MPAPASO WA MASAU BWIRE: Jaribo la kuokoa maisha ya staa lilivyokumbana na vikwazo

WIKI iliyopita katika safu hii ya Mpapaso nilielezea namna klabu mbalimbali za mpira wa miguu nchini zinavyoamini na kudhani ushirikina na uchawi ni moja ya njia na mbinu za kuwapatia ushindi na kuwafikisha katika mafanikio.
Nilieleza namna klabu hizo zinavyolazimika kuvunja sheria na kanuni zilizowekwa kuhakikisha wanatimiza matakwa na maelekezo ya kishirikina na uchawi waliyopewa na ‘mtaalamu’ wao wa uganga huo wa kienyeji ili wapate ushindi.
Tuliona namna ambavyo baadhi ya klabu hizo za soka, zikiwemo zile kubwa zinazoshiriki Ligi Kuu Bara wanavyofanya hadharani vitendo vya kishirikina na uchawi kwa kunyunyiza, kumwaga, kutupa na kufukia dawa viwanjani ili kuwaroga wapinzani wao na kuwawezesha wao kupata ushindi.
Wakati mwingine wanafanya uharibifu wa miundombinu ya viwanja kusudi tu watimize masharti ya kishirikina na uchawi, wanaruka ukuta, wanavunja mageti uwanjani, wakikwepa kupitia mlango ulio rasmi wakihisi kwamba timu pinzani imeweka uchawi katika lango la kuingilia na kwamba, kama wakiingia kwa kutumia lango hilo ambalo ni rasmi, watafungwa.
Hali hiyo ya ushirikina na uchawi imekuwa changamoto kubwa katika soka letu inayoidhalilisha ligi yetu, klabu na hata wachezaji wenyewe mbali na kuwepo kwa kanuni zinazokataza matendo hayo ya kishirikina na uchawi, adhabu kali kwa yeyote atakayebainika bado watu wanafanya wakiamini bila hivyo, ushindi haupatikani.
Katika mpapaso wa leo, najaribu kuonyesha namna ambavyo imani hizi za kishirikina na uchawi zimewakaa baadhi ya wachezaji, kiasi kwamba bila kuzishiriki, hawaamini kama watafanya vizuri na watafanikiwa kupitia soka. Kwa kuwa ushirikina na uchawi ndivyo vimekuwa dira kwa wachezaji wengi kwamba ndicho chanzo chao kuonekana bora kiuchezaji na kuwafikisha kwenye mafanikio, wanapoumia mchezoni au mazoezini huamini kwamba wamerogwa.
Kwa imani hizo potofu za kishirikina na uchawi, imani za kishetani, baadhi ya wachezaji wamejikuta wakiathirika pakubwa wanapopata maumivu katika maungo yao au wanapougua maradhi ya kawaida, wamekuwa wakidai wamerogwa, hivyo kukataa kutibiwa hospitali na kwenda kutibiwa kwa waganga wa kienyeji, wao wakiwaita waganga hao kwa jina la heshima la ‘wataalamu’.
Sikusema na sikutaka kusema chochote kuhusu alichoniambia aliyekuwa mchezaji wa timu yangu ya Ruvu Shooting FC, Hayati Ali Mtoni (Sonso) kuhusu ushirikina na uchawi, siku niliyompeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili kutibiwa maradhi ya mguu aliyokuwa nayo.
Nimewiwa na kulazimika kusema kupitia andiko hili, ili kuwasaidia wengine kuachana na imani hizo ambazo kwa kutojua wanadhani zinawasaidia, kumbe zinawaangamiza na kuwaua kwa haraka. Huenda wapo watakaoumizwa na haya nitakayoyasema niwaombe tu wanisamehe ili niokoe na niponye wengine wenye kuwaza hivyo.
Mchezaji Sonso nilimpenda sana alikuwa na nidhamu ya hali ya juu mno. Alipenda kuniita kiongozi, aliniheshimu kwa heshima na utii wake kwangu kama kiongozi wake nilijikuta nampenda kuliko kawaida. Nilipopata taarifa kwamba Sonso hajiwezi ni mgonjwa amelala kitandani, haraka nilimjulisha mwenyekiti wa timu, kiongozi wangu mkuu Kanali Peter Elias Mnyani nikampa msisitizo wa ukubwa wa tatizo la mchezaji wetu huyo na kwa uelewa na moyo wa upendo alionao kwa wachezaji wake, mwenyekiti alitoa maelekezo ambulance ya jeshi itolewe tukamchukue mgonjwa awaishwe Muhimbili kwa ajili ya matibabu.
