ya mchezo wa dabi na baadaye kupatikana suluhu, Simba na Yanga zililazimika kukutana Juni 25, 2025 ambapo Yanga ilishinda kwa mabao 2-0 na kuchukua ubingwa huo.
Msimu huu pia timu hizo zilirudia mbio hizo, zikikimbizana kwa karibu, lakini Yanga tena ikachukua ubingwa kwa kuizidi Simba kwa pointi mbili pekee, na kutwaa taji lake la tano mfululizo.
SITA ZA JUU KAMA MSIMU ULIOPITA
Ukiangalia namna msimamo wa msimu huu ulivyomalizika, utagundua jambo moja kwamba timu sita za juu zilivyomaliza ni kama ilivyokuwa msimu uliopita, zikitofautiana kwa pointi pekee.
Yanga ilimaliza kinara na pointi 75, ikipungukiwa pointi saba dhidi ya msimu uliopita ilipomaliza na pointi 82. Simba msimu huu ilimaliza na pointi 73, ikiwa imepungua pointi nne baada ya msimu uliopita kumaliza na pointi 78.
Azam ipo nafasi ya tatu msimu huu ikimaliza na pointi 64, matajiri hao wa Chamazi wakiweza kujivunia ongezeko la pointi moja baada ya msimu uliopita kumaliza na pointi 63. Singida Black Stars ilishika nafasi ya nne ikimaliza na pointi 50, wakati msimu uliopita ilimaliza na pointi 57.
TRA United nayo ilibaki nafasi ya tano na pointi 43, zikiwa zimeongezeka kwa pointi tano, baada ya msimu uliopita (wakati ikijulikana kama Tabora United) kumaliza na pointi 38. JKT Tanzania nao walibaki nafasi ya sita wakiwa na pointi 42, baada ya msimu uliopita kumaliza na pointi 36.
KMC MAPEMA SANA
KMC ndiyo ilikuwa ya kwanza kuthibitisha kushuka daraja baada ya kuwa na msimu mbovu zaidi, ikimaliza na pointi tisa pekee zilizotokana na kushinda mechi mbili na kutoa sare tatu, huku ikipoteza michezo 25 ndani ya msimu mmoja.
KMC mapema ilionesha kuwa inakabiliwa na msimu mgumu kutokana na makosa ya udhaifu wa kikosi chake yaliyotokana na usajili hafifu wa timu iliyoingia msimu huu, na sasa ni rasmi itakuwa Championship msimu ujao.
MTIBWA IMERUDI CHAMPIONSHIP
Mtibwa Sugar imeshuka tena daraja baada ya kupoteza mchezo wa mwisho ugenini kwa mabao 2-1 dhidi ya Namungo, ikimaliza msimu na pointi 27, ikipoteza mechi 15, ikishinda sita na kutoa sare tisa.
Mtibwa ilianza vizuri msimu huu lakini baadaye mabadiliko ya makocha na changamoto za kiuongozi zikaondoa utulivu wa kikosi hicho, na sasa inarejea Championship ilikocheza msimu uliopita.
Kuna maisha fulani pale Mtibwa; utakumbuka msimu uliopita ilipopanda ilipishana na ndugu zake wa damu Kagera Sugar ambayo ilikuwa inashuka Championship. Msimu huu Mtibwa inashuka huku Kagera Sugar ikirejea Ligi Kuu.
MBEYA DERBY NDANI YA PLAY OFF
Timu mbili zinazotoka jiji la Mbeya, Mbeya City na Prisons hazikuwa na msimu mzuri ambapo maisha yao yamekuwa ya hesabu kubwa kutokana na kukosa matokeo mazuri. Wanajeshi hao wa Magereza walimaliza nafasi ya 13 na pointi 32, wakati City ilimaliza nafasi ya 14 na pointi 30.
Timu hizo sasa zitalazimika kucheza mechi mbili za play off ambapo mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu, huku itakayoshindwa ikienda kukutana na Polisi Tanzania kuamua nani atapanda au kushuka.
FEI TOTO DAH!
Kiungo wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’, kwa msimu wa pili mfululizo ameikosa tuzo ya mfungaji bora akimaliza na mabao 15, akizidiwa na mshambuliaji Mosi Ndumumwe wa Singida Black Stars aliyefunga mabao 17.
Msimu wa juzi Fei Toto aliikosa tuzo hiyo baada ya kuzidiwa na Stephane Aziz Ki aliyemaliza na mabao 21, huku Fei akimaliza na mabao 19. Itakumbukwa msimu uliopita tuzo hiyo ilichukuliwa na Jean Charles Ahoua wa Simba aliyefunga mabao 16, huku Clement Mzize wa Yanga akimaliza wa pili na mabao 13.
NDUMUMWE KIBOKO
Akiwa ameichezea Singida nusu msimu tu, Ndumumwe ameweka rekodi ya kuchukua tuzo ya mfungaji bora akifunga mabao 17, jambo ambalo halikutarajiwa kabla ya raia huyo wa Burundi.
Ndumumwe pia aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza msimu huu kufunga hat trick, lakini pia akifanya hivyo mara mbili, akifungua mlango wa mabao ya aina hiyo, na baadaye kukawa na hat trick nyingine nne.
MABAO 522
Msimu huu umemalizika ukishuhudia jumla ya mabao 522 yakifungwa, ikiwa pungufu kwa mabao 50 dhidi ya yale 572 yaliyofungwa msimu uliopita. Yanga imeweka rekodi ya kuwa timu iliyofunga mabao mengi zaidi, 71, ikiwa pungufu ya mabao 12 dhidi ya msimu uliopita ilipofunga 83.
Nyuma ya Yanga kuna Simba iliyofunga mabao 54, ikiwa pungufu ya mabao 15 dhidi ya msimu uliopita ilipofunga 69.
Timu iliyofunga mabao machache zaidi msimu huu ni Mashujaa lakini ikasalia Ligi Kuu, wakati KMC iliyoshuka daraja ilimaliza na mabao 16, huku Prisons ikiwa na mabao 23.
HAT TRICK TANO
Ligi imetamatika ikizalisha hat trick tano zilizofungwa na wachezaji tofauti, wakiwemo Ndumumwe aliyepiga hat trick mbili, kiungo wa Yanga Allan Okello, Fabrice Ngoy wa Namungo na Mathew Tegisi wa Pamba Jiji.