Mourinho anavyofukuzia rekodi za kibabe Ligi Kuu England
Muktasari:
- Dyche amefutwa kazi baada ya kampuni ya The Friedkin Group kukamilisha kuinunua klabu hiyo ya Goodison Park kwa Pauni 400 milioni.
LONDON, ENGLAND: JOSE Mourinho ametajwa kwenda kuchukua mikoba ya Sean Dyche huko Everton.
Dyche amefutwa kazi baada ya kampuni ya The Friedkin Group kukamilisha kuinunua klabu hiyo ya Goodison Park kwa Pauni 400 milioni.
Dyche, 53, amepigwa kibuti akiiacha Everton nafasi ya 16 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, pointi moja juu ya janga la kushuka daraja.
Na sasa, kocha wa zamani wa Chelsea, Mourinho huenda akapewa mikoba hiyo - licha ya kwamba alifutwa kazi na Dan Friedkin mwaka mmoja uliopita.
Friedkin pia ni mmiliki wa AS Roma ya Italia ambaye alimfuta kazi Mourinho baada ya timu kupata matokeo ya hovyo.
Mourinho alikwenda kujiunga na Fenerbahce miezi mitano baadaye, lakini kinachoelezwa ni kwamba hafurahishwi na maisha ya Uturuki anafikiria kuhama.
Oktoba mwaka jana, kocha huyo alitoa ujumbe kwa timu za Ligi Kuu England kwenda kumchukua baada ya kufanya hivyo kwenye michuano ya UEFA.
Kama Mourinho atanaswa na Everton na kukubali kwenda kuinoa timu hiyo basi ataingia kwenye kundi la makocha ambao wamewahi kufanya kazi kwenye timu tofauti zinazoanzia nne na kuendelea...
David Moyes - klabu 4
Moyes ni mmoja wa makocha mahiri kwenye Ligi Kuu England. Aliinoa Everton kwa miaka 11 huko Goodison Park, ambako alianzia kazi kabla ya kupewa kibarua cha kwenda kurithi mikoba ya Sir Alex Ferguson huko Manchester United. Kwenye timu hiyo ya Old Trafford alidumu miezi tisa kabla ya kutimkia Hispania kujiunga na Real Sociedad.
Alirudi England kuinoa Sunderland, Julai 2016 kabla ya kukubali mikoba ya kuinoa West Ham United, ambayo aliipa ubingwa wa Europa Conference League 2023 na mwaka uliofuata akaondoka. Kwa sasa hana timu kocha huyo anafikiriwa na Everton.
Rafa Benitez - Klabu 4
Kocha huyo Mhispaniola ameingia kwenye rekodi ya kuzinoa klabu zote mbili za Merseyside, Everton na Liverpool.
Mafanikio makubwa zaidi aliyapata 2005 alipoiongoza Liverpool kushinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kupindua meza dhidi ya AC Milan kwenye fainali.
Lakini, kwenye klabu za England, Benitez aliwahi kuzinoa pia Newcastle na Chelsea na hivyo kumfanya kuwa kwenye orodha ya kocha aliyefanya kazi na klabu nne tofauti Ligi Kuu England.
Mara ya mwisho alikuwa Celta Vigo kwa miezi 10 kabla ya kufukuzwa kazi Machi 2024.
Claudio Ranieri - Klabu 4
Mtaliano huyo aliweka rekodi ya kibabe aliponyakua taji la Ligi Kuu England akiwa timu isiyodhaniwa na wengi ya Leicester City.
Ranieri alibeba taji hilo msimu wa 2015-16 baada ya kikosi kuonyesha uborkwelikweli uwanjani kilipokuwa na huduma ya wakali kadhaa akiwamo kiungo N’Golo Kante na straika Jamie Vardy.
Lakini, kwenye kikosi hicho cha King Power, Ranieri alifutwa kazi mwaka uliopita baada ya Leicester kuanza kuporomoka kwenye msimamo. Ranieri, 73, alizonoa pia Chelsea, Fulham na Watford kwenye Ligi Kuu England.
Steve Bruce - Klabu 5
Mwamba mwingine kwenye Ligi Kuu England, Steve Bruce aliyewahi kuzinoa klabu tano tofauti.
Kwa ujumla wake, Bruce ameshuhudia mechi 477 akiwa kocha kwenye mechi za ligi hiyo, huku akipita Newcastle United, Hull City, Sunderland, Wigan Athletic na Birmingham City.
