Morrison pasua kichwa

KAMA ikitokea nyota wa Yanga, winga Bernard Morrison akaondoka nchini ataacha mengi ya kukumbukwa.

Wamepita mastaa wengi wa kimataifa wanaokumbukwa lakini kwa Morrison ni mchezaji ambaye mbali na ufundi wake uwanjani, alikuwa na vituko nje na ndani ya uwanja.

Alirejea Yanga akitokea Simba na usajili wake ulishtua kwani hakuna aliyeamini tukio hilo na kuitumikia timu ya Wananchi hadi sasa na mkataba wake unafikia rasmi mwisho leo Jumatano na kuna tetesi huenda asiongeze mwingine.

Hata hivyo, Kocha Nasreddine Nabi na baadhi ya viongozi wanakiri ni bonge la mchezaji. Ishu yake ya kusalia Jangwani inaonekana kukaa vibaya ingawa lolote linaweza likatokea.

Ikumbukwe Morrison ndiye aliyefunga bao la pili Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Marumo ya Afrika Kusini, Uwanja wa Benjamin Mkapa na hapo ndipo ilipoanzia safari ya kutinga fainali za CAF, kwenye michezo yote ya mwishoni kaonyesha uwezo wa juu haswa.

Ana bahati ya mataji. Alibeba kombe la Ligi Kuu akiwa na Simba msimu wa 2020/21, baada ya kurejea Yanga 2022/23 na kubeba tena.

Kikubwa kinachoonekana kupasua vichwa viongozi wa Yanga ni vituko vyake vya mara kwa mara na Mwanaspoti linakukusanyia matukio aliyoyafanya msimu mzima uliopita.


VITUKO, UTUNDU IKULU

Kwa sasa ameshazoeleka na wengi. Mirrison amekuwa na vituko sana nje na ndani ya uwanja na kuna baadhi vinampandisha na kumshusha hadhi yake.

Moja ya tukio kubwa alilolifanya ni Juni 5, Yanga ilipoalikwa Ikulu kwenda kula chakula cha jioni pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan, wakati Injiania Hersi Said (rais) anatoa utambulisho wa klabu hiyo kuweka historia ya kuchezesha kijana mdogo zaidi kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Clement Mzize, Morrison alisimama na kupungia watu mikono kama utambulisho ulimuhusu yeye na kusababisha ukumbini watu kuangua vicheko.

Wakati Morrison anatambulishwa na kutakiwa kusimama aligoma, jambo lililowafanya waliokuwepo eneo hilo kuangua tena kicheko, ingawa kwa wengine ilikuwa aibu.


KUMVALISHA MEDALI AHMED ALLY

Morrison alifanya tukio lingine siku hiyo Ikulu, alikwenda hadi alipokuwa amekaa meneja wa Habari na Mawasilino wa klabu ya Simba, Ahmed Ally kisha akamkumbatia na kumvalisha medali ya CAF, huku akicheka jambo lililowafanya watu wengi waliokuwa wamejazana hapo Ikulu kucheka.


PESA ZA WAZIRI

Jun 2, Alipo Morrison hapawezi kukosekana kicheko, wakati Waziri wa Michezo Pindi Chana alipofanya kikao cha kuihamasisha Yanga nchini Algeria siku moja kabla ya timu hiyo kucheza fainali dhidi ya wenyeji wao USM Alger, staa huyo alifanya kituo cha mwaka.

Wakati waziri huyo anawaambia wachezaji wa Yanga wanaweza kuchukua ubingwa wanatakiwa kupambana bila kuogopa, kuna mtu aliguswa maneno hayo akamtunza kiwango kadhaa cha Dola, Morrison alinyanyuka haraka alipokuwa amekaa na kuzichukua kisha kuziweka mfukoni kwake, kitu kilichofanya makocha, viongozi na wachezaji wenzake kucheka na kumshangaa alipata wapi ujasiri huo, hata hivyo waziri naye alicheka na kuendelea na hotuba yake.


KUGOMEA SABU

Mambo yasiyowezekana kwa wachezaji wengine kwa Morrison ni tofauti kabisa, Wakati Yanga ilipocheza dhidi ya Dodoma Jiji ikashinda mabao 4-2, Mei 13 Uwanja wa Azam Complex, Kocha Nasreddine Nabi alifanya mabadiliko ya kumtoa Mghana huyo ili aingie Clement Mzize lakini akagomea sabu kama dakika kadha akionyesha yeye hatakiwi kutoka kisha akatoka nje kwa hasira, hata hivyo Nabi alionekana kukasirishwa na jambo hilo.


AINGILIA MAHOJIANO YA NAHODHA

Mei 31, Uwanja wa Avic Town, wakati nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto aliulizwa kuhusu maandalizi ya mechi ya pili ya fainali dhidi ya USM Alger, ghafla Morrison aliibuka mbele ya kamera alipoambiwa wanafanya mahojiano, akauliza mmeanza wakajibu ndio, kilichofuata ni hiki.

Japokuwa Kiswahili cha Morrison hakijanyooka alisema: “Gaizi tusikate tamaa, tutashinda kule iwe kuchukua ubingwa au la.”

Lakini jambo kama hilo alilifanya tena wakati timu ilipokuwa inarejea kutoka Mbeya kwenye mchezo wa mwisho wa ligi na walikuwa kwenye paredi maalum la kushangilia ubingwa, kituo cha Azam TV kilikuwa kinafanya mahojiano ya moja kwa moja na Fiston Mayele, lakini wakiwa katikati Mghana huyo aliibuka na kuondoa kipaza sauti na kumwambia mwandishi: Inatosha sasa.


AISIMAMISHA MSIMBAZI

Morrison ni mchezaji mwenye vaibu kubwa, wakati gari maalumu lililowabeba wachezaji wa Yanga likitokea Uwanja wa ndege, lilisimama Msimbazi karibu na jengo la Simba na Morrison alishuka chini na kuanza kucheza na mashabiki.

Baada ya mabaunsa wa Yanga kuona usalama ni mdogo kwake wakamshika na kumrudisha kwenye gari.

Pia kuna picha zilizokuwa zinamuonyesha amekamatwa na askari, ikidaiwa alikataa gari lake kukaguliwa na baadaye akapelekwa kituo cha polisi cha Oysterbay kisha akaachiwa.

Aziz Ki ni kati ya wachezaji wa Yanga walionja joto ya jiwe ya vituko vya Morrison alionekana akiwa naye ndani ya gari, akimrekodi akiwa amelala kisha akamshtua na kuanza kumcheka, video hiyo ilitamba sana kwenye mitandao ya kijamii.