Moto wa Simba balaa tupu!

Muktasari:

MABAO mawili ya Chris Mugalu na jingine la Luis Miquissone juzi dhidi ya Dodoma Jiji FC kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, yalitosha kuifanya Simba iboreshe rekodi yake ya kutopoteza idadi kubwa ya mechi mfululizo katika Ligi Kuu kufikia michezo 18.

MABAO mawili ya Chris Mugalu na jingine la Luis Miquissone juzi dhidi ya Dodoma Jiji FC kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, yalitosha kuifanya Simba iboreshe rekodi yake ya kutopoteza idadi kubwa ya mechi mfululizo katika Ligi Kuu kufikia michezo 18.

Tangu Oktoba 25, 2020 Simba ilipofungwa na Ruvu Shooting kwa bao 1-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, imeshinda katika mechi 15 na kutoka sare tatu, ikifunga mabao 42 na kuruhusu nyavu zake zitikiswe mara sita.

Hata hivyo, ushindi wa juzi dhidi ya Dodoma Jiji FC haukuja kirahisi na Simba walilazimika kufanya kazi ya ziada ndani ya uwanja kuupata kutokana na ushindani ulioonyeshwa na wapinzani wao katika dakika 90 za mchezo huo.


Ubora uliamua mchezo

Dodoma Jiji walionekana kujiandaa vyema kimbinu kuikabili Simba na kulianza kuwepo dalili za wao kuvuna pointi katika mchezo huo kwa namna walivyocheza katika kipindi cha kwanza ambapo walijilinda vyema na kushambulia mara kadhaa kwa kushtukiza na wakafanikiwa kupata bao moja ambalo lilikuwa la kusawazisha likifungwa na Cleoface Mkandala katika dakika ya 29.

Hali ilikuja kubadilika katika kipindi cha pili hasa baada ya Simba kufanya mabadiliko ya kumtoa Mzamiru Yassin na kumuingiza Bernard Morrison ambaye kuingia kwake kuliiongezea kasi Simba katika kushambulia tofauti na ilivyokuwa mwanzoni na ikaweza kupata mabao mawili katika dakika hizo 45 za mwisho.

Kikubwa kilicholeta utofauti katika mchezo huo wa juzi ni ubora binafsi wa wachezaji wa timu hizo mbili, ambapo wale wa Simba walionekana kuwa wabunifu zaidi katika kuvunja ukuta wa Dodoma Jiji ambao walijaza idadi kubwa ya wachezaji pindi walipokuwa wanajilinda.


Mugalu akoleza vita ya ufungaji

Kitendo cha mshambuliaji Chris Mugalu kufunga mabao mawili katika mchezo wa juzi, kimefanya ushindani katika chati ya ufungaji kuwa mkali sio tu ndani ya Simba, bali pia katika Ligi Kuu Bara msimu huu.

Mabao hayo yamemfanya Mugalu kushika nafasi ya tatu katika chati ya ufungaji ndani ya Simba na pia kwenye orodha ya wanaosaka zawadi ya ufungaji bora Ligi Kuu msimu huu, yupo katika nafasi ya tano na mabao yake nane, akizidiwa kwa mabao manne tu na kinara, Prince Dube wa Azam FC.


Utulivu uliwaangusha Dodoma Jiji

Licha ya Simba kutengeneza idadi kubwa ya nafasi za mabao katika mchezo huo, Dodoma Jiji nao walipata chache ambazo kama wangezitumia vizuri, pengine wangeweza kuwashangaza Simba katika mchezo huo.

Washambuliaji wake Seif Karihe na Dickson Ambundo walionekana kukosa umakini pindi walipokaribia lango la Simba na kujikuta wakipoteza kirahisi mipira ya mwisho ama kwa kupiga mashuti yaliyotoka nje au hafifu ambayo yaliokolewa au kuporwa mipira kirahisi na wachezaji wa Simba.


Manula kajinyima rekodi

Ilikuwa ni fursa nzuri kwa Aishi Manula kuweka rekodi ya kuwa kipa aliyecheza mechi nyingi mfululizo bila kuruhusu bao, lakini kosa alilofanya la kuutema mpira wa kona iliyochongwa na Dickson Ambundo miguuni mwa Mkandala lilimgharimu baada ya kiungo huyo wa Dodoma Jiji FC kuukwamisha wavuni.

Kabla ya bao hilo, Manula alicheza mechi nne mfululizo bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa ambazo ni dhidi ya timu za Gwambina, Kagera Sugar, Mwadui na Mtibwa Sugar.


Chama hana mpinzani

Ni wazi kwamba Clatous Chama ni mchezaji wa aina yake ambaye Ligi Kuu Tanzania Bara imebahatika kumpata katika miaka ya hivi karibuni.

Pasi mbili za mabao aliyopiga kwa Luis Miquissone na Chris Mugalu zimemfanya atimize pasi za mabao 13 kwake msimu huu ambayo imemfanya avunje rekodi yake ya msimu uliopita ambao alipiga jumla ya pasi 12 za mwisho. Ikumbukwe Chama pia msimu huu amepachika mabao saba kwenye Ligi Kuu tofauti na msimu uliopita ambao alifunga jumla ya mabao mawili.


Upana wa kikosi unaibeba Simba

Katika mchezo wa juzi, Simba haikuwakutumia Meddie Kagere, Lwanga Taddeo na Joash Onyango ambao nafasi zao zilichukuliwa na Kennedy Juma, Erasto Nyoni na Chris Mugalu.

Hata hivyo haikuonekana kucheza tofauti na ilivyozoeleka kwani ilitawala mchezo kwa muda mrefu na ilitengeneza idadi kubwa ya nafasi za mabao pamoja na kupata ushindi mnono ambao umewafanya wazidi kujiimarisha kileleni wakifikisha jumla ya pointi 61, nne mbele ya Yanga walio katika nafasi ya pili.


Makocha wafunguka

Kocha wa Simba, Didier Gomes alisema amefurahishwa kupata ushindi katika mchezo wa juzi hasa ukizingatia wamecheza mechi nyingi ndani ya muda mfupi.

“Ni jambo zuri kuzidi kuongeza tofauti ya alama dhidi ya wanaotufuata katika msimamo, wachezaji wangu wamefanya kazi kubwa hadi kufikia hapa,” alisema Gomez.

Kocha wa Dodoma Jiji, Mbwana Makatta alisema kuwa timu yake ilipoteza kutokana na kupoteza umakini.

“Mechi ilikuwa ni nzuri na tumemaliza tukipoteza kwa mabao 3-1. Kipindi cha kwanza tumecheza kwa nidhamu nzuri na kuziba mianya yote na kushambulia kwa kutumia mashambulizi ya kushtukiza.

Kipindi cha pili tulipoteza umakini, kikubwa niwapongeze Simba kwa kushinda,” alisema Makatta.