Wakati taratibu za kwenda kumchukua Sonso nyumbani kwake Chamazi, Temeke jijini Dar es Salaam zikiendelea kwa uratibu wangu kama nilivyoelekezwa na mwenyekiti kwa kushirikiana na shemeji yangu, Betty Mkwasa, mke wa kocha wetu mkuu Charles Mkwasa tuliwasiliana na Hospitali ya Muhimbili, tukampata daktari bingwa ambaye alikuwa tayari kumpokea na kumhudumia hii ni baada ya kutuma picha iliyoonyesha tatizo la ugonjwa wake.
Tulipomfikisha Muhimbili mapokezi ya dharura, tulipokewa vizuri dada mmoja muuguzi aliyetupokea alionyesha upendo wa hali ya juu mno kwa Sonso, alituhudumia kwa haraka. Taratibu za mapokezi zikakamilika mapema, mgonjwa akatakiwa kupelekwa wodini.
Kabla ya kumpeleka wodini nilishauriana na muuguzi huyo aliyetuhudumia kwa upendo wodi gani tutampeleka mgonjwa wetu, nikaomba kama inawezekana apelekwe wodi la VIP. Niliondoka na muuguzi huyo hadi wodini kuwaona wahusika kuangalia uwezekano wa mgonjwa wetu kulazwa wodi hiyo. Nashukuru huko nako tulipokewa vizuri, tukafanikiwa kupata atakapolazwa mgonjwa. Nilimjulisha daktari wodi atakalolazwa mgonjwa akaniambia tukamchukue mgonjwa, yeye, daktari tutamkuta wodini.
Tulipofika eneo la dharura alipokuwa mgonjwa, mimi na muuguzi ili tumchukue tumpeleke wodini, kwa mshangao na maajabu makubwa, kijana mpendwa wangu niliyependezwa naye niliyetamani atibiwe apone haraka arudi uwanjani kucheza mpira, aligoma kwenda wodini na akakataa katakata kutibiwa hospitalini kwa madai kwamba ugonjwa alionao amerogwa ‘mtaalamu’ amekataza kutibiwa hospitalini na kwamba, hairuhusiwi kabisa sindano ya hospitali kuugusa mwili wake.
Nilijitahidi kubembeleza, kumshauri kiasi cha kuwashirikisha watu wengine kushauri, akiwemo afande mstaafu wa jeshi la polisi, Jamal Rwambow, wachezaji wa zamani na makocha wa mpira wa miguu, Boniface Pawasa na Mecky Maxime, lakini ilishindikana.
Baada ya kushauri na kubembeleza kwa muda mrefu wa zaidi ya saa nne, daktari wodini aliniuliza mbona mgonjwa haonekani. Nikiwa na majonzi mengi, nikilengwa na machozi, nilimsogelea Sonso katika kitanda alichokuwa amelazwa eneo la mapokezi ya dharura mimi na yeye tu nikamsihi sana, lakini wapi, nikamtaka aniambie kama anamfahamu aliyemroga anitajie ili kama ikiwezekana nikamuombe amsamehe amponye maradhi hayo!
“Kiongozi, mie nimerogwa zamani, tangu naichezea (anaitaja timu) aliyeniroga yupo, hachezi mpira kwa sasa na hataki nicheze mpira. Hapendi tu mafanikio yangu, niachie tu huyu mtu nitapambana naye, naenda kwa mtaalamu nitapona na yeye lazima nitamuonyesha”, aliniambia Sonso, akatoa machozi ya maumivu, nami nikajikuta machozi yananitoka!
Daktari akiwa wodini alinipigia simu, aliniuliza mgonjwa mbona haonekani, nilimsimulia kilichotokea akashauri kama yupo ndugu yake wa karibu niende naye kwake wodini amshauri kitaalamu. Alikuwepo baba mzazi wa Sonso nilienda naye, lakini bado ushauri wa daktari pia uligonga mwamba.
Itaendelea wiki ijayo