Kocha huyo ni mmoja wa manguli kwenye Ligi Kuu England na amekuwa na heshima. Kwa sasa, Bruce, 64, anainoa Blackpool, ambapo alichukua mikoba kwenye kikosi hicho mwaka jana.
Harry Redknapp - Klabu 5
Moja ya vipenzi vikubwa kwenye soka la England ni Harry Redknapp, ambaye ameshuhudia mechi 642 akiwa kocha kwenye Ligi Kuu England.
QPR, Tottenham, Portsmouth, Southampton na West Ham United ni miongoni mwa klabu alizozinoa kabla ya kuamua kustaafu 2017.
Baada ya kuachana na soka, Redknapp aliingia kwenye mashindano ya shoo za televisheni ya ‘I’m A Celebrity Get Me Out of Here!’ Aliibuka kuwa mshindi aliponyakua taji la King of the Jungle 2018.
Kwa sasa amekuwa akitumika kama mshauri klabu ya Bournemouth inayoshiriki Ligi Kuu England.
Mark Hughes - Klabu 6
Mark Hughes ameweka rekodi ya kunoa klabu sita tofauti kwenye zama za Ligi Kuu England.
Kocha huyo, ambaye pia alitamba enzi zake alipokuwa mchezaji kwenye Ligi Kuu England, kwenye kazi yake ya ukocha alizinoa Southampton, Stoke City, QPR, Fulham, Manchester City na Blackburn Rovers na hivyo kumfanya awe kwenye mikikimikiki hiyo ya Ligi Kuu England kwa miaka 12.
Kibarua chake alichodumu kwa muda mrefu zaidi ilikuwa Stoke City, ambapo aliinoa timu hiyo kwa miaka mitano baada ya kutua kwenye timu hiyo mwaka 2013. Ni mmoja wa makocha wenye hadhi kubwa.
Roy Hodgson - Klabu 6
Roy Hodgson kazi yake ya ukocha kwenye Ligi Kuu England kwa hivi karibuni alikuwa huko Crystal Palace, ambapo aliachana na timu hiyo Februari mwaka jana baada ya kufikisha mechi 200 kwenye timu hiyo.
Alikuwa kwenye hatari ya kufukuzwa kazi kwenye timu hiyo ya Selhurst Park kabla ya kuamua mwenyewe kung’atuka na kustaafu. Hodgson, 77, aliwahi kuzinoa pia Watford, West Brom, Liverpool, Fulham na Blackburn Rovers kwenye Ligi Kuu England.
Ukiweka rekodi zake tamu kwenye klabu za Ligi Kuu England, Hodgson aliwahi kuwa kocha wa timu ya taifa ya England kwa miaka minne kabla ya kuondoshwa 2016.
Sam Allardyce - Klabu 9
Kocha aliyenoa timu nyingi zaidi kwenye Ligi Kuu England ni Sam Allardyce, akipita kwenye klabu tisa tofauti.
Kocha huyo maarufu kama Big Sam anashikiria rekodi pia ya kuwa kocha aliyedumu kwa muda mfupi zaidi kwenye klabu ya Ligi Kuu England, siku 30 huko Leeds United mwishoni mwa msimu wa 2022-23.
Big Sam, 70, aliteuliwa kwa muda kuinoa timu hiyo, lakini alishindwa kuinusuru isishuke daraja na hivyo ikaibukia kwenye Championship.
Timu nyingine alizowahi kuzinoa ni West Brom, Everton, Crystal Palace, Sunderland, West Ham, Blackburn, Newcastle na Bolton. England aliinoa kwa siku 67 tu.
Makocha wengine
Kwenye orodha hiyo, makocha wengine walionoa klabu kuanzia nne tofauti kwenye Ligi Kuu England ni Chris Hughton (Newcastle, Birmingham, Norwich na Brighton), Ron Atkinson (Nottingham Forest, Sheffield Wednesday, Coventry City na Aston Villa), Neil Warnock (Sheffield United, Cardiff, Crystal Palace na Queens Park Rangers), Graeme Souness (Liverpool, Southampton, Blackburn na Newcastle), Marco Silva (Fulham, Everton, Watford na Hull City), wakati Alan Pardew amezinoa klabu tano (West Brom, Crystal Palace, Newcastle, Charlton na West Ham).